MTOTO ALIYEPOTEA MIEZI MITATU ILIYOPITA APATIKANA AKIWA HAI

Mwenyekiti wa Mujata, Chifu Shayo Soja Masoko  akiwa na mtoto Martha Jackson

Mwenyekiti wa Mujata, Chifu Shayo Soja Masoko akiwa na Familia ya Martha





MWANAFUNZI Marha Jackson(13) wa darasa la sita Shule ya Msingi Mwasote iliyopo Kata ya Nsalaga Uyole Jijini Mbeya, ambaye alitoweka katika mazingira ya kutatanisha nyumbani kwao Disemba 17, 2013 amepatikana eneo la Tunduma akitokea Ilula Mkoani Iringa.
Baadhi ya mashuhuda waliomuona binti huyo walipomuuliza mahala alipokuwa akiishi na mazingira aliyoondokea nyumbani kwao alisema alichukuliwa na bibi yake aliyemtaja kwa jina la Hidaya Yailah Mussa(35)anayemiliki mgahawa eneo la Mtuha uliopo Ilula Mkoani Iringa ambako alidai alikuwa akitumikishwa na bibi yake huyo katika shughuli mbali mbali akiwa na wenzake kumi.
Alisema alichukuliwa na bibi yake huyo kutoka Nsalaga hadi Mlima Nyoka ambapo baada ya kufika huko walipanda kitu kilichodaiwa ni ndege hadi Ilula ambako walipelekwa moja kwa moja kufanya kazi katika mashamba ya Nyanya, Pilipili na Mahindi huku wao wakiwa wakilishwaMananasi na mahindi.
Mwanafunzi huyo alisema siku ya kwanza walifikia makaburini ambako aliwakuta watu wengi ambapo aliweza kuwatambua baadhi yaokwa majina ambapo waliendelea na kazi za bibi huyo hadi siku ambayo aliamua kuondoka na kujikuta akiwa amesimama katika eneo la Sogea Tunduma wilaya ya Momba Mkoani hapa.
Aliongeza kuwa hadi kufika eneo hilo alitumia usafiri ule ule unaodaiwa kuwa ni ndege na baada ya kutua alikutana na mama yake mzazi aliyemtaja kwa jina la Agnetha Joseph(37) Mkazi wa Sogea Mji mdogo wa Tunduma ambaye hakumtambua mara moja kutokana na kutokuwa na ufahamu kwa wakati huo na kumuona kama watu wengine wa kawaida.
Alisema wakiwa shambani walifanyishwa kazi bila malipo yoyote na kuambulia kulishwa mahindi na mananasi huku Nyama wakilishwa mara chache baada ya kuletewa na bibi yake huyo.
kwa upande wake mama mzazi wa binti huyo Agnetha Joseph alisema alipatwa na mshtuko kuona mwanae akiingia nyumbani huku akiwa amechafuka sana majira ya saa tatu usiku huku akiwa hana fahamu sawa sawa hali iliyomlazimu kumpeleka Nsalaga alikokuwa akiishi awali na bibi yake.
Kupatikana kwa mtoto huyo kumetokana na juhudi zilizofanywa na Muungano wa Jamii Tanzania(MUJATA) ambao mara nyingi wamekuwa wakikemea vikali vitendo vinavyotokana na imani za kishirikina ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya.
Mwenyekiti wa Mujata, Chifu Shayo Soja Masoko alisema kupatikana kwa mtoto huyo akiwa ni mzima ni kutokana na taarifa walizozipata kutoka kwa wataalamu wa jadi waliobainishwa uwepo wa mtoto akiwa hai na kuchukuliwa kwa imani za kishirikina.
Alisema baada ya kufanya vitu vyao waliweka mtego wa kumbaini mtu anayehusika na vitendo hivyo jambo ambalo lilizaa matunda kwa kujitokeza mbele yao Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Hidaya Mussa ambaye aliwasili Mbeya Machi 15 akiwa ameambatana na baba mzazi wa binti huyo aliyejulikana kwa jina la Kulwa Khatibu.
Mzazi wa Binti huyo Kulwa Khatibu ambaye ni mkazi wa Tabata Jijini Dar Es Salaam alisema hakuwa na taarifa za kupotea kwa mtoto wake kutokana na yeye muda mwingi kuwa kikazi Mkoani Mtwara hivyo kukosa imani na taarifa za kupotea kwa mwanae huyo hadi aliposikia ameonekana jambo lililomlazimu kufika kujionea hali halisi.
Kwa upande wake Chifu Soja alipomhoji Hidaya kuhusiana na upotevu wa Mwanafunzi huyo alikiri kumuona Ilula na kuongeza kuwa kuna mzee mmoja kijijini kwao ambaye anahusishwa na matukio ya kuwachukua misukule watoto wa watu na kuahidi kutoa ushirikiano kwa Mujata ili kumbaini mzee huyo jambo ambalo halikueleweka vizuri kwa wananchi waliokuwa wamefurika hadi na kuzua taflani iliyolazimu Jeshi la Polisi kumchukua na kuondoka naye.
Mwisho.

NaEzekiel Kamanga
Mbeya yetu

Comments

Popular posts from this blog