KILA MTU NI MROHO WA MADARAKA LAKINI UROHO UNATOFAUTIANA, WEWE UMESIMAMA WAPI?


Nguvu ya madaraka na uwezo wa madaraka yenyewe yamefanya watu wengi kufanya vitu vingi ili angalau aonekane anastahili kuwepo kwenye hayo madaraka. Wiki hii sizungumzii viongozi wa serikali, vyama na mashirika bali ni katika maisha ya kawaida ambayo sisi wengine tupo huko kwa wingi wetu. Kwa tafsiri rahisi ni uwezo anaopewa mtu juu ya jambo fulani yeye kulisimamia au kusimamia kitengo fulani cha watu fulani ndipo tunaposema mtu huyu ana madaraka ya kitu fulani.
Ukifuatilia kwa makini uroho wa madaraka hauko huko juu tu, bali hata huku mtaani mambo yanaendelea hivyo hivyo. Sikujua kuna watu wanatamani wawe ndo wenyeviti wa harusi, wasipowekwa utalijua kasheshe lake, inabidi waanze kwa kusema unajua huyu mwenyekiti hana uzoefu kabisa na nina wasiwasi kama ana hekima. Nikajaribu kuwaza je tatizo ni mwenyekiti au tatizo ni wewe? Upo kwenye kamati kwa ajili ya kusaidiana na huyo mwenyekiti ili mfanikishe hiyo harusi. Kwani kwenye harusi zaidi ya michango na kujua harusi itafanyikia wapi, je wewe utakuja na ubunifu gani mpya watu wasioujua? Je kwanini huwezi kuthamini na kuheshimu watu wengine wakiwa juu yako? Inawezekana watu hawakuamini au hauna mvuto wa kuwaongoza katika hiyo kamati, unachotakiwa ni kujishusha na kuruhusu wakati mwingine uongozwe ili uweze kujifunza.

Je una ajenda gani ya siri kwenye hayo madaraka unayoyataka? Unajua ni rahisi kuwasema viongozi wa juu kuwaona kuwa ni waroho. Utagundua kila mtu ni mroho wa madaraka ila kiwango cha uroho kimetofautiana. Labda ukichukua uenyekiti wa maandalizi ya harusi, itabidi uipigie chepuo biashara yako au kamisheni ya mapambo , ukumbi, vinywaji na hata usafiri na video shooting? Je agenda yako ni nini?
Agenda yako ndio itakufanya ung’ang’anie uongozi au usiung’ang’anie uongozi. Kama una mpango wa kusaidia kwa roho safi ni vizuri zaidi. Ila kama ni kwa ajili ya umaarufu na kuleta mivutano isiyo ya kawaida, ninakushauri kaa pembeni. Kama una mpango wa kusaidia hata usipokuwa mwenyekiti au ngazi yeyote , bado unaweza kusaidia na mchango wako utafaa sana. Jifunze kujitolea hata kama hujapewa cheo.
Kumbuka, mwoaji na mwolewaji ndio wanajua wanachokitaka , hivyo kila jambo lazima liende kulingana na hao wanaofanya mkae kikao. Ingawa kuna mambo yamekuwa yakiendelea ambapo watu wengine ndo wanaosema harusi iweje, ni kana kwamba vitu ambavyo havikufanyika katika maisha yao wanataka vifanyike kwenye maisha ya wengine. Kama ya kwako ulidunda, usilazimishie kwa wengine, kila mtu ana kitu anachokipenda kitokee kwenye maisha yake hivyo waruhusu kama inawezekana wao ndo waamue kitu wanachokihitaji. Wewe ni kuwasaidia wafike pale wanapotakiwa kufika, sizungumzii utamaduni ninazungumzia kwamba mwisho wa siku kumbukumbu ni kwa ajili ya hao wawili nyinyi ni mashahidi tu.
Ni mwendelezo wa kuelewa kabla ya kufanya jambo au kutekeleza jambo.

Comments

Popular posts from this blog