HALIMA MDEE AMLIPUA PROF TIBAIJUKA
- Adai anamiliki maelfu ya ardhi hapa nchini
- Wabunge wamshambulia, Makinda amuokoa
- CCM waitisha kikao cha dharura kumnusuru
Mdee
ambaye ni Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alirusha kombora
hilo jana bungeni wakati akisoma maoni ya kambi hiyo kwa Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Makombora
hayo ya Mdee, yalimfanya Waziri Tibaijuka, kutumia muda mrefu zaidi
kujibu mashambulizi badala ya hoja za wabunge wakati akihitimisha hoja
yake.
Majibu
hayo yalimfanya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kila mara kumtaka Waziri
Tibaijuka ajibu hoja za wabunge badala ya kujikita kumjibu Mdee, katika
masuala yanayoonekana ni binafsi.
Waziri
Tibaijuka, alisema kuwa Mdee amekuwa bingwa wa kuiba siri za serikali
ikiwemo mwaka jana kuiba andiko la chuo kikuu na mwaka huu ameiba barua
zake za siri alizomuandikia Waziri Mkuu.
Hoja za Mdee
Mdee,
alisema Waziri Tibaijuka ana maslahi makubwa katika sekta ya ardhi
ambapo anamiliki kiasi kikubwa cha ardhi maeneo ya Kigamboni na Kagera
Wilaya ya Muleba ambako katika eneo la Kyamnyorwa ana hekta 800.
Kwa mujibu wa Mdee, mjini Bukoba, waziri huyo mwenye dhamana ya ardhi, anadaiwa kumiliki ekari 100 alizozipata kiujanja.
Alisema
eneo hilo alilipata kwa kuwahamisha wamiliki halali kwa nafasi yake ya
ukurugenzi wa UN-Habitat na baadaye ya uwaziri wa ardhi.
“Mheshimiwa
Spika, linapokuja suala la migogoro ya ardhi, Waziri Tibaijuka anakosa
“moral authority” katika kuutafutia ufumbuzi wa haki. Hivyo basi, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka serikali kuliangalia upya suala lolote la
ardhi ambalo waziri atajiingiza kwani nyuma ya sakata hilo kuna maslahi
binafsi yake kama hili la Chasimba, na Kigamboni,” alisema Mdee.
Mbunge
huyo alifichua siri nyingine ya umiliki wa ardhi ya waziri huyo katika
eneo la Kigamboni ambako kuna mradi mkubwa wa ujenzi wa mji mpya na wa
kisasa.
Alisema
katika eneo hilo, Waziri Tibaijuka, kwenye ekari 50,934 zilizoongezwa
kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa mji mpya wa Kigamboni, amejimegea maelfu
ya ekari.
Alisema Waziri Tibaijuka aliongeza eneo la mradi kutoka hekta 6,494 zilizokuwepo awali hadi hekari 50,934.
“Hoja
hapa ni je kati ya hekta zilizoongezwa 44,440, zinazomilikiwa binafsi na
waziri ni ngapi? Hii haina siri, akikataa kusema wananchi wanaelewa ni
ngapi, na hotuba ya mwaka kesho zitatajwa hapa bungeni,” alisema Mdee.
Alisema
anaitaka serikali kuangalia upya mipango ambayo inatayarishwa na
kusimamiwa na Waziri Tibaijuka na jinsi gani inatekelezwa kwa madai kuwa
haaminiki tena.
Mdee
alisema katika migogoro mingi ya ardhi, Waziri Tibaijuka amekuwa
akitajwa kuhusika na katika mazingira hayo ni dhahiri kuna jambo
limejificha, hivyo ni wakati mwafaka kuchukua hatua kabla ya majanga
zaidi kutokea.
Mbunge
huyo alimshambulia Tibaijuka, kwamba hawezi kusimamia wizara hiyo kwani
hata kwenye nafasi aliyoachia Umoja wa Mataifa, aliondolewa kutokana na
uwezo mdogo wa kufanya kazi.
Akizungumzia
sarakasi za mradi wa Kigamboni, Mdee alisema mpango wa ujenzi wa mradi
huo, umekuwa ukilalamikiwa sana na kutiliwa shaka na wananchi wa eneo
hilo.
Mbunge huyo alisema mpango huo ambao unaelezwa kuwa wa serikali, sio sahihi kwani umevalishwa koti tu la serikali.
Kwa
mujibu wa Mdee, ukweli huo unathibitika kutokana na mvutano uliopo kati
ya wananchi wa Kigamboni wakiongozwa na mbunge, Dk. Faustine Ndungulile
na Waziri Tibaijuka kuhusu kukiukwa kwa sheria ya mipango miji.
