DAWA YA MALARIA YA METAKELFIN YAMGEUZA KIJANA WA KIUME KUWA ALBINO MKOANI TABORA.


AMA kweli hujafa, hujaumbika. Usemi huu una maana kubwa kwa kijana Hafidh Masokola, mkazi wa eneo la National Housing mkoani Tabora ambaye kwa miaka zaidi ya 40 alikuwa na ngozi isiyo na chembe ya tatizo, lakini sasa amegeuka albino. Kwa mujibu wa Masokola, ambaye sasa ana umri wa miaka 47, alipata tatizo hilo kutokana na madhara ya dawa ya malaria aliyoimeza aina ya Metakelfin miaka minne iliyopita. 

Na kutokana na tatizo hilo la kiafya lililobadilisha kabisa ngozi yake, amelazimika kujiunga na Chama cha Maalbino Tanzania. Masokola, mwenye mke na watoto watatu, anasema alipata uthibitisho wa kuathiriwa na aina hiyo ya dawa baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kimaabara katika hospitali kadhaa, ikiwemo ya KCMC iliyopo Moshi, mkoani Kilimanjaro. 
Katika mazungumzo na gazeti hili hivi karibuni, kijana huyo alisema aina hiyo ya dawa ilimponza kwa kunywa vidonge vitatu tu katika dozi yake ya kwanza mnamo Julai mwaka 2010. Akisimulia zaidi, alisema; “Baada ya kupima malaria katika hospitali ya mkoa ya Kitete, nilikwenda duka la dawa na kununua hii Metakelfin, sikuwahi kutumia dawa nyingine kabla ya hapo. 
“Hata kabla sijarudia dozi ya pili ambayo huwa ni baada ya siku saba, damu ilianza kuvilia kwenye nyayo za miguu na viganja vya mikono. Nikalazimika kwenda tena hospitali ya mkoa kwa ushauri wa daktari wangu, George Msalale, nikaambiwa nitumie mafuta mazito kukabili mzio wa dawa. 
“Sikuwa nawashwa, ila hali hii ya maumivu iliendelea kwa takribani wiki nne. Hali ya kuvilia damu ikasambaa katika sehemu nyingine za mwili huku ikianza kutoa madoadoa. Aidha, ngozi ilianza kubadilika ikawa na makunyanzi na kavu, ikanibidi niwe mtu wa kutembea na mafuta mazito ya Vaseline ili nijipake mara kwa mara.” Anasema pamoja na juhudi hizo, hali haikubadilika na akaongeza kutumia losheni aina ya “hydrocortisone cream”. 
“Baada ya kutumia mafuta na cream hiyo, ngozi ilibadilika rangi na kuwa nyeusi, iliyopauka kama mtu aliyemwagiwa gundi. Lakini mabadiliko hayo hayakuathiri sehemu zake za nywele licha ya nyayo na viganja kukakamaa mithili ya magome ya mti. Macho pia yaliathirika kwa kupunguza nuru ya kuona, nikawa naona ukungu zaidi, huku nikiwa na homa za mara kwa mara,” anasema. 
Kutokana na hali hiyo, aliendelea kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya ambapo walimbadilishia dawa na kumpa shampoo ya kuoga iliyomsaidia kuondoa magamba kwenye ngozi yake ingawa aliendelea kuwa na mabaka meusi na meupe. 
Aidha, katika kipindi hicho anasema; “midomo yake ilipasuka pasuka nikawa nashindwa kula chakula vizuri na wakati mwingine ilibidi kutumia tishu au kitambaa kuzuia damu iliyokuwa ikitoka mdomoni wakati wa kula.” 
Pamoja na kupasuka kwa midomo, nywele zake pia zilianza kukatika na kung’oka huku kichwa kikiwa na kitu mithili ya ukoko na kutoa vidonda vyenye maji. Na kufikia Januari mwaka 2011, mara nyingi akikumbana na maumivu ya kichwa mara kwa mara, alijikuta hana nywele kabisa na badala yake kichwa kikifunikwa na ngozi iliyokakamaa. 
Kutokana na hali kuzidi kuwa mbaya, anasema alilazimika kurudi tena hospitali ya Kitete alikoshauriwa kutumiwa sabuni za ngozi na losheni aina ya “beta cort- N” anayosema ilimsaidia kuondoa ngozi ngumu na kuotesha nywele, lakini zikiwa nyeupe badala ya nyeusi kama alizokuwa nazo kabla ya kuugua malaria. 
