RUKUVI ARIDHIKA UKUMBI WA BUNGE LA KATIBA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi jana alitembelea ukumbi wa Bunge maalum la Katiba, linalotarajia kuanza Februari 18, mwaka huu na kujiridhisha na marekebisho ambayo yamefanyika.
Akizungumza na waandishi wa habari, Lukuvi alisema viti 676 vimeshafungwa pamoja vipaza sauti vyake.
Alisema maeneo kwa ajili ya chakula kwa wajumbe tayari yamekamilika, ofisi za viongozi wakiwemo Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti watakaoteuliwa tayari pamoja na kumbi nyingine ndogo.
Lukuvi alisema Ofisi ya Bunge imeshatafuta kumbi nyingine nje ya Bunge, kwa ajili ya kufanyika mikutano itakayohitaji wajumbe wengi.
"Maandalizi ya msingi sasa yameshakamilika, kilichobaki Katibu wa Bunge na Naibu wake ambaye ni Katibu wa Baraza la Wawakilishi watangaze siku ya kuja," alisema Lukuvi.
Hata hivyo, alisema wabunge wote watatakiwa kuwepo Dodoma kabla ya Februari 18, siku ambayo vikao vya bunge hilo vinaanza.
"Siku moja kabla ya vikao kuanza, wabunge wataitwa katika ukumbi huu kupewa maelekezo ya jinsi ya kukaa na jinsi ya kutumia vifaa vilivyomo ikiwemo vipaza sauti," alisema Lukuvi Februari mosi mwaka huu Rais Jakaya Kikwete alitembelea na kukagua ukumbi huo, kuona maandalizi yanavyoendelea na aliahidiwa kuwa Februari 10 maandalizi yote ya uwekaji viti na vipaza sauti, yangekuwa yamekamilika.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Seif Sharif Hamad ametaka wajumbe wa Bunge la Katiba kutoka Zanzibar, kuweka maslahi ya taifa mbele na kuachana na ushabiki wa kisiasa.
Alisema hayo Chake Chake Pemba wakati akihutubia wananchi na wafuasi wa chama katika mkutano wa hadhara. Alisema wajumbe hao wamebeba majukumu makubwa ya hoja mbali mbali za kunufaisha Zanzibar katika mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
“Mchakato wa kupata wajumbe wa Bunge la Katiba sasa umekamilika ambapo wajumbe wanatakiwa sasa kuweka maslahi ya taifa mbele na sio ushabiki wa vyama vya siasa,” alisema.
Wakati huo huo Kamati Kuu ya Chama cha Sauti ya Umma (SAU) imempongeza Rais Jakaya Kikwete anavyoendesha mchakato wa mabadiliko ya Katiba kwa uhuru na uwazi. Mkurugenzi wa Uenezi na Uchaguzi Taifa wa SAU, Johnson Mwangosi alisema jana wanajivunia kuwa na Rais Kikwete .
Alisema bila kujali itikadi za kisiasa, alikaa na viongozi wa vyama vya siasa kitendo ambacho ni cha kiungwana.
Aidha kamati hiyo imesema inaamini itawakilishwa vizuri kupitia wawakilishi wake, Yusuph Manyanga na Bether Mpata kwenye bunge hilo.
CHANZO:HABARILEO
Comments
Post a Comment