WARIOBA:SERIKALI TATU SI MZIGO

MWENYEKITI wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini,

Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, ametetea muundo
wa serikali tatu kuwa hauna gharama, tofauti na
inavyotafsiriwa na wengi. Mbali na kutetea gharama za uendeshaji wa serikali
tatu, Jaji Warioba pia amewashukia wanaodhani
mapendekezo ya muundo wa serikali tatu ni yake
binafsi, kutokana na msimamo wa siku nyingi wa
kiongozi huyo. Akizungumza na Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Jaji
Warioba alisema muundo wa serikali tatu umepunguza
gharama za uendeshaji. Kwa mujibu wa Jaji Warioba, chini ya muundo huo
hata Bunge linatarajiwa kuwa na wabunge 75 tu,
hatua ambayo itapunguza gharama. Mwenyekiti huyo alisema kuwa gharama za uendeshaji
wa Serikali ya Muungano zitakuwa katika Wizara ya
Ulinzi na Usalama pamoja na Mambo ya Nje huku
katika maeneo yaliyobaki gharama zake zitakuwa
zimepungua zaidi. “Hivi kwa nini hili la muundo wa muungano tunajadili
gharama wakati kila mwaka tunapoongeza mikoa,
wilaya, tarafa, majimbo na vijiji gharama
zinaongezeka wala hakuna anayezungumzia wala
kuhoji? Hivyo hivyo kwa kuwa na serikali tatu, hakuna
gharama, tena kimsingi tumepunguza gharama za migogoro ya mara kwa mara ya kushughulikia kero za
Muungano,” alisema Jaji Warioba. Mwenyekiti huyo wa tume ambaye alitumia muda
mwingi kufafanua mambo mbalimbali, alisema suala
la mgawanyo wa mikoa ikiwemo wanaopendekeza Jiji
la Mbeya ligawanywe pamoja na Songea, kuna
gharama kubwa za uendeshaji. “Hivi mnajua namna gani viongozi wa serikali ya
Mapinduzi Zanzibar na Tanzania Bara wamekutana
kujadili matatizo ya Muungano? Gharama
wanazotumia mnazifahamu?” alihoji. Alisema kuwa hata kuwepo kwa serikali mbili bado
hakutapunguza gharama, hivyo ni muhimu
kukubaliana na mawazo ya wananchi juu ya muundo
wa serikali tatu ambazo zimepunguza gharama. Mwenyekiti huyo alisema Serikali ya Muungano
itakuwa na chanzo chake cha mapato ambayo
hayatokani na kodi. Alisema kuwa gharama itakayoendesha Serikali ya
Muungano ni ile inayohusu mambo ya utawala ambayo
ni ndogo. Akizungumzia baadhi ya makada na viongozi wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaomlaani kwa
kuingiza hoja ya muundo wa muungano kwenye
rasimu, Warioba alisema rasimu hiyo si yake bali ni
maoni ya Watanzania. Alisema wananchi wameona sababu za kuwepo
serikali tatu na tume imechambua na kuona kuwa
kuna hoja za msingi za kuwapo muundo wa serikali
tatu. “Wanaotafsiri rasimu hii ni lazima waelewe kuwa
wanatafsiri maoni ya wananchi, si ya Warioba,
hatutaki sisi kuhusishwa na vyama maana tumefanya
kazi kama walivyosema Watanzania ambao wanataka
serikali tatu,” alisema. Alisema kuwa anashangazwa na maoni yanayotolewa
na baadhi ya wachache kuwa tume imemgeuka hayati
Mwalimu Julius Nyerere. “Sijui hawa wanafikiri Mwalimu angekuwa na mawazo
mgando wakati wote,” alisema huku akitolea mfano
Nyerere alivyokubaliana na ripoti ya Jaji Nyalali ya
kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi huku wengi
wakikataa. Alisema kuwa masuala ya Muungano yameanza
kufanyiwa mabadiliko wakati Nyerere akiwa hai,