“Na ngozi yangu yote ya mwili ilipoteza vinyweleo na kubadilika rangi kutoka ya asili niliyokuwa nayo na kuwa nyeupe kama ya mzungu. Hapo ikabidi nilazwe kwa uchunguzi wa kina hapo hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora. Mambo yalikuwa magumu, nikaandikiwa rufaa kwenda KCMC kwa uchunguzi zaidi. 
“Agosti 22 ya mwaka 2011 niliwasili KCMC na kuanza matibabu baada ya kufanyiwa vipimo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kukatwa sehemu ya nyama ya paja kwa uchunguzi. Vipimo vilionesha nimepatwa na madhara ya dawa nilizotumia na kupata ugonjwa aina ya “Psonasis” ambao umesababisha kupoteza rojo chembe yaani “melanin” inayosababisha kupotea kwa rangi ya ngozi. 
Mimi nilipoteza rangi nyeusi na kupata huu ualbino,” anasema na kusisitiza kuwa, hakuwahi kutumia dawa nyingine zaidi ya Metakelfin. Kutokana na kubainika kwa tatizo lake, alishauriwa kutumia mafuta maalumu kwa lengo la kutakatisha ngozi, huku akielezwa kuwa kama akifuata ushauri, baada ya muda ngozi inaweza kurudi katika hali yake ya asili. 
“Nilipotumia mafuta hayo mazito, magamba yaliyokuwa kwenye ngozi taratibu yaliondoka na kubaki na ngozi nyeupe. Kucha za mikono na miguu zilizokuwa zimeng’oka na ngozi za nyayo za viganja vilianza kujitengeneza upya,” anaeleza. 
Anaongeza kuwa, akiwa KCMC alipatiwa elimu ya kutunza ngozi kutokana na michubuko na kujikinga mionzi ya jua ambayo inaweza kumsababishia saratani ya ngozi. 
Anasema alielimishwa namna ya kutumia losheni za aina mbalimbali ili kutunza ngozi ikiwa ni pamoja na “betamethasone cream au beta cort- N ambapo kwa sasa anatumia Sun block- SPF 60 cream, pia anatumia mafuta ya Vaseline yenye mchanganyiko wa vitamin A na vidonge vya vitamin A. 
Aidha, anatakiwa kuhudhuria kliniki maalumu ya ngozi katika hospitali ya KCMC mara moja kwa mwaka. Akizungumzia athari anazozipata kutokana na ulemavu wa ngozi alioupata akiwa mtu mzima, anasema kuwa ni pamoja na unyanyapaa na kushindwa kufanya shughuli zake za ujasiriamali ambazo kwa sehemu kubwa alikuwa akizifanya akiwa juani. 
Kwa sasa, muda wake mwingine anautumia kuwa muelimishaji wa VVU na Ukimwi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Tabora huku pia akiutumia muda wake mwingine katika shughuli za chama cha albino wilayani Uyui, Tabora. 
Anasema lengo lake kubwa ni kuendeleza harakati za kuelimisha umma kutambua thamani ya utu wa binadamu kwani hakuna ajuae ni lini ataingia kwenye kundi la watu wenye ulemavu. Baba huyo wa watoto watatu, Juma (20), Sizya (16) na Radhia (15) aliozaa na mkewe Hanzelani Kauzu, anasisitiza; “Mungu amenichagua mimi kuwa mfano kwa watu wengine ambao wanaendeleza mauaji kwa albino, kwani hata wao wanaweza kubadilika na kupata ulemavu wa ngozi kama yeye na kwamba hakuna haja ya kufanya mauaji ya albino.” 
Mkewe ameizungumzia hali ya mumewe kuwa ni changamoto kubwa kutokana na baadhi ya watu kuihusisha na imani za kishirikina, huku akisisitiza kama familia wamekubaliana nayo na wako imara katika kuhakikisha maisha yanaendelea kama ilivyokuwa kabla ya ulemavu wa mumewe. 
Akiizungumzia hali hiyo, mmoja wa madaktari bingwa nchini, Dk Ali Mzige alisema matukio ya aina hiyo yapo. Dk Mzige aliyewahi kuwa Mganga Mkuu wa Wizara ya Afya, alisisitiza kuwa Metakelfin na dawa nyingine zenye salfa huwa na madhara kutegemea na mtu na mtu. 
Alisema wakati mwingine hutegemea na afya ya mtu na historia ya magonjwa mbalimbali. Hata hivyo, alishauri kwa yaliyomkuta Masokola, ni vyema akazingatia ushauri wa madaktari, huku akimtaka kutopuuzia matumizi ya losheni na kufanya mazoezi ili kujikinga na uwezekano wa kupata ugonjwa wa saratani

Comments

Popular posts from this blog