ZSTC yastawisha upya zao la karafuu, Zanzibar.
Zanzibar
ni visiwa vinavyosifika kwa uzalishaji wa karafuu bora duniani. Katika
miaka 30 ya nyuma pia ilisifika kwa uzalishaji karafuu nyingi, wastani
wa tani 8,605 zilikuwa zikizalishwa kwa mwaka.
Jamii ya
wakati huo walikuwa wakizijali, wakizithamini na wakizipenda sana
karafuu ukilinganisha na kizazi cha sasa. Walihakikisha karafuu zao
wakiuza vituoni tena zinakuwa safi, zimekauka vizuri na zinapata daraja
la kwanza.
Katika
miaka hiyo zao la karafuu lilikuwa ndiyo tegemeo kubwa la pato la
kiuchumi katika visiwa vya Zanzibar. Pato la Serikali lilitegemea sana
zao hilo na kuiwezesha kuenedesha mipango yake ya kiuchumi na kijamii
bila ya kuyumba. Hali hiyo ilitokana na ukubwa wa soko la dunia na ubora
wa kipekee wa karafuu za Zanzibar katika soko hilo.
Lakini
kwenye miaka ya 1990, hali ya soko haikuwa nzuri sambamba na kushuga kwa
bei na kuongezeka kwa nchi zinazozalisha karafuu duniani na hivyo
kuleta ushindani wa kibiashara.
Kushuka
kwa bei katika soko la dunia kulipelekea kushuka kwa ari ya uzalishaji
kwa wakulima na kupelekea visiwa vya Zanzibar navyo kupoteza muelekeo wa
zao hili. Zao hili lilipoteza hadhi yake ya kuwa zao la uchumi wa nchi.
Wakulima
wengi waliacha kulima zao la karafuu na badala yake walijihughulisha na
mazao mengine ukiwemo ukulima wa mwani ambapo wakati huo ulionekana
kama ungelikuwa mbadala wa zao la karafuu.
Lakini
pamoja na kuyumba kwa soko la dunia, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
iliendelea kununua karafuu kutoka kwa wakulima, ingawa si kwa bei ya
kiwango cha juu. Serikali ililazimika wakati mwengine kufidia gharama za
bei katika kuona mkulima ambaye ni mwananchi anaendelea kujenga imani
na kulithamini zao la karafuu.
Wanafalsafa
ya kiswahili wanao msemo usemao baada ya dhiki faraja, hivyo ndivyo
ilivykuwa kwa wakulima wa karafuu baada ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, kupandisha bei ya zao hili kufuatia kutengemaa kwa hali katika
soko la dunia mwaka 2011.
Serikali
iliamua kupandisha bei hadi kufikia shilingi 15,000 kwa kilo kabla ya
kushuka kidogo kutokana na kutegemea kupanda na kushuka kwa bei katika
soko la dunia.
Aidha
katika mwaka 2011 ZSTC ilimeongeza bei ya karafuu kutoka 3500/- hadi
10000/- na baadae kuongezwa tena hadi 14,000/- kwa kilo. Mkulima
analipwa asilimia 80 ya bei inayouzwa nje ya nchi.
Baada ya
Serikali kuliimarisha Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC), hali ya
ustawishaji wa zao la karafuu ilianza kurejea na wakulima walianza tena
kulistawisha zao hilo. Mtazamo chanya wa ZSTC kwa kiasi kikubwa umeweza
kurudisha hadhi ya zao la karafuu ya Zanzibar kuanzia kwa wakulima na
hata katika soko la dunia.
ZSTC
chini ya Mkurugenzi Muendeshaji Bi. Mwanahija Almas Ali imekuwa mstari
wa mbele hivi sasa kuhakikisha hadhi ya karafuu ya Zanzibar inarejea
katika sifa yake ya asili kwa kushirikiana na wadau wa zao hilo wakiwemo
wakulima.
Kiujumla,
karafuu ni zao pekee la kilimo ambao linaiingiza fedha nyingi za
kigeni, ambapo serikali imetoa kipaumbile kwa zao hilo katika kukuza
uchumi Zanzibar pamoja na ustawi wa wananchi wake.
