HOFU YATANDA: BINTI ALIYEZIKWA AIBUKIA KWAO
Witness
Obed (21) aliyefariki dunia Aprili 12 mwaka huu na kuzikwa kwenye
makaburi ya nyumbani kwao Kijiji cha Nanja, mkoani Arusha na kuibuka
akiwa hai tena.HOFU ya
ushirikina imetikisa Mkoa wa Arusha kufuatia tukio la hivi karibuni
ambapo mwanafunzi wa Chuo cha Kompyuta jiji hapa, Witness Obed (21)
aliyefariki dunia Aprili 12, mwaka huu na kuzikwa kwenye makaburi ya
nyumbani kwao Kijiji cha Nanja, Kata ya Moshono wilayani Arumeru, Arusha
kuibuka akiwa hai.
Binti huyo aliibuka kwao hivi karibuni akiwa mpole na kuwafanya baadhi ya watu, wakiwemo wazazi wake kutimua mbio kwa hofu.
Watu kutoka maeneo
mbalimbali
jijini hapa wamekuwa wakimiminika nyumbani kwa wazazi wa binti huyo
kwa lengo la kumshuhudia kwa vile ndugu walishaamini kuwa, mpendwa wao
huyo alishakufa na alizikwa.
UWAZI LATIA TIMU NYUMBANI
Baada
ya kusikia taarifa hizo, Uwazi lilifunga safari mpaka eneo la tukio na
kumshuhudia binti huyo kisha likaenda kwenye kaburi alilozikwa.
Kwenye
kaburi hilo, msalaba wenye kuonesha siku yake ya kuzaliwa (1992) na
kufa (12, Aprili, 2014) ulikuwa bado umesimama imara huku kaburi lenyewe
likionesha dalili ya kutitia kidogo.
BABA MZAZI ASIMULIA
Akisimulia mkasa huo kwa mshangao mkubwa, baba mzazi wa binti huyo, Obed Leiyo alisema:
“Ilikuwa Aprili mwanzoni, binti yangu alitoweka nyumbani baada ya kurudi kutoka chuoni majira ya saa 2 usiku akiwa amechelewa.
Mimi kama mzazi nilimfokea kwa kuchelewa kwake kurudi nyumbani.
“Yeye kwa hasira zake alizunguka nyumba akaondoka muda huohuo na hakurudi kabisa hapa nyumbani.
“Siku
iliyofuata tulianza kumtafuta maeneo mbalimbali bila mafanikio, tukatoa
matangazo kwenye vyombo vya habari lakini binti yangu hakuonekana.”
TAARIFA ZAFIKA, KAFA
Mzazi
huyo aliendelea kusema: “Siku moja tulipata taarifa kwamba kuna mwili
wa msichana umeonekana katika Kijiji cha Bwawani hapahapa Arumeru.
“Mimi pamoja na ndugu wengine tuliamua kwenda katika kile kijiji.
Tulipofika tuliambiwa ni kweli mwili wa msichana uliokotwa lakini
wananchi wakauzika.”
WAFUKUA KABURI
Baba
huyo anaendelea: “Niliamua kwenda Kituo cha Polisi cha Usa River ambako
niliomba kibali kwa ajili ya kufukua kaburi na kuutoa mwili ili
kuutambua kama ni binti yangu au la!
“Nilipewa
kibali, tukafukua kaburi na kutoa mwili. Nilimtambua kuwa ni binti
yangu kutokana na alama mbalimbali alizokuwa nazo, ikiwemo rangi kwenye
kucha na sehemu ya kushoto ya uso ilikuwa nyeusi kwa sababu aliwahi
kupooza.
MWILI WASAFIRISHWA, WAZIKWA
Baba
huyo wa Witness alizidi kueleza kuwa waliusafirisha mwili huo hadi
nyumbani kwake Moshono na kuandaa taratibu za mazishi ambapo Aprili 23,
mwaka huu mwili ulizikwa.
AIBUKA GHAFLA
Hata
hivyo, Obed anasema alishangaa siku ya tukio kumwona binti yake huyo
akiibuka nyumbani hapo akiwa hai jambo ambalo lilimshangaza na kumfanya
akimbie kwanza na baadaye kufanya mawasiliano naye.
BINTI ASIMULIA
Akizungumza na Uwazi, binti huyo alikiri kutoweka nyumbani kwao Aprili 15, mwaka huu na kwenda kusikojulikana.
Alisema
hakujua kilichoendelea baada ya kuondoka nyumbani lakini baadaye
alibaini kuwa alikuwa katika Kijiji cha Olkokola wilayani Arumeru na
alikwenda kwenye nyumba ya mwanamke mmoja asiyefahamiana naye akamuomba
maji ya kunywa.
“Nilifika
kwenye nyumba moja nikamkuta mama mmoja, nikamwomba maji ya kunywa
akaenda kuniletea. Nilikunywa huku amenisimamia, lakini maji yalikuwa
machungu sana, nikamrudishia, akanilazimisha ninywe kwa kunisukumia
kikombe kinywani. Nilipomaliza nilipoteza fahamu.
“Baadaye nilizinduka, nikaendelea kuishi palepale nyumbani kwa yule mama lakini sifahamu nilikuwa nafanya nini.
“Juzi ndiyo nikashangaa
kujikuta nimerudi nyumbani, mimi sijui nini kilikuwa kikiendelea,” alisema binti huyo.
MAJIRANI NAO
Majirani
kadhaa waliokuwepo nyumbani kwa Obed walilielezea tukio hilo kwamba ni
la ushirikina huku wakisema ni jambo la kuogofya ambalo halikuwahi
kutokea kijijini hapo kabla.
Wengine walisema kuwa binti huyo alifufuka na wengine walisema alichukuliwa msukule.
“Hili
si suala la kawaida lazima kuna ushirikina kwani huyu binti
tulishamzika na wazazi wake walimtambua kabisa kuwa ni yeye baada ya
kuambiwa
alikutwa amekufa, sasa hebu fikiria tangu tumezika mbona hakuna mtu
aliyekuja na kusema na yeye alipotelewa na binti yake halafu cha ajabu
hilo kaburi mbona limebonyea? Atakuwa amefufuka,’ alisema mkazi mmoja
aliyejitambulisha kwa jina la Amina Liwa.
Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Usa River, Benedict Mpujila amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unafanyika.
KUMBUKUMBU
Mapema
mwaka jana tukio la kishirikina liliibuka katika wilayani Arumeru eneo
la Kwa Mrefu ambapo mtu mmoja alidaiwa kudondoka na ungo, muda mfupi
baadaye alitoweka na kwenye ungo kubaki mayai na kuku mweupe.
Comments
Post a Comment