HATA KAMA YUKO MBALI, UNAWEZA KUWA KARIBU NAYE!
UMBALI katika uhusiano, mara nyingi husababisha hofu. Fikra za usaliti hutawala sana kwa wenzi wanaoishi mbali. Lakini vipi, mwenzako asisafiri au asiishi mbali kwa kuhofia hayo wakati kitendo hicho kinasababishwa na jukumu la kikazi?
Ndugu zangu, baadhi yetu, kama hatutakuwa makini, umbali huweza kuchochea usaliti. Lakini kuna njia ambazo zikitumika kwa usahihi, husaidia kuliweka penzi hai na kuzidi kuwa na mshawasha mkubwa.
Wiki iliyopita nilianza kwa kueleza umuhimu wa mawasiliano, hasa simu, waraka pepe na mitandao ya kijamii. Kuweka utani kwa mwenzako, kusoma ratiba yake na kuishika siku yake sawasawa kunamfanya mwezako asikusahau na wakati fulani ahisi kukukosa.
Zawadi ni kati ya mambo ambayo humfanya mpenzi wako afurahie uhusiano wake na wewe. Hakuna zawadi za moja kwa moja ambazo ni rasmi kwa ajili ya mwenzi wako, lakini ni vyema ukamtumia zawadi kulingana na mapenzi yake zaidi.Kwakuwa wewe unamfahamu zaidi mwenzi wako, unaweza kujua zawadi gani ni nzuri zaidi kwake au anayopendelea kuliko aina nyingine. Katika vijipengele vifuatavyo, nimechambua aina kuu za zawadi ambazo ukimtumia mpenzi wako unamteka hisia zake na kuona kama yupo karibu na wewe hata kama yupo mbali.
(i) Mavazi
Mavazi ni kati ya zawadi ambazo zitamfanya mpenzi wako azidi kukupenda na kuwa karibu zaidi na wewe. Kama nilivyotangulia kusema awali, aina ya nguo ambazo unaweza kumtumia mpenzi wako ni zile ambazo unadhani atavutiwa nazo zaidi au zile ambazo zitampendeza na kumfanya aonekane nadhifu.
Hata hivyo, zipo aina za mavazi ambazo zimependekezwa zaidi kwa ajili ya wenzi kutumiana wanapokuwa mbali.
KWA WANAUME:
Kama wewe ni mwanamke unataka kumtumia mwenzi wako wa kiume, mavazi haya yanafaa zaidi. Saa nzuri ya mkononi, nguo za ndani, lakini lazima uzingatie rangi ya bluu, bluu bahari au nyeupe kimsingi zisiwe za rangi inayoficha uchafu.
Zingine ni fulana za ndani, tisheti, mkanda wa kiunoni, simu ya mkononi, vitambaa vya jasho n.k. hakikisha katika zawadi zako hizo, unaambatanisha na manukato mazuri (hasa unayotumia wewe).
Haishauriwi kumtumia suruali au shati kwa sababu inaweza kuwa kubwa au ndogo, hivyo kupunguza ladha ya zawadi hasa kama atakuwa ameipenda. Zawadi za aina hiyo, unaweza kumpa mwenzi wako ofa ya kwenda kuchagua moja kwa moja dukani.
KWA WANAWAKE:
Kama wewe ni mwanaume na unataka kumtumia mpenzi wako wa kike zawadi, lazima uwe makini sana! Mavazi yaliyopendekezwa hapa ni pamoja na batiki (gauni, blauzi na sketi, blauzi yenyewe n.k), hereni, bangili, mkufu wa vito, simu, saa, nguo za ndani, viatu n.k.
Kama umesoma vizuri utaona mwanamke anaweza kununuliwa vitu vingi zaidi, tofauti na mwanaume. Hii inatokana na aina za mavazi na saizi zao kukaririka kirahisi zaidi au kutokuwa na saizi ya moja kwa moja.
Kama kawaida, mavazi haya ambatanisha na manukato mazuri sana, hasa yale ambayo unapenda kutumia wewe. Ninaposema uweke manukato unayotumia, maana yake itamsaidia kumsogeza karibu zaidi kihisia kwa kuhisi harufu yako.
Wiki ijayo tutaendelea na mada yetu, USIKOSE!
ILA USISITE KUKUTUMIA MAONI YAKO NDUGU MDAU WETU
Comments
Post a Comment