MHADHIRI WA CBE AFUKUZWA KAZI KWA KUJIHUSISHA NA NGONO NA WANAFUNZI

 
Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), tawi la Dar esSalaam, kimemfukuza kazi mhadhiri wa chuo hicho anayedaiwa kuhusika na vitendo vya ukiukaji wa maadili ikiwamo kufanya ngono. Mhadhiri huyo ambaye jina halikutajwa alinaswa nakamera za kisasa za kurekodi matukio za CCTV zilizofungwa kwenye vyumba vya madarasa ili kudhibiti nidhamu, miongoni mwa wanafunzi na wahadhiri.Kamera hizo zimefungwa kwenye vyumba vya madarasa 20 ili kudhibiti vitendo vya ngono baina ya walimu na wanafunzi, wizi wa mitihani na matendo mengine yanayovunja sheria.



Hayo yalibainishwa jana jijini na mkuu wa chuo hicho, Profesa Emanuel Mjema (pichani), alipokuwa akizungumza na wanahabari wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Janeth Mbene.

Profesa Mjema, alisema, walifikia maamuzi ya kuweka kamera hizo za kisasa ndani ya madarasa Aprili mwaka jana baada ya kujiridhisha na taarifa za kuwapo matukio ya ukosefu wa maadili miongoni mwa wahadhiri ikiwa ni pamoja na kutoa alama za juu kwa baadhi ya wanafunzi wa kike baada ya vitendo vya ngono. 
“Nilipoingia chuoni hapa Januari mwaka jana, nilisikia kuwa kuna baadhi ya wahadhiri wamekosa maadili, wanatoa alama za juu kwa wanafunzi wa kike kwa masharti hata kama hawajafaulu kwa kiwango hicho. Nikaona vyema tuweke vifaa hivyo ili kudhibiti vitendo hivyo,” alifafanua Profesa Mjema.
Alieleza kuwa baada ya kuweka kamera hizo 20 kwa kila darasa kuwa na kamera moja, walifanikiwa kumnasa mwalimu mmoja kwa kitendo cha kukiuka maadili yake ya kazi na kumfukuza kazi.
Alisema kuwa, kamera hizo pia, zinasaidia kuwadhibiti wanafunzi wenye tabia ya kuiba mitihani, kwani mikakati iliyopo hata wakufunzi na wanafunzi hawajui anayetunga mitihani ili mradi ipo ndani ya silabasi ya chuo. 
Kamera hizo zinadaiwa kuwa na uwezo wa kumvuta karibu mwanafunzi aliyeko darasani na kujua anachokiandika, pia mhadhiri iwapo anachokifundisha ni cha ukweli au anadanganya kwa hiyo zinatumiwa wakati wote kwenye vipindi na mitihani.
Alisema, chuo kimeajiri walinzi kwa ajili ya kuwadhibiti wanafunzi ambao wanavaa nguo ambazo hazina maadili mazuri na pia hukagua vitambulisho wanapofika getini, lengo likiwa ni kukifanya chuo hicho kubakia katika heshima yake.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Mbene, alipongeza jitihada hizo zilizofanywa na chuo hicho, huku akikemea vikali tabia inayofanywa na baadhi ya wahadhiri hao, akiongeza kuwa, ni lazima mwanafunzi apewe madaraja ya matokeo ya mitihani kutokana na ufaulu na uwezo wake. 
Pia, aliahidi kushughulikia suala la uvamizi wa eneo la chuo hicho pamoja na maombi ya kuongezewa madarasa ikiwa ni pamoja na kupewa majengo ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula cha Taifa (NFRA).

CHANZO: NIPASHE

Comments

Popular posts from this blog