Ajifungua pacha wa kike walioungana kifua, tumbo
Musoma. Mwanamke mmoja mkazi wa Kata ya
Buhare, Manispaa ya Musoma mkoani Mara, Helena Paulo (20), amejifungua
watoto pacha wa kike walioungana eneo la kifuani hadi tumboni wakiwa na
uzito wa kilo 4.6 kwa pamoja.
Tukio hilo la ajabu katika Mji wa Musoma na
mkoa kwa jumla, liliwavutia hisia za wananchi hali iliyosababisha
msongamano katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa madhumuni ya kutaka
kushuhudia.
Akizungumza katika wodi ya wazazi
hospitalini hapo, muuguzi wa zamu, Naabu Geraruma alisema mwanamke huyo
alijifungua juzi saa saba usiku kwa njia ya upasuaji.
Geraruma alisema tukio hilo ni la kwanza
katika hospitali hiyo na hali ya afya ya mzazi huyo na watoto inaendelea
vizuri na muda wowote atahamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando,
Mwanza.
Kwa upande wake, Mganga wa Idara ya
Magonjwa ya Wanawake, Dk Simon Kamuli alisema baada ya jitihada za
kuhakikisha mwanamke huyo anajifungua salama kukamilika, kinachofuatia
ni kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa uangalizi zaidi.
Alisema kuwa hospitali ya mkoa haina
uwezo wa kuwafanya chochote watoto hao, ikiwamo kuwatenganisha na
taratibu zingine kabla ya uchunguzi wa kina.-MWANANCHI
Comments
Post a Comment