DK. MARIA KAMM AIBUKA KIDEDEA TUZO YA MWANAMKE BORA

kammm (1)WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewataka wanawake walioteuliwa kwenye Tuzo ya Mwanamke Bora wa mwaka 2013/2014 wasibweteke bali waendeleze juhudi zao na wazidi kung’ara zaidi.Ametoa wito huo jana usiku (Jumamosi, Machi 29, 2014) kwenye hafla ya kumtuza mwanamke bora wa mwaka 2013/2014 iliyofanyika kwenye ukumbi wa African Dream nje kidogo ya mji Dodoma.“Lazima muendelee kuonekana mnazidi kung’ara. Tuzo ni njema kwa upande mmoja lakini pia ina changamoto zake kubwa ikiwa ni ya kuendelea kubaki mnang’ara hadi waliowapigia kura wakawaona mnafaa,” alisema Waziri Mkuu.Utoaji wa tuzo hiyo uliwapambanisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka; Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro; Mwalimu Mkuu Mstaafu na Mbunge Mstaafu, Dk. Maria Kamm pamoja na Mbunge wa Same Mashariki, Bi. Anne Kilango Malecela.
Kila mmoja alikabidihiwa Tuzo ya Mwanamke Bora na Waziri Mkuu Pinda lakini Dk. Maria Kamm ndiye aliyeibuka mshindi wa jumla kwa kukabidhiwa medali maalum pamoja na hundi ya sh. milioni tano.
Waziri Mkuu alipongeza Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Global Publishers, Bw. Eric Shigongo kwa kuthamini mchango wa wanawake katika jamii na kuanzisha wazo la kutoa tuzo hiyo.
Alimtaka Bw. Shigongo aangalie uwezekano wa kuiendesha tuzo hiyo iendane na maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8, kila mwaka. “Kabla ya siku hiyo, kuwe na wiki nzima ya maadhimisho, iendeshwe mijadala kuhusu shughuli za wanawake, mada zinazohusu masuala hasi na chanya ya wanawake zitolewe,” alisema.
“Ningependa kuona viongozi wa Kitaifa wakiibeba Wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake kama njia ya kutambua mchango wa wanawake kwenye Taifa hili. Tunao mwaka mzima wa kujiandaa kwa ajili ya jambo hili, tutashirikiana kadri inavyowezekana,” alisisitiza.
Wanawake waliopewa tuzo walimshukuru Bw. Shigongo kwa kutambua jitihada za wanawake mbalimbali hapa nchini na kuamua kuazisha tuzo hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
DODOMA.
JUMAPILI, MACHI 30, 2014

Comments

Popular posts from this blog