“Huu ni
udhaifu mkubwa kwa upande wa utawala kwani ndio kinakuwa chanzo cha
mgogoro usiokwisha na kusababisha hata kama kuna nia njema basi dhamira
ovu inaanza kujitokeza wazi mbele ya uso wa jamii,” alisema.
Mbunge
huyo alisema katika kikao cha bajeti mwaka jana, Bunge lilitoa mwongozo
wa kumaliza mgogoro kwa kuitaka serikali kupitia kwa Waziri Tibaijuka,
kukaa na mbunge na wananchi kumaliza mtafaruku huo, lakini hadi sasa
kikao hicho hakijawahi kufanyika.
Kibaya
zaidi Mdee alisema wizara imeandaa Master Plan bila kuwashirikisha
wananchi kupata maoni yao kama sheria ya mipango miji inavyotaka.
“Mheshimiwa
Spika, kambi rasmi inauliza je hayo maoni ya mwanzo yalikusanywa lini?
Kama yalikusanywa mbona wananchi wanalalamika? Tunamtaka waziri atoe
majibu ya kueleweka,” alisema Mdee.
Mbunge
huyo ambaye jana alikuwa mwiba kwa Waziri Tibaijuka, alihoji kama kuna
uhalali wa kuendelea na mpango huu kabambe pamoja na wakala wa
kuendeleza mji wa Kigamboni.
Mgogoro wa ardhi Chasimba
Akizungumzia mgogoro wa Chasimba, Mdee alisema kwa muda mrefu wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakiitwa wavamizi.
Lakini
alisema ukweli unabaki kuwa kuna siri kubwa sana iliyojificha ya namna
Kiwanda cha Wazo Hill kwa kutumia viongozi wa kijiji wa kipindi kuuza
ardhi ya wananchi wakiwa ndani, kisha kubadilisha mipaka na hatimaye
kiwanda hicho kupewa hati kinyemela.
Kwa
mujibu Mdee, mahakama iliamua wananchi wahame, lakini pia iliiagiza
serikali kwamba wajibu wake katika mgogoro huu ni kuwapatia makazi
mbadala.
Alisema amri hiyo ilishindwa kutekelezwa kwa madai ya ukosefu wa fedha na eneo la kuwahamishia.
“Mheshimiwa
Spika. hatimaye ‘inasemekana’ wizara ilipata ‘eneo’ la ekari 1,000
ukilinganisha na ekari 630 za eneo la Chasimba, mchakato ulisababisha
kuitisha kikao cha wananchi, waziri na timu yake na mthamini mkuu wa
serikali na timu yake, walifikia muafaka wa wananchi kufanya tahmini na
kulipa fidia wote waliotathminiwa ambao jumla yao ni 4096,” alisema.
Mdee alisema wananchi hao waliahidiwa kulipwa sh 15,000 kwa mita moja ya mraba, pamoja na viwanja mbadala.
“Mheshimiwa
Spika, lakini katika kile kilichoonekana kuna harufu ya wizi na rushwa,
katika kikao kilichofanyika baa kikiwahusisha Waziri Tibaijuka, Diwani
wa Kata ya Bunju, Mwenyekiti wa Mtaa wa Basihaya, pamoja na inayoitwa
‘Kamati ya Wananchi’, wWaziri alisema wananchi hawatalipwa tena sh
15,000 kwa Square Metre, bali watapewa 5,000 ya kifuta jasho,” alisema.
Mbunge
huyo wa CHADEMA, alisema kilichofanyika baadaye, waziri na timu yake
walianza kutumia vitisho na kuwataka wananchi wafungue akaunti na kujaza
fomu zisizo hata na muhuri wala nembo ya wizara, zikiwataka waandike
namba zao za akaunti na kwamba wangekutana na pesa zao huko huko.
Na zaidi
ya hiyo, wananchi hao waliambiwa asilimia 10 ya pesa watakayolipwa
itakwenda kwenye Saccos, ambayo haijulikani ni ya nani, imeundwa lini na
kwa madhumuni gani.
“Mheshimiwa
Spika, mpaka sasa waziri akiulizwa tutajazaje fomu na kuandika akaunti
ili tuingiziwe pesa ambazo hata hatujui ni kiasi gani, anajibu
utakachokikuta hata kama ni 200 ndio halali yako,” alisema Mdee.
Dalili za wizi
Kwa
mujibu wa nyaraka ambazo kambi ya upinzani inazo, Mdee alisema kaya
4,096 zilizofanyiwa tathmini, kwa kiwango cha sh 15,000 kwa mita moja ya
mraba, fedha iliyotakiwa kulipwa ni sh 47,368,357,520/-.
