MENEJA EWURA AJIUA HOTELINI BAADA YA KUHOJIWA NA BUNGE





    Dar/Dodoma. Meneja Biashara wa Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) amekutwa amekufa hotelini katika mazingira ya kutatanisha muda mfupi baada ya kuwasili jijini Dar es Salaam akitoka Dodoma ambako alihojiwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Meneja huyo, Julius Gashaza, ambaye alikuwa na jukumu la kupanga bei za mafuta za kila mwezi, alihudhuria kikao hicho mjini Dodoma kwa siku mbili; Ijumaa na Jumamosi iliyopita kuhusu mambo mbalimbali, yakiwamo kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini, mgawo wa fedha unaotolewa na Ewura kwenda kuhudumia umeme vijijini (Rea) na fedha za mfuko wa barabara.
Jeshi la Polisi, Mkoa wa Temeke limethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa meneja huyo alikutwa amejinyonga kwa kutumia tai kwenye hoteli ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo Vituka wilayani Temeke.
Nyumbani kwa meneja huyo wa Ewura, kulikuwa na waombolezaji waliokuwa kwenye vikundi na kikao cha maandalizi ya mazishi kilifanyika ndani ya nyumba ya marehemu iliyopo Yombo Vituka na baadaye kuhamia nyumba ya jirani.

Kamati ya Bunge ya Bajeti, inayoongozwa na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ilikutana na maofisa wa Ewura, akiwamo Gashaza na wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kugundua kuwapo kwa tofauti katika takwimu za kiwango cha mafuta kilichostahili kutozwa kodi.
Gashaza alikwenda Dodoma kutoa ripoti ya Ewura kwenye kamati hiyo ya Bunge akimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kamati hiyo, takwimu za Ewura ziliashiria kuwa fedha zilizopatikana ni nyingi zaidi ya zile zilizoelezwa na TRA, lakini Wizara ya Fedha ilisisitiza zifuatwe takwimu za mamlaka ya mapato.

Habari hizo, zinasema baada ya kurejea Dar es Salaam juzi majira ya saa tatu usiku, Gashaza hakwenda nyumbani kwake na badala yake alikwenda kwenye hoteli iliyo karibu na nyumbani ambako mkewe na ndugu yake mmoja walimfuata na akawaeleza kuwa anahisi kutishiwa maisha yake.
Baadaye walifanya maombi maalumu kabla ya kuachana naye.

Inadaiwa kuwa marehemu aliomba akalale hotelini kwa sababu hakuona kama ana amani kulala nyumbani kwake na ilipofika asubuhi alikutwa ‘amejinyonga’ ndani ya chumba alicholala hotelini humo.
Nyumbani kwa marehemu waombolezaji walikusanyika katika makundi, lakini baada ya kukaa katika kikao cha familia walitoka na kauli moja kuwa hawatasema chochote na kwamba jukumu hilo libaki mikononi kwa polisi.


Polisi wathibitisha.Chanzo Mwananchi

Comments

Popular posts from this blog