akitolea mfano mwaka 1977 makusanyo ya kodi ya
Zanzibar yalivyopendekezwa kubaki huko. Warioba alisema kuwa mwaka 1984 ilipitishwa sheria
na Zanzibar kuwa kodi yoyote itakayopitishwa na
Bunge au sheria yoyote ni lazima ijadiliwe na Baraza la
Wawakilishi. Katiba ya Tanganyika Warioba alisema kwa kutumia sheria za Local
Government na kupitia Hansard, Katiba ya Tanganyika
itaweza kupatikana ndani ya kipindi kifupi kisichozidi
miezi mitatu. Alisema hakuna haja ya kutumia fedha nyingi kupata
mawazo mapya ya kuanzishwa kwa Katiba hiyo. Mwenyekiti huyo alisema ili kuhakikisha Katiba mpya
inatumika katika Uchaguzi Mkuu ujao ni lazima kuna
muundo wa vitu vitakavyobadilika ikiwemo Tume ya
Uchaguzi. “Ukishakubali Katiba hii lazima uunde Tume Huru ya
Uchaguzi na katika hilo naona hakuna tatizo na
nilishasema kutunga Katiba ya Tanganyika si kazi
ngumu,” alisema. Alisema kuwa ukisoma rasimu ya pili ukurasa wa
kwanza hadi wa tano ni maoni yanayotokana na
mawazo ya Watanzania, hivyo hakuna jambo ambalo
linaweza kubadilika katika maoni ya maadili, malengo,
haki za binadamu na mamlaka ya wananchi. Kuwania uongozi Jaji Warioba alisema kutokana na maoni ya wananchi,
viongozi waliostaafu hawatakuwa na haki ya kuwania
uongozi wowote wa kisiasa hadi ipite miaka mitatu
tangu kustaafu kwao. Aliwataja wanaoangukia katika sheria hiyo kuwa ni Jaji
Mkuu, Jaji wa Mahakama ya Juu, Mwenyekiti wa Tume
ya Maadili na wajumbe, Mkurugenzi wa Uchaguzi,
Msajili wa Vyama vya Siasa, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali (CAG), Spika na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali. “Usipofanya hivyo hao hawatakuwa ‘active’ ni lazima
wakisha staafu ipite miaka mitatu ndiyo waruhusiwe
kuwania nafasi za uongozi,” alisema. Alisema kuwa wananchi wamefikia uamuzi huo baada
ya wastaafu walio wengi kukimbilia siasa baada ya
kustaafu. Mikopo kwa viongozi Alisema kuwa Katiba inazuia matumizi mabaya ya
vyeo hivyo kiongozi wa umma hapaswi kutumia
madaraka yake na kukopa mikopo katika taasisi za
kifedha. “Katiba inazuia matumizi mabaya ya vyeo, katika
rasimu tumeweka ile miiko lakini sheria itakuja na
kutaja ni viongozi wapi wanahusika katika hilo,”
alisema. Warioba alisema kuwa wamezuia viongozi kutumia
madaraka yao kupata mikopo bali anaweza kukopa
kwa utaratibu wa kawaida. Uraia Jaji Warioba alisema kuwa rasimu ya kwanza
haikuzungumza juu ya uraia bali kwa sasa
imezungumzwa na kuwekwa kwa aina yake. Alisema kuwa kwa sasa Mtanzania anaweza kupata
uraia wa nchi mbili (kinasaba) bila kupoteza haki zake.
“Sawa hawezi kuwania urais lakini kuna haki za msingi
anazopaswa asipoteze,” alisema. Ukomo wa Tume Alisema kuwa tume itakamilisha kazi yake
itakapowasilisha rasimu hiyo katika Bunge la Katiba
kutokana na muongozo wa sheria unavyoainisha. Mwenyekiti huyo alisema kuwa sheria iliweka wazi
watu gani wanaostahili kuingia katika Bunge hilo,
hivyo tume hiyo itabaki kuwa mshauri. “Sisi kazi yetu itabaki kuwa washauri na si kuwa
wabunge, tunafuata kama sheria inavyosema, hivyo
wakitaka ushauri tutawapa lakini kazi kubwa
tumekamilisha,” alisema.

Comments

Popular posts from this blog