MASHOGA SASA WAWEKWA KITANZINI, OBAMA AWATETEA...
Baadhi ya mashoga wakisherehekea siku yao. |
Hatimaye Rais Yoweri Museveni amesaini Muswada wa Sheria inayoharamisha na kutoa adhabu kali kwa wanaojihusisha na vitendo vya ushoga nchini na wanaowaficha.
Msemaji wa Serikali, amesema Rais alitaka kutetea “uhuru wa Uganda dhidi ya shinikizo la mataifa ya Magharibi.”
Rais Barack Obama wa Marekani alishahadharisha dhidi ya Muswada huo, akisema kuwasilishwa kwake kunaashiria Taifa la Uganda linapiga hatua moja nyuma.
Rais Museveni awali alikubali kuweka pembeni Muswada huo, akisubiri ushauri wa kisayansi kutoka Marekani. Vitendo vya ushoga nchini hapa tayari ni haramu.
Desemba mwaka jana, mwanaharakati mtetezi wa haki za mashoga, alielezea hofu yake juu ya sheria hiyo.
Sheria hiyo mpya inatoa adhabu kwa wakosaji wa kwanza kufungwa miaka 14 jela na inaruhusu adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa vitendo vya “ushoga uliopindukia.”
Pia kwa mujibu wa sheria hiyo, ni kosa la jinai kwa mtu ambaye hatafichua mashoga, halikadhalika ni kosa la jinai “kutangaza” na hata “kutambua tu” uhusiano wa kishoga “kupitia au kwa msaada wa chombo chochote cha serikali nchini au asasi yoyote isiyo ya serikali ndani na nje ya nchi.”
Wasagaji nao kwa mara ya kwanza wameguswa na sheria hii. Lakini wanaharakati wanaotetea haki za mashoga, wamesema watapinga sheria hiyo mpya mahakamani.
Awali Muswada huo ulikuwa unapendekeza adhabu ya kifo kwa vitendo vya ushoga, lakini baadaye ilibadilishwa kutokana na kelele za kimataifa.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la AP, maofisa wa Serikali walipiga makofi baada ya Rais Museveni kusaini Muswada huo mbele ya waandishi wa habari katika Ikulu jijini hapa jana.
BBC inaripoti kwamba ni mara chache sana kwa Rais kusaini miswada hadharani. Lakini Muswada huu ulikumbwa na utata mkubwa, hivyo kusababisha wanahabari kuitwa kushuhudia ukisainiwa.
Mapema, Msemaji wa Serikali, Ofwono Opondo aliiambia Reuters, kwamba Rais Museveni alitaka "kuthibitisha uhuru wa Uganda licha ya uchokozi na shinikizo la Magharibi.”
Mtetezi na muasisi wa Muswada huo, Mbunge David Bahati, alisisitiza kuwa ushoga ni “tabia ya kujifunza na inaweza kukomeshwa pia.
“Ushoga ni tabia mbaya, ambayo haipaswi kuruhusiwa katika jamii yetu,” aliiambia BBC. Lakini mwanaharakati wa haki za ushoga nchini alisema “ametishwa,” sana na sheria hiyo mpya.
“Sikwenda hata kazini leo (jana). Nimejifungia ndani. Na sijui ni nini kitatokea sasa. Nazungumza na wanaharakati wangu wote kwa simu. Nako ni hivi hivi, wamejifungia majumbani mwao. Hawawezi kutoka nje. Wamekaa wanaangalia kinachoendelea.”
Kusainiwa kwa Muswada huo kunaonesha mgeuko wa ghafla kutoka ahadi ya hivi karibuni ya kuuweka kando ukisubiriwa ushauri kutoka Marekani.
Katika kauli yake, Museveni alisema: “Naisihi Serikali ya Marekani kutusaidia kwa kushirikiana na wanasayansi wetu, kutafiti ili kujua kama, hakika, kuna watu wanazaliwa wakiwa mashoga. Hilo litakapothibitishwa, tunaweza kupitia upya sheria hii.”
Comments
Post a Comment