KUSAIDIA JAMII KWAMPA CHETI CHA HESHIMA MAMA KIKWETE

IMG_0090Na Anna Nkinda – Brussels, Ubelgiji
 Mke wa Rais Mama Salma Kikwete amepewa cheti na Umoja wa wake wa Mabalozi  wa Afrika waishio katika  nchi za Jumuia ya  Ulaya kwa kutambua na kuthamini mchango wake na kazi anazozifanya za kuwasaidia wanawake, wasichana  na watoto wa Tanzania. 
Cheti hicho amekabidhiwa jana katika hafla fupi  ya chakula cha mchana kilichoandaliwa na wake hao wa mabalozi katika ukumbi wa mikutano uliopo Hoteli ya Sheraton mjini Brussels.
Mama Kikwete ni mmoja kati ya wake wa Marais wa tano wa  Afrika waliokabidhiwa vyeti hivyo vya heshima kutokana na kazi zao wanazozifanya za kuisaidia jamii na kuhakikisha kuwa inapata mahitaji ya muhimu kama huduma ya afya na elimu.

Akiongea kabla ya kuwakabidhi wake hao wa marais vyeti hivyo Mke wa Balozi wa Equatorial  Guinea  ambaye pia ni rais wa umoja huo Mama Mangue de Nvono Nca alisema nia ya kuanzishwa kwa umoja wao ni kulitambulisha bara la Afrika ambalo linajulikana  kuwa na  changamoto za njaa, magonjwa, kutokuwa na haki na  usalama wa kutosha katika nchi za Ulaya.
“Siyo kama Bara letu la Afrika linakabiliwa na changamoto peke yake bali pia limejaliwa kuwa na  umoja, mshikamano na  ukarimu na haya yote yamejidhihirisha  kwetu leo hii kutokana na kitendo cha wake wa marais wetu kushiriki pamoja nasi katika hafla hii  na kubadilishana mawazo”, alisema Mangue de Nvono Nca. 
Alisema umoja huo  unatambua kazi kubwa inayofanywa na wake wa Marais wa Afrika kwa jinsi wanavyowaunga mkono wenza wao kwa  kufanya kazi   ambazo malengo yake makubwa ni  kuwasaidia wanawake, wasichana , watoto na watu ambao wako katika makundi  hatarishi ndani ya jamii. 
Akiongea  kwa niaba ya wenzake mara baada ya kutunukiwa vyeti hivyo Mke wa Rais wa Congo Brazzavile Mama Antoinette N’Guesso  aliwashukuru wake hao wa mabalozi kwa kazi wanayoifanya ya kulitangaza bara la Afrika kuwa ni nchi ya umoja, mshikamano na ukarimu jambo ambalo litaondoa dhana iliyopo miongoni mwa watu kuwa kitu pekee kilichopo barani Afrika ni matatizo.
Wengine waliokabidhiwa vyeti hivyo ni pamoja na  Malkia wa  Swaziland Inkhosikati Zena Seraya Mahlangu, Mke wa Rais wa Madagascar Mama Lalao Rajaonarimampianina, Congo Brazzaville  Mama Antoinette N’Guesso  na  Cameroon  Mama Chantal Biya.
Wake hao wa Marais wameambatana na wenza wao ambao ni Marais wa Afrika wanaohudhuria mkutano wa nne  wa wakuu wa nchi za Afrika na Jumuia ya Ulaya unaofanyika nchini humo.

Comments

Popular posts from this blog