MBWA WA UBALOZI WAMLA MTOTO!

NI vigumu kuamini kilichotokea lakini ndivyo ilivyokuwa! Mtoto Christian Alex (6) ameuawa kikatili kwa kuliwa na mbwa wanaodaiwa kuwa ni wa Ubalozi wa Qatar nchini Tanzania unaoongozwa na Balozi Jassim Mohammed Mubarak Daruwesh.

Mtoto Christian Alex enzi za uhai wake.
Tukio hilo la kusikitisha lilijiri Machi 26, mwaka huu Jangwani Beach, Kunduchi jijini Dar es Salaam ambapo mtoto huyo alishambuliwa na mbwa wa kigogo huyo alipokuwa na baba yake jirani na nyumba hiyo ya kupanga yenye nyumba nyingine mbalimbali (apartment).

MAELEZO KWA UFUPI
Inaelezwa kuwa, baba wa marehemu pia anaishi kwenye moja ya nyumba hizo akifanya kazi ya kutunza mazingira endapo mpangaji mmoja anahama. Wote wanaoishi humo wanatumia mageti mawili tu, kuingia na kutoka.

Mama wa mtoto Christian Alex akiwa amezimia wakati mwili wa mwanae unazikwa
BABA WA MAREHEMU ASIMULIA
Akizungumza na gazeti hili kwa majonzi kwenye msiba uliogubikwa na vilio na simanzi, baba wa mtoto huyo aliyejitambulisha kwa jina la Alex, alisema siku ya tukio yeye alikuwa akitoka nje ya nyumba anayoishi katika ‘apartment’ hizo, lakini ghafla nyuma yake alisikia kelele za mwanaye.
“Kwa kawaida ili utoke lazima uwe makini, kwanza ujue mbwa wako wapi? Nilipotoka nikiwa nawaangalia walipo, mara nikasikia kelele mtoto wangu analia, nilirudi haraka, nikamkuta mwanangu anashambuliwa na mbwa watatu huku tayari akiwa na majeraha makubwa.

Mazishi ya Mtoto Christian Alex (6).
“Ilibidi nimng’ang’anie mtoto ili kumwokoa ambapo pia niliokota jiwe kutaka kuwapiga, wakataka kuondoka lakini wakarudi tena na kumvamia.
“Hapo ndipo ilikuwa shughuli kwani walimfumua utumbo, wakazinyofoa sehemu zake za siri na kuziingiza midomoni huku kisogoni wakimtia kucha kali mpaka kumtoa ngozi.
“Wakati kitendo hicho kinaendelea huku nikishuhudia kwa macho, yule balozi akawa anaingia ndani, akawaamuru mbwa wake waache, walitii amri hiyo lakini hali ya mtoto wangu ilikuwa mbaya sana, akawa hasemi wala hapigi kelele tena za kuomba msaada,” alisema baba huyo huku akimwaga machozi. Inauma sana!

Mtoto Christian Alex baada ya kujeruhiwa na mbwa wa ubalozi wa Qatar.
Akaongeza: “Mpaka sasa siamini kilichotokea, nashindwa hata niongee nini, ninachoweza kusema ni kwamba mwanangu Christian nilikuwa nampenda sana kama vile ninavyompenda mwanangu mwingine, Sabina.
“Nahisi ukiwa baada ya kupoteza mtoto wa kiume niliyekuwa namtegemea. Itanichukua muda mrefu sana kusahau kile nilichokiona kwa macho yangu. Nimeshuhudia mwanangu akishambuliwa na wala sikusimuliwa na mtu.”


Mazishi yakiendelea.
KUMBE TAHADHARI ILITOLEWA
Baba anaendelea kusimuliza: “Kinachoniuma zaidi ni kwamba, nilishatoa angalizo tangu mwanzoni wakati huyu bwana anahamia kwenye nyumba hii. Nilimwambia mwenye nyumba amwambie huyu awajengee banda mbwa wake lakini wakapuuzia.”

ADAKTARI WALIVYOSEMA
Baadhi ya majirani walifika eneo la tukio na kukuta sakata hilo limefikia hatua ya mbwa kutii amri ya bosi wao na kurudi kwenye maskani yao.
Walimchukua mtoto huyo na kumkimbiza kwenye Hospitali ya IMTU iliyopo Mbezi, Dar ambapo madaktari walisema alishafariki dunia kitambo.

VILIO VYATAWALA
Baada ya kuzinyaka taarifa hizo, haraka mwandishi wetu alifika eneo la tukio muda mfupi baada ya mtoto huyo kupelekwa hospitali na kushuhudia vilio vikitawala kwa kila jirani aliyepata taarifa za kifo hicho cha kusikitisha.

MAJIRANI WASIMULIA
Wakionesha jinsi walivyoumizwa na tukio hilo, baadhi ya majirani walisimulia jinsi mbwa hao wanavyowatishia amani katika nyumba hiyo ambapo tangu kigogo huyo ahamie ndani ya nyumba hiyo wamekuwa watu wa kujifungia siku nzima wakihofia mbwa hao wakali.

“Jamani huyu mtoto kafa kifo kibaya sana, mbaya zaidi mbwa hawa wamekuwa tishio kiasi cha watu kushindwa kufanya shughuli zao za kila siku.
“Mbwa huwa hawafungiwi kwenye banda, labda ingekuwa hivyo wasingefanya hivi,” alisema jirani mmoja huku akilia bila kikomo.
POLISI WALIVYOFANYA
Paparazi wetu alipojaribu kuingia ndani na kwenda kuongea na balozi huyo, askari waliodaiwa ni wa Kituo cha Polisi Kawe jijini Dar walitia ngumu huku ikidaiwa kuwa maelezo waliyoyaandika ni mmiliki wa mbwa kuwa mzembe kwa kuwaachia mbwa kudhuru binadamu.

MAMA MZAZI AZIMIA
Maria Mvile, mama mzazi wa marehemu Christian kwa sasa yupo katika hali mbaya tangu mkasa wa kushambuliwa mwanaye na mbwa hao utokee ambapo amekuwa akizimia mara kwa mara.

Mwandishi wetu alimshuhudia mama huyo akishindwa kuweka shada la maua katika kaburi la mwanaye kwa kuanguka na kuzimia.
MAZIKO
Safari ya mwisho ya mtoto Christian ilifanyika kwenye Makaburi ya Mburahati, Dar es Salaam ikitanguliwa na misa iliyosomwa na Katekista wa Kanisa Katoliki Mburahati, Owen Hokororo.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, ACP Camillius Wambura amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kukiri kuwa ni nyumbani kwa balozi wa Qatar nchini.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.

Comments

Popular posts from this blog