KAZI IMEANZA, SIMBA SC YASAINI BEKI LA TAIFA STARS MIAKA MITATU...YANGA NA MAGAZETI YAO
KAZI
imeanza. Simba SC imesajili mchezaji wa kwanza kabisa kwa ajili ya
msimu ujao, ambaye ni chipukizi wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania,
Taifa Stars Joram Nason Mgeveke.
Mchezaji
huyo chipukizi pekee kutoka kikosi cha maboresho aliyebaki Taifa Stars
chini ya kocha Mholanzi Mart Nooij, amesaini Mkataba wa miaka mitatu
leo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili
ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba,
Joram amesaini mjini Iringa na rasmi sasa ni mchezaji wa Simba SC.
Kifaa cha kwanza 2014-2015; Joram Mgeveke akipeana mikono na Hans Poppe baada ya kusiani Mkataba wa miaka mitatu na Simba SC. Chini anasaini. |
“Tuna
muda mfupi sana kwa ajili ya kufanya usajili, sasa tuna orodha ya
wachezaji waliopendekezwa, kwa hiyo tunaanza kuwapandia ndege kuwafuata
na kumalizana nao, ndani na nje ya nchi. Tumeanza na Joram, kwa sababu
yuko Taifa Stars ambayo inakwenda kambini Botswana,”alisema Poppe.
Poppe
amewahakikishia wana Simba SC kwamba safari hii watasajili wachezaji
bora ambao watarejesha heshima ya klabu hiyo msimu ujao.
Kwa upande wake, beki huyo
mwenye misuli anayecheza nafasi za kati za ulinzi, amesema kwamba
amefurahi mno kujiunga na Simba SC kwa sababu ni timu kubwa, ambayo
anaamini itainua kiwango chake na kumfungulia milango zaidi ya
mafanikio.
Joram Mgeveke wa pili kutoka kushoto waliosimama akiwa kikosini Stars dhidi ya Malawi |
“Kwa
kweli nimefurahi sana kujiunga na Simba SC, ni timu kubwa na ya
kihistoria hapa Tanzania ambayo wamepita wachezaji wengi wazuri, ambao
na mimi ningependea kufuata nyayo zao,”amesema.
Beki
huyo alicheza kwa dakika 75 mechi ya kirafiki ya Tanzania na Malawi
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambayo bao pekee la Amri Kiemba wa Simba
SC liliipa Taifa Stars ushindi wa 1-0 kabla ya kumpisha Kevin Yondan wa
Yanga.
Tangu hapo amekuwemo kwenye
orodha ya wachezaji 18 walioshiriki mechi zote za Stars dhidi ya
Zimbabwe kufuzu Mataifa ya Afrika kama mchezaji wa akiba.
Nyota Njema ndiyo iliyomuibua
kinda huyo mwenye umri wa miaka 22, baadaye akachezea Polisi na Lipuli
zote za Iringa, kabla ya kuchukuliwa timu ya mkoa, ambayo ilimfungulia
milango ya kuingia Taifa Stars kupitia mpango wa maboresho. Katibu wa
Lipuli, Willy Chikweo ametoa baraka zake zote juu ya usajili huo.
“Kuanzia sasa, Joram ni wa Simba SC, kwa roho safi kabisa na tunamtakia
kila la heri,”amesema katibu huyo.
Wakati Simba SC inafanikisha
usajili wa mchezaji wa kwanza wa msimu ujao, watani wa jadi Yanga SC
wanaendelea kupamba kurasa za magazeti kwa majina ya wachezaji tofauti
ambao inadaiwa wanataka kuwasajili kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Na wakati dirisha la usajili
linafungwa mwishoni mwa mwezi huu, hakuna mchezaji hata mmoja ambaye
hadi asa Yanga SC imesema rasmi imemsainisha Mkataba, huku ikiwa tayari
imewapoteza Frank Domayo na Mrundi Didier Kavumbangu waliohamia Azam FC.
Comments
Post a Comment