JE! WAJUA KUWA WEWE UNAWEZA KUWA MCHAWI WA MAHUSIANO/MAPENZI YAKO?


WATU wanaamini mno katika uchawi. Wanamaliza fedha kwa waganga wa kienyeji wakiamini kwamba wamerogwa, hivyo wanatafuta ufumbuzi kutoka kwa wataalamu wa mambo ya asili. Wapo wanaoita mambo ya Kiswahili.
Kwangu napinga kuita hivyo kwa sababu nami ni Mswahili na kwa uzoefu wangu, sisi Waswahili hatuna utamaduni wa kutegemea mitishamba kuamua hatma za uhusiano wetu wa kimapenzi.

 Ila baadhi wapo, tena wengi haswaaa!
Shika hili kwamba wewe mwenyewe pengine ndiye mchawi wa mapenzi yako. Hujiulizi kwa nini wengine wanadumu? Ni vipi wenzi wengine wanaheshimiana? Inakuaje kwako imekuwa kinyume? Siyo suala la upepo, wakati mwingine ni kujitakia.
Kivipi mwenzi wako hakuheshimu? Ni makosa gani ambayo wewe umefanya? Ukishapata majibu ya maswali hayo, utaweza kujua faida za wewe kujitambua. Nakuasa ushike moja kuu kwamba mapenzi ni nidhamu.
Yapo kama kioo, ukiyaheshimu nayo yatakuheshimu na utayaona murua. Endapo utayachukulia kwa mzaha, nayo hayatasita kukufanyia mzaha. Mwisho utakuja kugundua kwamba yanakutesa, ukifika hapo usiache kukumbuka nawe ulivyoyatesa.
Baadhi ya watu wanaamini mazoea ndiyo yanasababisha mapenzi kupungua au kuchokana. Hilo siyo kweli hata kidogo, tena nakataa kwa herufi kubwa kwa sababu wapo mabibi na mababu waliopendana tangu enzi hizo mpaka hivi sasa
.
Mapenzi ni kitu tofauti sana kwenye hii dunia na hata nje ya sayari, husababisha mambo kwenda sawa au kuharibika, kuna baadhi ya vifo hutokana na mapenzi, kuna magonjwa watu nwanaumwa kisa mapenzi.
Ukipata mpenzi anayekuelewa, anakujali na anakupenda, hata dunia iwe ya tabu kwako kwa kiasi gani, utaiona inasogea kama kawaida na maisha yanaendelea vizuri tu, naamini hapo unakubaliana na mimi.
Lakini ukiumizwa kwenye mapenzi au kutopata mtu wa kukujali, kutosikilizwa basi hata kama dunia kwako ina raha, utaiona ni chungu na kama kwako dunia ni chungu tangu awali halafu ukaja kuumizwa, ndio hapo watu wanapowaza na kufikiria kujiua kwa sababu haoni hata umuhimu wa yeye kuishi.


Baadhi ya sababu zinazoweza kufanya mapenzi kupungua au mwenza wako kubadilika ni hizi;

1. KUTOSEMA KWELI
Katika mapenzi uongo ni kitu kibaya sana, uongo wa aina yoyote ile ni mbaya katika mahusiano yoyote yale na huweza kupunguza mapenzi ya dhati na uaminifu kwa kiasi kikubwa hasa kama mmojawapo atagundua kuwa mwenzi wake ni muongo, anamdanganya.
Wapo ambao wakigundua mpenzi wake ni muongo wanauliza au kuongea nao ambacho ni kitu kizuri na siku zote napenda sana kusisitiza suala la wapenzi kujadili vitu mbalimbali vinavyotokea kwenye mahusiano yao, lakini wengine wanaamua kunyamaza au kuacha kabisa.

2. KUTENGENEZA PENZI LA PEMBENI

Moja ya jibu nililolipata kwa watu wengi niliojaribu kujadiliana nao mada hii walisema kuwa, mahusiano mengine yanasababisha mapenzi kupungua, inaumiza sana kugundua yule unayempenda kwa dhati ana mpenzi/wapenzi wengine. Kubali au kataa, hii ni moja ya sababu kubwa zinazofanya mapenzi kupungua au kuvunjika kabisa.
Kamwe usimuumize moyo akupendaye kiukweli, usimfanye ajutie penzi lako,usimfanye anung’unike kwa unayomtendea, ipo siku utahitaji mapenzi ya kweli kwa mwingine na hutayapata, ukimuumiza ipo siku nawe utaumia, mapenzi ya kweli yanawezekana kama kunakuwa na uaminifu.

3. UPUUZI
Hii pia huchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza mapenzi kama sio kuyamaliza kabisa. Unapokuwa kwenye uhusiano jitahidi kumpenda mtu wako kwa hali yoyote na usiwe na dharau kwake au hata kwa marafiki zake au ndugu zake au hata wengineo. Hakuna mtu anayependa mtu mwenye dharau hata awe nani. Hata kama mwenzi wako ana uwezo mdogo kuliko wewe, hiyo isiwe sababu ya wewe kumdharau.

4.MSEMA HOVYO
Hakuna kitu kinachoweza kumfanya mwenza wako kukukimbia au hata kukosa uaminifu na wewe kama akija kugundua wewe ni mropokaji na huna ‘kifua’ hasa kwa yale mambo ambayo ni ya chumbani na hayakutakiwa kutoka nje. Hakuna mtu anayependa siri zake kutoka hadharani na huwa inaumiza sana kwenye mapenzi kumpa mtu siri zako halafu yeye anaenda kusimulia.
Mambo mnayafanya mkiwa wawili tena ndani lakini kesho unaenda kusimulia kwa watu, si jambo la busara hata kidogo.


NINI MAONI YAKO? USISITE KULIKE UKURASA WETU ILI KUPATA HABARI ZAIDI

Comments

Popular posts from this blog