KUTANA NA MTOTO WA KWANZA KUZALIWA KWA NJIA YA UPANDIKIZAJI NCHINI

 Unapoingia katika nyumba ya familia ya Salehe Saidi, macho  na masikio yako hayawezi kukwepa  ucheshi wa kijana wa miaka 13, Jumbe Salehe. Ni kijana anayeipa tabasamu familia hiyo.
Jumbe ni mwenye nguvu, afya, akili darasani na uchangamfu ambao kila mzazi angependa kuuona kwa kijana wake. Lakini Jumbe Salehe, hakuzaliwa kama watoto wengine. Alipatikanaji katika mchakato mrefu, uliohusisha teknolojia ya hali ya juu  na majaribio yaliyohitaji werevu. Jumbe alizaliwa kwa njia ya upandikizaji wa mbegu ambao kwa jina la kitaalamu unajulikana kama In-Vitro Fertilization (IVF). Mchakato huo ulisimamiwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Profesa Malise Kaisi.
Kwa nini Jumbe alizaliwa kwa njia ya IVF?
Mwanaidi Kombo, mama mzazi wa Jumbe, hakuwa na tatizo la uzazi hapo awali. Alifanikiwa kupata mtoto wake wa kwanza mwaka 1986.
Mwaka 1988 alipata ujauzito mwingine lakini kwa bahati mbaya, uliharibika na kuanzia hapo ikawa ni vigumu kwake kushika mimba nyingine.
“Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu nikajaribu kupata mtoto, lakini tatizo jingine likaanza. Mwaka 1990. Nilianza kupata maumivu makali ya tumbo,” anasema Mwanaidi.
Kutokana na maumivu hayo, alianza kusaka msaada wa kitabibu na alishauriwa kwenda kwa daktari wa magonjwa ya wanawake, Dk. Malikiti wa Hospitali ya MM.
Safari yake kwenda kwa daktari ilimsaidia kung’amua ukweli, kwani aliambiwa kuwa ana uvimbe mkubwa kwenye kizazi ambao unaweza kuhatarisha maisha yake na kuwa ndicho chanzo cha kushindwa kupata mtoto.
Hata hivyo, Dk. Malikiti alimuelekeza aende kuonana na Profesa Kaisi kwa kuwa ndiye mtaalamu wa masuala ya uzazi kwa wanawake.
“Nilipofika kwa Dk. Kaisi, nilimshangaa baada ya kuisoma picha ya Xray. Aliniambia niache kabisa kunywa dawa nilizoandikiwa za maumivu na kuambia ninywe panadol endapo nitakuwa na maumivu,” anasema.
Ingawa Mwanaidi alishangaa, aliendelea na kliniki ya Dk. Kaisi akihudhuria  kila wiki kwa zaidi ya miezi miwili.
Siku moja Dk. Kaisi akaamua kumfanyia kipimo cha CT Scan  kuangalia mirija ya uzazi na ndipo alibaini kuwa pamoja na uvimbe, mrija wake mmoja umepinda.
“Aliniambia niende nyumbani na nirudi baada ya mwezi mmoja kwa ajili ya upasuaji, lakini wakati huo alinipa masharti mengi kama nisinywe kabisa chai,” anasema.
 Baada ya mwezi mmoja, Mwanaidi alirudi kwa Dk. Kaisi ambaye alimwambia ni lazima amfanyie upasuaji mdogo kwanza kwa ajili ya kurekebisha mirija ya uzazi.
Katika upasuaji huo, ambao kitaalamu unaitwa ‘ovary re-implantation’, madaktari walirekebisha mirija hiyo kwa kufunga  kifaa maalumu.
Mwezi mmoja baadaye Mwanaidi alirudi kwa daktari ambaye aligundua kuwa bado mwanamke huyo ana uwezo mkubwa wa kuzaa kwani alikuwa na mayai ya kutosha kumuwezesha kushika ujauzito.
“Aliniambia nina mayai ya kutosha, lakini  tatizo ni hilo la uvimbe na kupinda kwa mirija ya kusafirisha mayai ya uzazi na mbegu,” anasema.
Baada ya hapo, Mwanaidi alifanyiwa upasuaji mwingine mkubwa kwa ajili ya kuondoa uvimbe. Zoezi hilo lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa ingawa siyo kuondolewa kizazi.
Baada ya hatua hii, Profesa Kaisi alimshauri Mwanaidi kuendelea kutafuta mtoto mwingine kwa sababu anao uwezo wa kubeba mimba ingawa itakuwa vigumu kwa yeye kupata ujauzito huo kwa njia ya kawaida.
 Profesa Kaisi anasema aliwashauri kuwa wanaweza kupata ujauzito kwa njia ya upandikizaji  jambo ambalo lilikubaliwa mara moja na wazazi hao. Disemba 2012, Mwanaidi alifanikiwa kushika ujauzito kwa njia ya IVF. Iliwezekana baada ya  mbegu za mume wake na mayai yake (Mwanaidi) yaliyopevushwa, kutolewa na baadaye kupandikizwa katika nyumba ya uzazi ya Mwanaidi.