Alisema
hiyo inathibitishwa kwa barua ya tarehe 8/11/2013, yenye kumbukumbu
namba CBA 171/312/01 kutoka kwa Waziri Tibaijuka kwenda kwa Waziri Mkuu
Mizengo Pinda.
Alisema
katika barua husika, pamoja na mambo mengine anampa taarifa waziri mkuu
juu ya uhitaji wa sh 69,051,215,426 kama hitaji la fedha kwa zoezi zima
la kulipa fidia kutwaa eneo la makazi mbadala, kulipanga eneo jipya
kimipango miji, kupima viwanja na kuweka miundombinu ya msingi hususan
barabara, maji, shule ya msingi, dispensari.
Mdee
alisema kitendo kinachofanywa na waziri pamoja na uongozi wa Kiwanda cha
saruji cha Wazo kumlazimisha Waziri Mkuu akubali deal hiyo ifanyike
haraka, inatia shaka kwani huenda Waziri Tibaijuka atafaidika na mpango
huo.
Mdee
alisema kwa mujibu wa tathmini, kaya zilizofanyiwa tathmini, na kutakiwa
kupewa viwanja mbadala ni 4,096, lakini wizara inataka kuvilipia
viwanja 4,500 na vilivyosalia 404 vya ziada havijulikani ni mali ya
nani.
Taasisi yenye mahusiano na Tibaijuka
Mdee,
alizidi kumkaba koo Waziri Tibaijuka kwamba ana mahusiano na taasisi ya
Tanzania Women Land Acces Trust (TAWLAT) ambayo imo katika mchakato huu
tata.
Alisema
kuwa ushahidi unaonyesha kuwa waziri alikishauri kiwanda kuingia mkataba
na taasisi hiyo ya TAWLAT kutoa elimu na kuendesha mazungumzo na
viongozi na wananchi wa Chasimba juu ya mgogoro wao.
Kutokana
na mazingira hayo, Mdee alisema kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina
shaka juu ya ushiriki wa shirika hilo katika mgogoro wa Chasimba pamoja
na kazi nyingine za wizara.
Alisema
kwenye mgogoro huo wa Chasimba, taasisi hiyo ililipwa sh milioni 300 na
milioni nyingine 300 zilizotolewa na Halmashauri ya Kinondoni.
“Mheshimiwa
Spika, kwa maelezo ya Waziri Tibaijuka, katika kazi hiyo taasisi hiyo
ililipwa sh milioni 300 na katika mchanganuo niliouainisha hapo awali,
wangelipwa sh milioni 500 kwa kazi hiyo. Nikiwa kama mbunge wa jimbo
husika, nikuhakikishie kwamba hiyo taasisi haikufanya kazi yoyote,”
alisema.
Mdee
alisema kazi ya uthamini ilifanikiwa baada ya aliyekuwa Mkurugenzi wa
Upimaji na Ramani na timu toka Wizara ya Ardhi kuja ofisini kwake
kumuomba awasaidie kutuliza upepo kwani wananchi walikuwa wakiwarushia
mawe.
“Mheshimiwa
Spika, ilituchukua mikutano mikubwa si pungufu ya sita mimi nikiwa
msemaji mkuu kuwaelimisha wananchi nia ya tathmini huku wakubwa hawa
wakiwahahakikishia kwamba watalipwa 15,000 kwa square metre na kupewa
maeneo mbadala. Hakukuwa na cha TAWLAT, wala Waziri Tibaijuka,” alisema.
Kutokana
na sarakasi hizo, Mdee alisema kambi ya upinzani inaitaka Takukuru
kufanya uchunguzi wa ushiriki wa TAWLAT kuhusu ushiriki wake wa shaka
katika kazi kadhaa za Wizara ya Ardhi na wasipofanya hivyo,
watawasilisha hoja binafsi kuhusu sakata hili.
CCM wakutana ghafla
Katika
hatua inayohusishwa na ugumu wa bajeti ya wizara hiyo, wabunge wa CCM
walikutana ghafla ambapo pamoja na mambo mengine walijadili mwelekeo wa
bajeti ya wizara hiyo.
Karibu wabunge wote waliochangia bila kujali itikadi, waliishambulia bajeti ya wizara hiyo na kutishia kuondoa shilingi.
Mbali ya
wabunge wa CCM kutishia kuondoa shilingi, mawaziri wengi hawakuwemo
wakati Waziri Tibaijuka anasoma bajeti yake na taarifa zinadai kuwa
wamemsusia kwa vile amekuwa hashiriki kwenye bajeti za wizara nyingine
kwa namna yoyote ile.
Mmoja wa wabunge wa CCM, aliliambia gazeti hili kuwa chama kimeweka msimamo wa kumnusuru Waziri Tibaijuka.
Comments
Post a Comment