UJUMBE MAALUM KUTOKA KWA SHIGONGO


Mkurugenzi wa Global Publishers, Eric Shigongo.
Hiki ndicho ninachokifahamu mimi ndugu yenu.
Maisha ni vita, maisha ni mapambano na mtindo pekee wa kukusogeza mbele ni kupigana! Hata uwe mwema kiasi gani utakuwa na maadui, Yesu alikuwa nao, Mtume Muhammad alikuwa nao, Mandela alikuwa nao na hata Mahatma Gandhi alikuwa nao.
Hata ufanyeje maadui watakuwepo tu, utapingwa, utapuuzwa, hivyo basi kamwe usijaribu kuwafurahisha watu, eti unafanya vitu ili watu wakupende, utapoteza muda wako bure.
Kumbuka kuwafurahisha watu ndio barabara kuelekea kwenye umasikini, siku zote fanya kitu ambacho moyo wako unaridhishwa nacho. Watu watakucheka, watakutukana matusi yote lakini mwisho wa siku kama ukiendelea mbele hao ndio watakuja kukupa mkono wa hongera pale utakapoibuka mshindi.
USHUHUDA WANGU; Kwa miaka yote kumi na tano ambayo nimeishi na kufanya kazi Dar es Salaam, nimetukanwa sana, nimeitwa majina yote mabaya, nimehukumiwa sana. Badala ya kuwachukia walionitukana na wanaonitukana (hivi sasa wakisoma ) ambacho mimi hufanya ni kuziba masikio na kuyachukua matusi yao kama hamasa kisha kusonga mbele.
Najua wapo watakaolia pindi nitakapokufa, lakini pia wapo watakaofurahi na kufanya sherehe kwamba nimekufa, cha muhimu kwangu ni urithi nitakaouacha hapa duniani baada ya mimi kuondoka, si urithi wa mali bali idadi ya watu ambao Mungu atasikia sauti zao wakisema “Mtu yule alikuwa mwenye dhambi lakini alisaidia kutupa tumaini na maisha yetu yakabadilika.” Hao wakiwa wengi itanitosha, yawezekana sauti zao zitamfanya Mungu aniangalie kwa jicho la huruma na kusema “KARIBU MWANANGU.”
Nawatakia mwaka mpya wenye mafanikio, kumbukeni katika nchi hii ukifanya kazi kwa nguvu na ukiwa na malengo nafasi ya kufanikiwa ipo bila kujali historia ya maisha yako. NAMUOMBA MUNGU MWAKA HUU UWE WA MPENYO KWA KILA MMOJA WETU.
Asanteni Mungu awabariki
Eric Shigongo James
Mkurungenzi Global Publishers Ltd





ShareThis Copy and Paste

Comments

Popular posts from this blog