WIVU WA MAPENZI ULIVYOUA WENGI 2013
Christina Alfred akiwa amejipumzisha nyumbani kwao Ilala baada ya kutoka hospitali kutibiwa jeraha la risasi. Picha ya Maktaba
Tumefunga mwaka 2013, milio mingi ya risasi ilisikika, watu walipigwa mapanga, wengine kunywa sumu kutokana na kukithiri kwa matukio mbalimbali yanayoambatana na visa na visasi vya wivu wa mapenzi yaliyojeruhi hata kupoteza maisha ya watu.
Matukio ya wivu wa mapenzi yalikithiri miongoni mwa jamii katika mwaka uliopita, hali iliyojenga hofu na kuondoa furaha ya kuingia kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Wachambuzi wa masuala ya uhusiano wanasema kuwa hatua hiyo inatokana na idadi kubwa ya wapenzi kukosa uaminifu, kutokana na tamaa ya fedha, udhaifu wa kingono, tendo la ndoa, kasumba, tamaa za kimwili na mambo kama hayo. Baadhi ya takwimu za matukio hayo zinaonyesha kuwa kwa Mkoa wa Tanga pekee kuanzia Januari hadi Agosti mwaka jana, watu 16 waliuawa katika matukio 377 ya wivu wa mapenzi, baada ya kukamatwa ugoni.
Mbali na takwimu hizo, ipo baadhi ya mifano iliyojitokeza katika kipindi cha kuanzia Januari mpaka Novemba 2013 hapa nchini.
Baadhi ya matukio yaliyojitokeza mwaka 2013
Novemba 13, mwaka huu, Mzee Juma Kondo (80), Mkazi wa Mkuranga mkoani Pwani alijiua kwa kunywa dawa ya macho kutokana na wivu wa kimapenzi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana katika eneo la tukio. Mzee Juma alikuwa akimtuhumu mkewe Asha Ali (50), kutembea na mtoto wao wa mwisho aliyekuwa na umri wa miaka 12, madai yaliyoelezwa kuwa ni ya muda mrefu.
Mke wa marehemu(Asha), alikiri mumewe kujiua kutokana na wivu huo wa mapenzi.SOMA ZAIDI
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mkuranga B, Abdallah Ali Kingwele alikiri kuwasuluhisha mara kwa mara, mbali ya mzee huyo kutaka mkewe aape mbele yake.
Hata hivyo, mkewe alikataa, hatua iliyosababisha kimya kirefu hadi alipofikia hatua ya kujiua. Risasi za Ilala,Dar
Siku saba baadaye, mfanyabiashara wa magari, Gabriel Munisi (35), alijiua kwa kujipiga risasi, baada ya kuwaua watu wawili akiwamo Rubani Francis Shumila aliyehisi alikuwa akitembea na mchumba wake Christina Alfred.
Munisi pia alimuua mdogo wa mchumba wake aitwaye Alpha (22), huku Mama yake Christina, Helen Alfred akiponea chupuchupu kwa kujeruhiwa katika Mtaa wa Ilala Bungoni. Hata hivyo, ilibainika kuwa mtu aliyedaiwa kuwa na mchumba wake alikuwa ni shemeji yake tu.
Mwandishi wa habari ITV
Oktoba 13, mwaka 2013, Mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro amejeruhiwa tumboni baada ya kupigwa risasi mbili alfajiri ya siku hiyo eneo la Kibamba, Dar es Salaam.
Tukio hilo lilithibitishwa na Jeshi la Polisi kwamba lilifanywa na mzazi mwenzake Anthery Mushi ambaye pia alidaiwa kumuua mama yake Ufoo, Anastazia Saro kabla ya yeye kujiua.
Katika tukio hilo, Ufoo alipelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), ambako alifanyiwa upasuaji.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova alithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililosababisha vifo hivyo na kumjeruhi mwandishi huyo.
Achoma nyumba
Wiki mbili baada ya tukio la mwandishi huyo, watu wawili waliuawa katika matukio mawili tofauti yaliyotokea wilayani Chunya mkoani Mbeya kwa madai ya wivu wa mapenzi.
Katika tukio hilo, Adelina Philimon (45), mkazi wa Kijiji cha Magamba wilayani humo na Wasiwasi Mwashiombo(28), mkazi wa Kijiji cha Ipoloto wilayani Mbozi, waliuawa na Zacharia Mwingila (39), aliyetajwa kuwa ni mpenzi wa Adelina. Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, mtuhumiwa alianza kwa kuwachoma na visu wagoni wake, ndipo alipoamua kuchoma moto nyumba hiyo ambayo iliwateketeza hadi kufa.
Agonga sita kwa gari
Tukio lingine la kusikitisha lilitokea Julai 5, mwaka 2013, ambapo watu sita walijeruhiwa ikiwemo kuvunjika baadhi ya viungo vya mwili, baada mfanyabiashara mmoja kuwagonga kwa gari katika eneo la Bahari Beach jijini Dar es Salaam.
Chanzo cha mauaji hayo kilielezwa kuwa ni hasira za wivu wa mapenzi zilizotokana na mfanyabiashara huyo ambaye pia ni dereva kusalitiwa na mpenzi wake.
Ajilipua kwa petroli
Siku tatu baada ya tukio hilo, Taliki Juma (22), aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Ufundi (VETA), mkoani Dodoma, alifariki dunia baada ya kujilipua kwa mafuta ya petroli, huku wengine wanane waliokuwa karibu na eneo la tukio wakijeruhiwa.
Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi mkoani ulionyesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi kwa mpenzi wake aliyejulikana kwa jina la Irene, baada ya kudaiwa kumsaliti.
Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, zilieleza kuwa tukio hilo lilitokea katika Kitongoji cha Machaka, Kata ya Nzughuni.
Auawa kwa upanga
Katika tukio lingine, Agosti 10, mwaka jana, dereva wa Bodaboda, mkazi wa Kijiji cha Igalako wilayani Mbarali mkoani Mbeya, Yohana Mkinga (17), ameuawa kwa kupigwa mapanga, kisha mwili wake kutekelezwa kwenye shamba la mpunga kwa madai ya wivu wa mapenzi.
Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya, Diwani Athumani aliyesema kuwa mwili wa Mkinga ulikutwa na majeraha ya mapanga, huku jicho na vidole vya kushoto vikiwa vimenyofolewa.
Kamanda Diwani alieleza kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa Mkinga aliuawa kwa wivu wa mapenzi, baada ya kuthibitishwa kutembea na mke wa Nicolaus Damson, ambaye alitoroka baada ya tukio hilo.
Kwa nini matumizi ya silaha?
Moja kati ya chanzo kikubwa cha mauaji ya risasi miongoni mwa wapenzi, ni ushawishi wa silaha nyingi kupatikana mtaani.
Baadhi ya matukio yaliyowahi kuripotiwa ni pamoja na baadhi ya watumiaji silaha katika sekta ya ulinzi na usalama nchini wakiwamo askari huzikodisha silaha zao kwa ajili ya kutumika katika matukio ya uhalifu.
Aidha, kuwepo kwa mianya ya uingizaji wa silaha nchini kwa njia haramu kutokana na udhaifu uliopo katika mipaka mipaka ya DR Kongo, Burundi, Rwanda na hata Zambia jambo ambalo ni hatari.
Mbali na mazingira hayo, Septemba 16, mwaka 2013, Kikosi cha Kuzuia Ujangili cha jijini Dar es Salaam (KDU), kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro, waligundua kiwanda cha kutengeneza bunduki na kuzikarabati kinyume cha sheria.
Kiwanda hicho kiligunduliwa katika Mtaa wa Kingo, Manispaa ya Morogoro, kutokana na msako uliofanywa na kikosi hicho.
Sababu za kukithiri
Akizungumza na mwandishi wa gazeti hili juu ya sababu za kukithiri mauaji hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya alisema kuwa chanzo kikuu ni pamoja na jamii kutoshughulika na magonjwa ya akili.
Alisema kuwa idadi kubwa ya watu hasa walioko kwenye uhusiano wa mapenzi, wamekuwa wakikosa msaada wa ushauri nasaha.
“Mtu anapoingia kwenye msongo wa mawazo, hajui aende sehemu ipi itakayomsaidia. Mbali na sababu hiyo, tatizo la mfumo dume bado linaendelea na wanaume wengi bado hawawezi kuachwa bali wao ndiyo wana mamlaka ya kuacha tu,” alisema Usu.
Katika kutafuta suluhu ya changamoto hiyo, Usu alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali nchini wanatakiwa kuongeza juhudi katika kupambana na tatizo hilo ikiwamo kuongeza madawati ya ushauri nasaha kote nchini.
“Lakini hata sisi makundi ya wanaharakati kwa pamoja tuhakikishe tunaongeza kasi ya kuelimisha na kuhamasisha jamii, ili ipate ufahamu juu ya matatizo ya akili na namna ya kuachana nayo,” alisema.
Alisema endapo huduma ya kutibu msongo wa mawazo ingepewa nafasi kama ilivyo kwa wanasiasa jukwaani, mauaji hayo yasingeweza kukithiri kwa kiwango hicho.
Katika hatua nyingine, Usu aliitaka Serikali kuhakikisha inadhibiti matumizi ya silaha hasai kwa vijana. “Siraha zimesambaa mtaani, vijana wanatembea nazo, Jeshi la Polisi washughulikie hilo pia,” alisema.
Hatima ya mauaji hayo
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova amesema kuwa kwa sasa jeshi hilo limeanzisha Dawati la Ushauri Nasaha kwa jinsia zote, ili kukabiliana na magonjwa ya akili katika jamii.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya kukithiri kwa mauaji yatokanayo na wivu wa mapenzi miongoni mwa watu wenye uhusiano.
Kamishna Kova alisema kuwa dawati hilo limeanza mwezi Desemba mwaka jana katika mikoa sita kote nchini kwa lengo la kuhakikisha jamii inapata huduma ya ushauri nasaha.
“Mikoa hiyo ni Kilimanjaro, Mbeya, Dodoma, Dar es Salaam, Musoma na Tanga. Kuna askari wetu ambao ni maalumu kwa ajili ya ushauri katika vituo hivyo,” alisema.
Mbali na hatua hiyo Kamishna Kova alisema kuwa kwa sasa jeshi hilo liko kwenye maandalizi ya kuongeza makali katika sheria ya umiliki wa silaha.
Aidha, Kamishna Kova aliongeza kuwa wakati maandalizi hayo yakifanyika, zoezi linaloendelea kufanyika kwa sasa ni kuhakikisha wanatoa adhabu kali kwa mtu yeyote atakayebainika na hatia ya kuonyesha silaha ovyo mtaani.
MWANANCHI
MWANANCHI
ShareThis Copy and Paste
Comments
Post a Comment