UCHAGUZI WA MARUDIO: KATIBU WA MBUNGE AJERUHIWA VIBAYA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo wilayani Iringa kimelalamikia rafu na
kasoro mbalimbali zilizojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa
uliofanyika Disemba 14 na kusema kuwa uchaguzi huo uligubikwa na kasoro
nyingi ambapo wakati uchaguzi huo wa marudio ukiendelea hapo jana,
watu wasiojulikana wamemshambulia kwa nondo na mapanga katibu wa mbunge
wa Iringa mjini Bwana Joseph Mgima.
Akizungumza kwenye mahojiano na mwandishi wetu, Bwana Mgima amesema
tukio hilo lilitokea usiku wa juzi majira ya saa Mbili usiku wakati
alipokuwa akienda kuzungumza na mawakala wa chama chake kwenye mtaa wa
Bwawani kata ya Mkwawa ndipo alipokutana na watu hao waliokuwa kwenye
bajaji mbili ambapo mmoja wa watu hao alimpiga teke na kuangukia mtaroni
ndipo watu wengine Sita kutoka kwenye hizo bajaji walipoanza kumpiga
kwa mapanga.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la CHADEMA wilaya ya Iringa Leonce Marto
amesema tukio hilo linauhusiano mkubwa na uchaguzi wa marudio wa
wenyeviti na wajumbe katika mitaa 19 katika manispaa ya Iringa
akiwatuhumu wapinzani wao wa CCM kutumia mbinu chafu kushinda kwenye
mitaa hiyo huku kamanda wa polisi mkoani Iringa Ramadhani Mungi akisema
jeshi hilo linachunguza tukio hilo na litawashughulikia wote
watakaobainika kufanya uhalifu huo.
Zoezi la uchaguzi limefanyika jana ikiwa ni marudio baada ya baadhi ya
maeneo katika mitaa ya manispaa ya Iringa kushindwa kufanya uchaguzi huo
kutokana na kasoro mbalimbali zilizojitokeza ikiwemo kukosekana kwa
baadhi ya vifaa ambapo jumla ya mitaa 10 imerudia kuchagua wenyeviti wa
mitaa na wajumbe wao na mitaa mingine 9 imerudia uchaguzi wa wajumbe
baada ya wajumbe hao kugoma kwa idadi ya kura.
Comments
Post a Comment