RAMBIRAMBI MSIBA WA KANALI MWANAKATWE
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha
aliyekuwa Katibu Mkuu wake (wakati huo ikiitwa FAT), Kanali mstaafu
Ali Hassan Mwanakatwe kilichotokea leo asubuhi (Juni 7 mwaka huu)
katika Hospitali Kuu ya Jeshi (GMH) Lugalo jijini Dar es Salaam.
Kwa
mujibu wa binti wa marehemu, Sophia, baba yake alianguka bafuni
nyumbani kwake Mbezi Beach ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Lugalo
ambapo ndipo umauti ulipomfika wakati madaktari wakimpatia matibabu.
Kanali
Mwanakatwe alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu
Tanzania (FAT) katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1993 mjini Kibaha
mkoani Pwani.
Baada
ya kuondoka FAT, aligombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kufanikiwa kushinda katika
uchaguzi uliofanyika mwaka 1997.
Msiba
huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu nchini na Afrika kwa ujumla
kwani, Kanali Mwanakatwen enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa akiwa
kiongozi, na mkufunzi wa utawala wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF). Pia aliwahi kuwa Kamishna wa CAF.
TFF
tunatoa pole kwa familia ya marehemu Kanali Mwanakatwe, DRFA, na Jeshi
la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu
katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Taratibu
za mazishi zinaendelea kufanywa na familia yake nyumbani kwake Mbezi
Beach karibu na hoteli ya Giraffe wakati ndugu wakisubiriwa kutoka
mikoani. TFF tunasubiri taratibu hizo ili tujipange jinsi ya kushiriki
katika msiba huo.
Sisi sote ni waja wake Mola. Hakika kwake tutarejea.
Comments
Post a Comment