ANGALIA PICHA NJIWA MWENYE HIRIZI ATIKISA MUHIMBILI
Njiwa aliyetua kwenye kitanda cha mgonjwa na baada ya muda mgonjwa akafariki.
Hofu
kubwa ilitanda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jumatatu ya wiki
iliyopita, baada ya Njiwa mweusi, mwenye miguu myekundu akiwa na hirizi
iliyofungwa katika mojawapo ya mabawa yake, kutua katika miguu ya
mgonjwa aliyekuwa amelazwa wodi namba tatu, jengo la Mwaisela.Taarifa
zilizopatikana kutoka kwa baadhi ya wauguzi wa wodi hiyo ambao
hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini, walisema tukio hilo lilitokea
saa 3.55 asubuhi ambapo njiwa huyo aliingia kupitia dirishani na kwenda
kutua mguuni mwa Mwanahawa Ngunda (61) aliyekuwa amelala kitanda namba
7, ambaye anadaiwa kuwa mkazi wa Kimara.
Inadaiwa kuwa baada ya kuingia wodini, njiwa huyo alianza kuzunguka na
kuleta taharuki kubwa kwa wagonjwa, wauguzi na ndugu waliokuwemo, kiasi
cha baadhi yao kukimbia huku wakipiga mayowe, kabla ndege huyo hajaenda
kutua miguuni mwa mgonjwa huyo, huku akiwa ametuna na macho yake mekundu
yakiwa yanalenga lenga machozi.
Inasemekena baada ya muda, ndege huyo aliruka na kutua dirisha
lililokuwa usawa wa kitanda alicholala Fatuma na kuzidi kuwakoroga watu
ambao waliamini kuwa ni mambo ya kishirikina. Ndugu wa mgonjwa
aliyetuliwa na njiwa huyo, anayedaiwa kuwa ni mama yake mzazi, alikosa
amani akiamini jambo baya lingemtokea.
Lakini katika hali ya kushangaza zaidi, mhudumu mmoja wa wodi hiyo
alisema wakati watu wakitaka njiwa huyo aondolewe ili kuondoa usumbufu,
dada wa Fatuma, aliyejulikana kwa jina la Mwanaisha Musa alimwambia
mhudumu kuwa yeye amempenda ndege huyo na anaomba apewe kwani anahitaji
kwenda kumfuga.
Kitanda kikiwa tupu baada ya mgonjwa kufariki.
Mhudumu
huyo alimweleza dada huyo kuwa anaweza kumchukua kama anaweza, ndipo
dada huyo alipomwambia kaka yake aliyetajwa kwa jina la Yasini
amkamatie, ambaye alimfuata dirishani na kumkamata bila ndege huyo
kuleta ubishi na kumkabidhi dada yake.
Baada ya dada huyo kukabidhiwa ndege huyo na yeye kumfunika na kanga
yake kama kichanga, ndipo ndugu wa mgonjwa aliyetuliwa na njiwa huyo
alipodaiwa kupandisha mashetani, akimfuata Mwanaisha ambaye alishaanza
kutoka wodini hapo.
Ndugu huyo alimfuata akidai kulikuwa na jambo kwani haiwezekani watu wote wamuogope njiwa huyo, lakini yeye amchukue bila hofu.
Inadaiwa kwamba pamoja na mtoto wa marehemu kupiga mayowe lakini
Mwanaisha hakuweza kumwachia njiwa huyo. Hata hivyo, mkusanyiko mkubwa
wa watu na mayowe, yaliwafanya walinzi kuingilia kati kumtaka mama
aliyemchukua njiwa huyo, kumkabidhi kwao mara moja.
Baada ya kukabidhi, Mwanaisha na kaka yake waliondoka na kumuacha ndugu
wa mgonjwa akilalamika juu ya usalama wa mama yake, hivyo kuanza
kuwapigia simu ndugu na jamaa zake akiwaeleza juu ya tukio hilo.
Mwandishi wa habari hizi alifika katika wodi hiyo na kukuta kitanda
alicholazwa mgonjwa aliyekanyagwa na njiwa akiwa hayupo na alipouliza,
wauguzi walisema mgonjwa huyo alifariki siku iliyofuata (Jumanne wiki
iliyopita) muda kama uleule wa saa 3.55 ambao njiwa huyo alifika.
Bi. Fatuma akiwa wodini.
Fatuma ambaye bado amelazwa wodini hapo alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikiri kutokea.
“Ni kweli njiwa mwenye hirizi alitokea hapa wodini na alipoingia akamkanyaga mgomjwa mwenzangu, hata hivyo dada yangu alimpenda,
alimuomba mhudumu amruhusu amchukue, alikubaliwa na alipomchukua ndipo
mtoto wa marehemu alipandisha mashetani na dada aliamua kuwakabidhi
askari,” alisema mgonjwa huyo aliyedai hali yake bado siyo nzuri na
kwamba anasubiri vipimo.
Habari zaidi zinasema njiwa huyo alitoweka kiaina kutoka mikononi mwa
askari wa Muhimbili wakati akishikiliwa katika ofisi kuu ya usalama
wakisubiri agizo kutoka kwa viongozi wa juu.
Msemaji mkuu wa hospitali hiyo, Aminiel Akaesha alipohojiwa alikiri
kutokea kwa tukio hilo huku baadhi ya wafanyakazi wa hospitali hiyo
wakizungumzia kuhusu uwepo wa ishara ya mambo ya kishirikina wakati
mwingine watu wasioonekana wakizungumza hasa katika eneo la chumba cha
kuhifadhia maiti.
Comments
Post a Comment