Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,Bernard Membe ahutubia Mkutano kuhusu Amani DRC na Nchi za Maziwa Makuu
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe
(Mb.) akiwa katika moja ya Mikutano ya Umoja wa Afrika inayoendelea
mjini Addis Ababa, Ethiopia. Mhe. Membe alihutubiaMkutano
wa Tatu wa Ngazi ya Juu kuhusu Utaratibu wa Usimamizi wa masuala ya
Amani, Usalama na Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC) na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu uliofanyika mjini Addis Ababa,
Ethiopia tarehe 31 Januari, 2014 pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi
na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea mjini hapa.
Naibu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliason akizungumza wakati wa
Mkutano kuhusu DRC na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika
Addis Ababa.
Mjumbe wa Sudan akisaini Mkataba wa Kujiunga na Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano ulio chini ya ICGLR
Wajumbe wengine kutoka nchi wanachama wa ICGLR wakifuatilia mkutano.
Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bibi Mary Robinson naye pia alikuwepo katika mkutano huo.
Baadhi
ya Wajumbe kutoka Tanzania wakiwa kwenye Mkutano kuhusu Nchi za Ukanda
wa Maziwa Makuu (ICGLR) mjini Addis Ababa. Mwenye tai nyekundu ni Bw.
Robert Kahendaguza, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kikanda
na Balozi David Kapya.Picha Kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa
---
Na Mwandishi Wetu, Addis Ababa
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe
(Mb.) ametoa rai kwa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) kuweka nia
mpya ili kutimiza lengo la kupatikana kwa amani ya kudumu katika Nchi za
Ukanda huo.
Mhe.
Membe aliyasema hayo wakati akihutubia Mkutano wa Tatu wa Ngazi ya Juu
kuhusu Utaratibu wa Usimamizi wa masuala ya Amani, Usalama na
Ushirikiano katika Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Nchi za Kanda ya Maziwa Makuu
uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu
wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) unaoendelea mjini hapa.
Waziri
Membe alisema kuwa kumekuwa na hatua nzuri zilizofikiwa katika kutafuta
amani ya kudumu DRC na katika Kanda kwa ujumla. Hatua hizo ni pamoja na
kusambaratishwa kwa kikundi cha Waasi cha M23 huko Mashariki mwa DRC.
Hata hivyo alisema bado kunahitajika jitihada na nia madhubuti ili
kuhakikisha migogoro isiyoisha inamalizwa kabisa.
“Tunayashukuru
Majeshi ya Ulinzi ya DRC kwa msaada wa Vikosi vya Kulinda Amani vya
Umoja wa Mataifa (MUNOSCO) na kile cha FIB ambapo tumeshuhudia
kusambaratishwa kwa Kikundi cha M23, tunapongeza pia jitihada za Rais wa
Uganda, Mhe. Yoweri Museveni ambaye pia ni msuluhishi wa mgogoro huo
kufuatia kusainiwa kwa Azimio la Amani kati ya Serikali ya DRC na M23
hapo tarehe 12 Desemba, 2013”, alisema Mhe. Membe.
Mhe. Membe aliongeza kuwa umefika wakati sasa kwa watu na nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu kusema inatosha kwa migogoro isiyoisha ili kuwawezesha kuwekeza nguvu na vipaji vyao katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Aidha,
kwa namna ya pekee, Waziri Membe alimpongeza Mjumbe Maalum wa Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, Mhe.
Bibi Mary Robinson na Kamati yake ya Ufundi (TSC) kwa kazi nzuri
waliyoifanya mwaka 2013. Kamati hiyo ya Ufundi imefanikiwa kutoa Mpango
Kazi kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa
Kanda.
“Nimeridhishwa na kazi inayofanywa na Kamati hiyo ya Ufundi kwa kutoa Mpango Kazi ambao unajitosheleza kwa ajili ya kuutekeleza Mpango
wa Amani. Hivyo, tumekutana hapa kuridhia mpango huo ili kila mmoja
wetu aweke nia mpya ya kutekeleza yale yote tuliyowahi kukubaliana chini
ya Mpango wa Amani” alisisitiza Waziri Membe.
Aidha,
wakati wa Mkutano huo nchi za Kenya na Sudan zilisaini rasmi Mkataba wa
kujiunga na Mpango wa Amani, Usalama na Ushirikiano wa Kanda ya Maziwa
Makuu ( Peace, Security and Cooperation Framework).
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan Eliasson.
-Mwisho-
Comments
Post a Comment