Jitihada
kubwa zinachukuliwa na serikali katika kuhakikisha kiwango cha
uzalishaji, usafirishaji na ubora wa karafuu za Zanzibar unaimarika kwa
kushirikina na wadau wote wa zao hili wakiwemo wakulima, wafanya
biashara, Serikali za Wilaya na Mikoa na Taasisi za ulinzi na usalama.
Miongoni
mwa mambo ambayo yaliofanywa na serikali katika jitihada za kuimarisha
zao la karafuu ni pamoja na kuongeza bei ambapo mkulima anapata asilimia
80% ya bei inayouziwa karafuu nje ya nchi.
Kutoa
miche bure kwa wakulima ili kuongeza idadi ya miti ya mikarafuu visiwani
sambamba na kujengwa vituo karibu na maeneo ya wananchi kwa kurahisisha
usafirishaji wa karafuu kutoka sehemu waliopo hadi vituoni.
Kuanzisha
mpango wa kuifanya karafuu ya Zanzibar ijulikane dunia nzima kutokana
na sifa zake za kipekee kupitia mradi wa tasnia bunifu (BRANDING).
Kuifanya karafuu kuwa chini ya umiliki wa serikali kwa lengo la
kumjengea mkulima uwezo wa kimaslahina kumuongezea ari ya kulipenda zao
la karafuu.
Kujenga
vituo vipya vya manunuzi karibu na wakulima ili kurahisisha shughuli za
usafirishaji wa karafuu mfano hivi sasa Pemba kuna vituo zaidi ya 30 na
Unguja kuna vituo zaidi ya sita ingawa hivi sasa Unguja kituo
kinachofanyakazi ni kimoja kilichokuwepo tangu miaka ya zamani, tofauti
ni kwamba kituo cha zamani kwa Unguja kilikuwepo Malindi na cha hivi
sasa kipo Saateni.
Kuongeza
idadi ya vituo ni moja ya juhudi za Serikali kuwapunguzia gharama za
usafiri wananchi wake pamoja na kuwaondolea usumbufu ambao sio wa
lazima.
Kuanzisha
vituo vya uatikaji miche ya mikarafuu, kununua miche ya mikarafuu
kutoka kwa wakulima walioanzisha vituo na kupatiwa bure miche hio
wakulima. Kila mwaka zaidi ya miche 1,000,000 inazalishwa na kugaiwa
bure kwa wakulima. Jitihada hizi zimeanza zamani na bado zinaendelea.
Karafuu
za Zanzibar zina sifa kubwa duniani ukilinganisha na karafuu
zinazozalishwa na nchi nyengine ambazo zinazalisha kwa wingi zaidi
ukilinganisha na Zanzibar.Sifa hiyo inahitaji kulindwa , Serikali hivi
sasa imeandaa mkakati wa kuilinda karafuu ya Zanzibar mkakati ambao
utawakwamisha wale wote watakaojaribu kuharibu sifa hiyo.
Sifa
nzuri za kiwango cha juu cha kipekee cha karafuu ya Zanzibar ni ukaukaji
wake, usafi wake ladha yake na haiba yake ya kimaumbile ambapo viwango
hivi vinafahamika katika soko la dunia tangu miaka 50 iliyopita na
vinaendelea kutumika hadi hii leo.
Sifa hiyo
ya karafuu inajengwa na wadau wote wenye kujishughulisha na zao hili,
hivyo haitokuwa vyema kufanya makosa ambayo yatapoteza ubora wa karafuu
ya Zanzibar, ikwemo kuanika barabarani na kuzichanganya na uchafu
usiohitsjika ikiwemo makonyo, matende au udanganyifu mwengine.
Jambo la
msingi ni kuongeza mashirikiano ya pamoja kati ya Shirika,Wakulima na
wadau wote wa zao la karafuu katika kuongeza kiwango cha uzalishaji,
usafirishaji na ubora wa karafuu za Zanzibar.
Comments
Post a Comment