KIFO CHA TYSON NI ZAIDI YA MSIBA KENYA

Majonzi na simanzi wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa mwongoza filamu za Kibongo, marehemu George Otieno Okumu ‘Tyson’ katika Viwanja vya Leaders.

WAKATI jana jiji la Dar likizizima kwa vilio, majonzi na simanzi wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa mwongoza filamu za Kibongo, marehemu George Otieno Okumu ‘Tyson’ nchini kwao Kenya ni zaidi ya msiba.

Tyson aliagwa na mastaa, mashabiki na wadau wa burudani Bongo kwenye Viwanja vya Leaders Kinondoni, Dar kabla ya mwili wake kusafirishwa kwa ndege kwenda Kenya kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika Kisumu nchini humo keshokutwa Jumamosi.
Mbali na Wabongo, pia kulikuwa na Wakenya ambao walitumia nafasi hiyo kumuaga mwenzao ambapo baadhi yao waliambatana na mwili huo kwenda Kenya.
Baada ya kuagwa, mwili wa marehemu ulipelekwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar tayari kwa safari ya Kenya.

Sonia na Monalisa wakiwa na nyuso za huzuni wakati wa kuuaga mwili wa marehemu Tyson.
Kwa mujibu wa shuhuda wetu, mwili wa marehemu ulipokewa kwa majonzi makubwa na ndugu, jamaa, marafiki, mastaa na watu mbalimbali kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, Nairobi nchini humo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo hasa redio, mitandao ya kijamii na ‘blogi’ vilieleza kwa simanzi kubwa juu ya kifo cha Tyson kwani kabla ya kujikita Tanzania mwaka 2000 alikuwa akifahamika kama bondia matata ndiyo chanzo cha kupewa jina la Tyson nchini humo.
JB akiaga mwili wa Tyson.
Baadhi ya vyombo vilivyoripoti na kusababisha Kenya kuzizima kwa vilio ni pamoja na Radio Citizen, Citizen Television, mitandao ya Kenya.co.ke, mseto.co.ke, Ghafla.co.ke na mingine kibao.
“Kusema kweli kwa hapa Nairobi, Tyson alikuwa akifahamika sana. Unajua watu wengi walikuwa hawaamini lakini baada ya mwili kuwasili ndiyo wameamini.
“Hata ndugu walikuwa hawaamini hadi walipoona jeneza na kuhakikishiwa kuwa limebeba mwili wa mpendwa wao,” alisema shuhuda wetu kutoka Jiji la Nairobi.
Baada ya kufikishwa Nairobi, ndipo taratibu za kuupeleka mwili huo zikaanza ambapo utapumzishwa kwenye nyumba ya milele Kisumu Jumamosi ijayo.
Dk. Cheni naye akimuaga Tyson.
Tyson alifanya kazi nyingi Bongo ikiwa ni pamoja na kufungua milango ya Bongo Movies alipotengeneza kwa mara ya kwanza Filamu ya Girlfriend na baadaye ikifuatiwa na Dilemma.
Pia alikuwa mwongozaji wa vipindi mbalimbali runingani kuanzia ITV, EATV na TV1. Alipatwa na mauti maeneo ya Gairo, Morogoro baada ya kutokea ajali mbaya akitokea Dodoma kutengeneza Kipindi cha Mboni Show cha EATV chini ya mwanadada Mboni Masimba.
Wakati wimbi la vifo vya wasanii likiongezeka, katika hali ya kushtua, mtabiri na mnajimu maarufu Bongo, Maalim Hassan Yahya Hussein ameendelea kusisitiza kuwa utabiri juu ya vifo vya mastaa utaendelea hadi mwezi Aprili, mwakani.
Wasanii wakiongozwa na Cathy kuaga mwili wa Tyson.
Akizungumza na waandishi wa Global Publishers kwenye makao makuu ya gazeti hili Bamaga-Mwenge jijini Dar, Maalim Hassan ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mnajibu Afrika na kwingineko duniani, marehemu Shehe Yahya Hussein alisema:
“Nasisitiza tena, mwezi wa kinyota huanza Aprili na kuishia Aprili. Katika kipindi cha mwaka huu, kinyota inaonesha watakufa wasanii mfululizo hivyo ni vema wakachukua tahadhari na kukubaliana na hali halisi.”
Alipoulizwa nini cha kufanya, Maalim Hassan aliendelea:
Mzee Chillo akitoa heshima zake za mwisho kwa mwili wa Tyson.
“Wasanii wanatakiwa kumuomba Mungu. Kama ni Muislam asikose kuswali msikitini, kama Mkristo asikose kuhudhuria kanisani na kama ni mpagani, basi atafute namna yake ya kumuomba mungu wake.”
Mbali na Mungu, Maalim alikwenda mbele zaidi: “Pia kinyota wasanii wasivae nguo nyekundu kabisa. Wasipake rangi nyekundu midomoni (lipstick) na kwenye kucha zote. Kimsingi waachane na vitu vya rangi nyekundu.
“Pia wasitoke kwenda kwenye starehe au shughuli za usiku hasa Jumanne na Jumamosi jioni kwani ni siku za vita kati sayari ya Venus na Mercury ambapo mkuu wake ni Israeli Mtoa Roho.”
Alisema kuwa suala la vifo vya wasanii si kwa Tanzania tu kwani hivi karibuni tasnia ya filamu duniani imekuwa ikiondokewa na wasanii kibao kuanzia Hollywood (Marekani),
Nollywood (Nigeria), Bollywood (India) na hata nchini Kenya mwigizaji aliyeigiza kama Idd Amin kwenye simema ya Rise and Fall of Idd Amin amefariki dunia hivi karibuni hivyo ndiyo hali halisi kwa kipindi hiki hadi Aprili, mwakani.
Mbali na Tyson anga la bururudani Bongo  liliwapoteza wasanii wengine kama Shaila Haule ‘Recho’ Adam Philip Kuambiana na Amina Ngaluma.
Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amina.

Comments

Popular posts from this blog