WAJAWAZITO 1,500 WAKUTWA NA VVU
JUMLA ya
wanawake wajawazito 1,576 kati ya 42,712 waliopima Virusi Vya Ukimwi
(VVU) mwaka jana katika vituo mbalimbali vinavyotoa huduma za afya
mkoani Pwani walipatikana na maambukizi ya ugonjwa huo.
Takwimu
hizo zilitolewa mjini Kibaha juzi na Mratibu wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi
Tanzania (Tacaids) Mkoa wa Pwani, Hafidh Ameir, wakati wa ziara ya
Kamati ya Bunge ya masuala ya ukimwi na dawa za kulevya ilipotembelea
mkoani hapa.
Ameir alisema
pamoja na takwimu hizo, lakini kwa sasa maambukizi ya VVU mkoa huo
yamepungua kutoka asilimia 6.7 mwaka 2008 hadi kufikia asilimia 5.9 kwa
mwaka 2012 kutokana na jitihada mbalimbali.
Alisema
kwa sasa mkoa una vituo vya tiba 263 na kati ya hivyo vituo 214 sawa na
asilimia 81 vinatoa huduma ya upimaji wa hiari na ushawishi wa VVU na
vituo 52 vinatoa huduma ya dawa za kufubaza makali ya VVU kwa watu
wanaoishi na VVU ambavyo ni asilimia 24 ya vituo 214.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Lediana Mng'ong'o, alitoa wito kwa halmashauri
kushirikisha kikamilifu wadau ikiwa ni pamoja na kuweka wazi taarifa zao
za vikao.
Mng'ong'o
ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu, alisikitishwa na kitendo cha
kutokuwepo kwa viongozi wa kisiasa kwenye kikao cha kamati hiyo na
wataalamu wa halmashauri, hivyo kutoa wito wa kushirikishwa kwa viongozi
hao ili wajue taarifa muhimu za wananchi wao.
Kamati hiyo ya Bunge iko kwenye ziara ya siku mbili mkoani Pwani katika Wilaya ya Kibaha Vijijini na Bagamoyo.
CHANZO:TANZANIA DAIMA
Comments
Post a Comment