CHADEMA YAAHIDI MAKUBWA CHALINZE ENDAPO WATAICHAGUA
Mwenyekiti
wa Baraza la Vijana (Chadema) Mkoa wa Pwani, Elison Kinyaha amesema
ili kudumisha maendeleo, upendo na amani ndani ya Jimbo la Chalinze, upo
ulazima wa wakazi wa jimbo hilo kumchagua Mathayo Torongey katika
uchaguzi mdogo unaotarajia kufanyika mapema Aprili 6, mwaka huu.
Kinyaha
alisema kutokana na uelewa mpana wa wakazi wa jimbo hilo ni wazi kuwa
chama hicho ndicho kinachoweza kuibuka na ushindi kwani mtu anayegombea
nafasi hiyo ni mpigania haki za wanyonge na anayetambua shida
zinazowakabili kwa kipindi kirefu.
Alisema
kumpitisha mgombea huyo hawakukurupuka bali walitumia utashi na heshima
kubwa iliyomo ndani ya uongozi wa Chadema, hivyo mpaka sasa wanatambua
kuwa, kazi wanayoifanya sasa ya kampeni si ya kubahatisha bali ni
kushika uongozi wa ubunge ndani ya Jimbo la Chalinze.
“Sisi
leo tuko Kata ya Pera na Kijiji cha Chamakweza, tukiendelea na kampeni
ambayo tuliizindua tangu Jumapili. Kikubwa ni kuzungumza na wananchi kwa
ustaarabu na kuwajulisha chama wanachopaswa kukichagua ambacho ni
Chadema pekee kinachojali shida za wanyonge,” alisema
Alisema
kuwa katika kipindi kifupi tangu chama hicho kilipozindua kampeni, hali
ya mwitikio imekuwa ya kutia matumaini hususan katika mahudhurio ya
kampeni kwenye maeneo mbalimbali na kudai hilo linaonyesha ni kukubaliwa
kwa sera za chama hicho ambazo zaidi zinajikita kwenye kutetea wanyonge
na usawa.
Alisema
katika zoezi zima la kampeni, chama chao kitafanya kazi hiyo kwa
ustaarabu na kuepusha vurugu na ni imani yake wana Chadema wote
watajiepusha na hali yoyote inayoweza kutokea kwa upande wa vyama
vingine.
Wakati
huohuo juzi, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza alisema katika
kuhakikisha Uchaguzi wa Jimbo la Chalinze unafanyika kwa amani na
utulivu ni vyema viongozi wa dini zote wakafanya maombi kwa Mungu.
Alisema
viongozi hao wanayo nafasi kubwa kutokana na imani tangu enzi na
kuwataka kuhubiri mema kwa waumini wao ambao wengi ni wafuasi wa vyama
vinavyoshiriki uchaguzi huo mdogo.
“Ndugu
zangu viongozi wa dini, msijisahau katika maombi yenu ombeeni na huu
uchaguzi mdogo utakaofanyika mapema mwezi ujao ili haki, amani na hekima
itawale kwenye zoezi zima la kazi hiyo muhimu,” alisema.
Comments
Post a Comment