WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU HAWA GHASIA AUMBUKA KUTOKA KAMBI YA UPINZANI BUNGENI.
- LAPF yakana kumdai Mbowe
- Yaruka kuwasaidia Msigwa, Mbilinyi
SIKU chache baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali za
Mitaa Tawala za Mikoa (Tamisemi), Hawa Ghasia, kusema kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amekopa kiasi cha sh bilioni
moja kwenye Mfuko wa Pensheni kwa Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa
(LAPF), Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Eliud Sanga, amekanusha.
LAPF pia
imekana kuwasaidia fedha au vifaa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi
na Iringa Mjini, Peter Msigwa, kama ilivyosemwa bungeni.
Juzi,
Ghasia alisema kuwa Mbowe anadaiwa sh bilioni moja na LAPF na ametumiwa
waraka wa kumkamata ili afikishwe kwenye vyombo vya sheria.
Waziri huyo alisema si kosa kwa wabunge kupewa fedha na LAPF, lakini ni kosa kwa mbunge kutorejesha fedha alizokopeshwa.
Kauli ya LAPF
Mkurugenzi
Mkuu wa mfuko huo, Sanga, alibainisha kuwa LAPF haijawahi kumkopesha
Mbowe sh bilioni moja, na kwamba mfuko huo hauna utaratibu wa kukopesha
mtu mmoja mmoja, hivyo hakuna mikopo ya aina hiyo.
“Mfuko wa
LAPF hauna utaratibu wa kukopesha mtu mmoja, hivyo hakuna mikopo ya
aina hiyo na wanachofanya ni kutoa mikopo ya wanachama wake kupitia
vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) na mikopo ya nyumba kwa wanachama
wanaokaribia kustaafu,” alieleza Sanga.
Alisema shughuli kuu za mfuko huo ni kuandikisha wanachama, kukusanya michango, uwekezaji na kulipa mafao.
“Ieleweke
kuwa ingawa waheshimiwa wabunge au mtu au taasisi yoyote hazuiliwi
kuomba msaada wa kijamii, Mbilinyi na Msigwa hawajawahi kuwasilisha
maombi na hawajawahi kupewa msaada wowote na LAPF.
“Taarifa
zilizotolewa na vyombo vya habari mbalimbali Mei 26 ambapo gazeti
mojawapo lilikuwa na kichwa kilichosema ‘Waheshimiwa wabunge ni
wasumbufu na kumfanya Mkurugenzi Mkuu asiende bungeni’ si za kweli,”
alisema.
Alibainisha kuwa pamoja na majukumu hayo, mfuko unashiriki katika kuisaidia jamii kupunguza umasikini na kuchochea maendeleo.
“Misaada
hii ina lengo la kusaidia jamii yote ya Watanzania yenye mahitaji
mbalimbali kwa kutambua kuwa misaada hii itawanufaisha si wanachama wa
LAPF tu bali wananchi wote na kwamba imekuwa ikitoa misaada ya kijamii
kwa wananchi wote.
“Imekuwa
ikitoa misaada ya kijamii katika sekta mbalimbali kama vile sekta ya
afya, elimu, vituo vya watoto yatima, kusaidia mashuka, vyandarua na
dawa kwa watu wanaokumbwa na maafa,” alisema.
Aliongeza kuwa LAPF wamekuwa wakichangia elimu kwa kujenga madarasa, ununuzi wa madawati na vifaa vya maabara.
Hata
hivyo, alisema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2013/2014 LAPF imetoa
misaada mbalimbali ikiwa ni pamoja na vifaa vya ujenzi katika Chuo cha
Madaktari Bugando na Chuo Kikuu Huria (OUT).
Alisema
kuwa LAPF haizuii taasisi yoyote kuomba msaada wa kijamii kwa kuwa hutoa
misaada mbalimbali kwa kuzingatia mpango wa bajeti iliyoidhinishwa kwa
kuzingatia sera ya misaada ya kijamii na maombi yaliyowasilishwa.
Sanga,
alisema hata taasisi au mtu hapewi fedha mkononi taslimu, bali LAPF
inanunua vifaa na kuwasilisha moja kwa moja kwa wahusika.
Comments
Post a Comment