STAREHE NA WABONGO NI KAMA MAPACHA...HATUOGOPI KITU TUNAPOSIKIA MATANUZI....!SOMA ZAIDI HAPA...!


Taasisi isiyo ya kiserikali inayojishughulisha na masuala ya Madeni ya Taifa na Maendeleo (TCDD), kila mwaka imekuwa ikitoa taarifa kuhusu kukua kwa deni la taifa na kuihadharisha Serikali ya Tanzania kuhusu tabia yake ya kupenda kukopa kwa ajili ya matumizi yasiyo na msingi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Hebron Mwakagenda, Serikali imekuwa ikikopa fedha kwa ajili ya matumizi yasiyo muhimu na ndiyo sababu ya kukua kwa deni la taifa.

Serikali imetamba kuwa itaendelea kukopa kwa sababu Tanzania ina rasilimali nyingi ambazo inaweza kuzitumia kuweka rehani ili ipate mikopo na haijafikia hatua ya Serikali ishindwe kukopesheka.
\
Hii ni akili ya ajabu kabisa, kwamba unakopa kwa rasilimali ulizonazo ambazo nyingine hata hujaanza kuzivuna, bila ya kuzingatia kuwa rasilimali hizo siyo zako peke yako ni kwa ajili pia ya vizazi vingi vijavyo.
Serikali inachofanya ni ulafi, ponda mali, kufa kwaja. Kwa sababu inafahamu awamu hii itaondoka madarakani na itakuja awamu nyingine na itakuwa imewaachia mzigo mkubwa wa madeni, shauri zao wenyewe, watajijua!

Hapa ndipo tunapomkumbuka Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jinsi alivyolinda rasilimali za nchi, hakuwa tayari madini yaliyopo yachimbwe hadi pale watoto wa Kitanzania watakapokuwa na elimu ya kutosha kuwawezesha kuchimba madini yao na kuyatumia kwa busara.

Hakuwa tayari kuwaachia wawekezaji wachimbe madini na kuwaachia Watanzania mahandaki.
Mwaka 2011, deni la taifa lilikuwa ni Sh21 trilioni, miaka miwili baadaye deni limefikia trilioni 27, ukiuliza limefikaje? Utaambiwa ni gharama za uendeshaji Serikali zikiwamo posho, gharama za safari (ndani na nje), mafunzo (ndani na nje ya nchi), mafuta na vilainisho, viburudisho, ununuzi wa magari, ununuzi samani, ununuzi wa vifaa (sare, stationary n.k) upangaji holela (Dodoma na Dar es Salaam) gharama kubwa za matengenezo na ukarabati (barabara, majengo na magari), uhamisho holela na mishahara hewa, mambo haya yote ndiyo TCDD iliyoyasema kuwa ni gharama zisizo za lazima.

Katika kikao cha Bunge kilichoketi Juni mwaka jana, mbunge wa Tumbe kwa tiketi ya Chama cha Wananchi- CUF, Abdallah Rashid Ali aliyadadavua matumizi ya Serikali na kusema kwamba ”siku nyingi Serikali ilikuwa inaahidi kupunguza matumizi ambayo siyo ya lazima, lakini jambo hili linafanywa kinyemela na kwa usiri mkubwa sana. Nasema hivi kwa sababu, ukiangalia mafungu kwa ujumla ya warsha, mwaka jana (2012) ilikuwa ni bilioni 66, lakini mwaka huu (2013) ni bilioni 79, kuna ongezeko la bilioni 13, haya ni matumizi ya warsha tu.

“Kuna vinywaji na viburudisho, mwaka jana ilikuwa bilioni 19, lakini mwaka huu ni bilioni 24, ni ongezeko la bilioni tano. Ofisa pamoja na watu wengine wanakaa ofisini, wanakula na kunywa, tumeongeza bilioni tano.


“Mafuta, mwaka jana ilikuwa bilioni 66, lakini mwaka huu yamepanda bilioni 70 na kwa hiyo, kuna bilioni nne zimeongezeka, ni sawa na asilimia sita. Kuhusu safari pia zimeongezeka, mwaka jana ilikuwa bilioni 147, lakini mwaka huu ni bilioni 163, ni ongezeko la bilioni 16, ni ongezeko la asilimia 12. Bado haya ni matumizi ya kawaida, fedha nyingi zinatumika katika matumizi ya kawaida. Kwa hiyo, waziri bado hajaamua kupunguza matumizi ambayo siyo ya lazima.”
 Pamoja na angalizo hilo lililotolewa na mbunge, bado Serikali imeweka pamba katika masikio, bado inaendelea kuwabebesha wananchi mzigo mkubwa wa madeni kwa sababu ya kukidhi matumizi haya yasiyo ya lazima.

Comments

Popular posts from this blog