“Baada ya mchakato huo kumalizika nilitakiwa kuhudhuria kliniki kila wiki kwa ajili ya kuangaliwa jinsi mimba inavyokua,” anasema Mwanaidi.
Mwanaidi anasema katika ujauzito ule hakuwa akiumwa au kupata matatizo yoyote kama ilivyokuwa kwenye ujauzito wake wa kwanza. Alikuwa na hali ya kawaida kabisa kuliko alivyotarajia.
Anasema Profesa Kaisi alimwambia kuwa huenda angejifungua Agosti 17, mwaka 2000 na ikawa hivyo. Alijifungua siku hiyo saa 2:00 usiku kwa njia ya upasuaji.
“Namshukuru Mungu kuliko kawaida. Huu kwangu ni muujiza na ninamshukuru sana Profesa Kaisi kwa uwezo ambao Mungu amempa,” anasema Mwanaidi.
Mwananidi anamwelezea mtoto wake kuwa ni mwenye nguvu, mwili  mkubwa, na mcheshi.
“Ni mtoto wa kawaida kabisa, ana uwezo mkubwa darasani na alifaulu vizuri mtihani wa darasa la saba. Ni mtoto mwenye kumbukumbu za ajabu,” anasema mama huyo wa Jumbe.
 Mwanaidi anasema kwa kuwa sasa ana watoto wawili, bado anatamani mtoto mwingine na anasema iwapo Profesa Kaisi angekuwa hajapooza, angeomba apate mtoto mwingine kwa njia ya IVF.
“Kuugua kwa Prof. Kaisi ni pigo kwa kila mtu. Wapo mamia ya wanawake wanaohitaji huduma za uzazi... kwa kweli sijui itakuwaje,” anasema.
 Si hivyo tu. Mwanaidi anasema Profesa Kaisi hakuwahi kuwalipisha hata senti tano ya matibabu tangu alipofanyiwa upasuaji wa uvimbe hadi alipopata ujauzito kwa njia ya IVF.
 Profesa Kaisi anasema hakuweza kuwalipisha fedha katika mchakato huo kwa sababu matibabu hayo yalikuwa chini ya programu iliyodhaminiwa na watu kutoka nje, ambao walilipia gharama zote.
IVF hufanyikaje?
Profesa Kaisi anasema yai la mama hupevushwa  kwa kutumia dawa maalumu na hufuatiliwa  kwa kutumia mashine ya uchunguzi wa ndani ya mwili(Ultrasound).
“Baada ya yai kukomaa, sindano maalum yenye wembamba mithili ya unywele huingizwa ukeni hadi kwenye mirija na yai lililopevuka huchukuliwa na kutolewa nje,” anasema.
Yai  au mayai hayo  huwekwa kwenye chombo maalumu (test tube) kabla ya kuhamishwa  kwenye beseni maalumu ambalo hufanya yai liendelee kuwa hai licha ya kutoka nje ya mwili wa binadamu.
“Beseni hilo halina budi kuwa na mazingira kama ya mwilini. Kwa mfano joto, mwanga na kusiwepo na sauti, kwani yai huweza kuharibika kwa kasoro ndogo ndogo sana,” anasema.
Anasema wakati huo  mbegu za mwanaume hupimwa kama hazina walakini na  hutolewa kwa mwanaume kujichua au kama hawezi kujichua basi hutakiwa kufanya tendo la ndoa na mke wake na kisha mbegu kukingwa kabla ya kuwekwa kwenye chombo maalumu.
Mbegu za baba hutakiwa kutolewa saa mbili mara tu baada ya  yai la mama kutolewa ili visipishane.
“Baada ya yai na mbegu kutolewa,  hatua inayofuata ni kuichoma mbegu kwenye yai kwa kutumia sindano maalumu. Mchakato huu unaitwa kwa kitaalamu, Intra Cytoplasmic Sperm Injection au ICSI),” anasema.
Anaeleza kuwa, baada ya mbegu na yai kuchanganywa, huwekwa kwenye chombo maalumu cha  joto kitaalamu ‘Incubator” kwa saa 40 kabla ya kuwekwa  au kupandikizwa kwenye kizazi cha mama.
“Hali kadhalika ‘incubator’ inatakiwa kuiga hali ya tumboni mwa mama wakati yai la mama na mbegu za baba vinapowekwa kabla ya kuwekwa kwenye kizazi cha mama, kwa mfano joto, mwanga na sauti,” anasema Profesa Kaisi.
Profesa Kaisi anasema IVF ina mafanikio makubwa kwa mtu yeyote isipokuwa wanawake wenye umri wa miaka 40 na kuendelea. Anaeleza zaidi kuwa, wanawake walio wengi hudhani kuwa ni wagumba lakini kumbe hawajafahamu matatizo yao

Comments

Popular posts from this blog