SIMBA SC YAWAONYA YANGA KWA KUANZA UJENZI WA UWANJA BUNJU, ZANA ZATUA RASMI!

Hivi ndivyo mambo yalivyo huko Bunju. Picha hii ni kwa hisani ya Blog ya Bin Zubeiry.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WAKATI mchakato wa uchaguzi wa klabu ya Simba unaotarajia kufanyika juni 29 mwaka huu ukizidi kushika kasi hasa baada ya mgombea aliyeenguliwa kuwania Urais Michael Richard Wambura kurejeshwa, taarifa njema kwa mashabiki wa klabu hiyo ni kwamba mkakati wa ujenzi wa uwanja umechukua sura mpya leo hii.
Mtandao huu unafanya jitihada za kuwatafuta viongozi wa Simba ili kujua zoezi hilo linaendeleaje huko Bunju.
Hata hivyo, Msemaji wa Simba sc, Asha Muhaji ameuambia mtandao huu kuwa hajapewa taarifa rasmi na uongozi kuhusu zoezi hilo.
Muhaji amesema linapotokea jambo katika klabu hiyo anapewa taarifa, hivyo ameahidi kufikia baadaye atakuwa na taarifa zaidi.
“Mimi bado sijapewa taarifa kamili, labda tuwasiliane baadaye ili tujue”. Amesema Muhaji.
 Uongozi wa Simba amepeleka magari yanayomwaga vifaa na kusafisha eneo la uwanja wao  uliopo Bunju jijini Dar es salaam.
Awali suala hili lilichukuliwa kwa utani na kuwabatiza viongozi na wanachama wa Simba jina la utani la`wazee wa kilimo kwanza` , lakini mambo yamebadilika baada ya viongozi kuonekana wamekusudia kujenga uwanja wa kisasa wa klabu hiyo.
Jina hilo lilitokana na katibu mkuu wa Simba kutangaza kuwa wanachama wachukue majembe, makwanja,nyengo ili wakafyeke na kusafisha eneo la uwanja wa Bunju.
Leo hii mambo yamebadilia na magari yameanza kazi ya kusafisha eneo na kumwaga vifaa kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Suala la uwanja limekuwa wimbo wa taifa kwa klabu za Simba na Yanga tangu zianzishwe miaka mingi iliyopita.
 
Picha hii ni kwa hisani ya Blog ya Michezo ya Bin Zubeiry. Unaweza kuitembelea kwa picha zaidi.

Lakini sasa klabu zote zinaonekana kuwa katika mipango ya ujenzi wa viwanja vyao.
Yanga chini ya mwenyekiti aliyeongezewa muda wa mwaka mmoja Yusuf Manji wapo katika mkakati mzito wa kujenga uwanja wa kisasa maeneo ya jangwani.
Lakini kwa upande wa Simba, mwenyekiti wake Ismail Aden Rage alileta siasa katika suala la uwanja, ila sasa inaonekana kuna watu wameamua kulivalia njuga.
Japokuwa kuna watu wanahoji kwanini suala hili limekuja wakati huu wa uchaguzi?, mpango huo unataka kutumika kama kampeni kwa wagombea Fulani?
Lakini bado majibu hayajapatikana kwasababu haijatangazwa kuwa ni mtu fulani anasimamia suala hilo.
Kujenga uwanja ni muhimu sana kwa klabu kama Simba, lakini wasiwasi kwa baadhi ya watu unakuja kulingana na wakati ilionao Simba.
Klabu inaelekea kwenye uchaguzi wiki mbili zijazo na siku kadhaa, hivyo watu wanaanza kuhusianisha na kampeni.
Lakini hata kama ni kampeni, bado ukweli uko pale pale kuwa kiongozi yeyote atakayeingia madarakani ajitahidi kujenga uwanja.
Endapo Kuna watu wameamua kuwahadaa wana Simba kwa ujenzi huo, basi ni tatizo na inaweza kuleta mashaka kama mpango wenyewe utakamilika.
Tusubiri kampeni, kama kuna mtu ametumia ujenzi huo itajulikana, lakini kwasasa tuliache.

Comments

Popular posts from this blog