TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
:
Kwa kipindi kirefu sasa vijana ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tumeshuhudia na kusikia kauli na vitendo vya baadhi ya wanachama wa CCM vinavyoashilia ukiukwaji wa makusudi wa maadili, miiko na kanuni za Chama.
Kwa kipindi kirefu sasa vijana ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) tumeshuhudia na kusikia kauli na vitendo vya baadhi ya wanachama wa CCM vinavyoashilia ukiukwaji wa makusudi wa maadili, miiko na kanuni za Chama.
CCM katika uhai wake wa miaka 37 baada ya kuunganisha TANU na ASP, imeendelea kukua na kushamiri kutokana na misingi imara ya kikatiba tuliyojiwekea tangu mwaka 1977, ambayo wana CCM wote kwa utashi na hiari tumeienzi na kuifuata.
Asiyetaka, ni ruksa kuondoka na kutuachia chama chetu.
Ni kwa njia hii tumeweza kuimarisha mshikamano ndani ya Chama Cha Mapinduzi na kutuwezesha kushinda katika chaguzi mbali mbali, hivyo kuendelea kutoa uongozi katika ngazi zote za utawala nchini.
Hivyo basi, kitendo chochote kile chenye mwelekeo wa kubomoa mshikamano ndani ya Chama, ni kitendo cha kutudhoofisha, hivyo kutuengua katika uongozi wa nchi. HILI KWA VIJANA WA CCM, HALIKUBALIKI!
Tunasema hivyo kwa sababu kuanzia mwaka huu tunaingia kwenye mchakato wa chaguzi mbali mbali zitakazohitimishwa mwakani na uchaguzi mkuu, mchakato unaohitaji mshikamano wa hali ya juu ndani ya chama. Bila ya tunu hiyo, chama kitatetereka na hatma yake ni vurugu, mipasuko na utekelezaji mbovu wa ilani ya chama ambayo ni silaha yetu kuu ya kukonga nyoyo za Watanzania.
CCM iliyotulea sisi vijana inatutaka kipindi kama hiki kuhakikisha kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM inatekelezwa kikamilifu, hivyo penye mapungufu parekebishwe na penye mafanikio pashangiliwe.
Na bahati yetu nzuri ni kuwa Serikali ya Rais Kikwete imefanya mengi mazuri yenye kumgusa kila Mtanzania mwenye nia njema na nchi yake.
Lakini tunachokiona sasa ni kitu tofauti kabisa na malezi na makuzi yetu ndani ya Chama kwani tayari baadhi ya wana CCM, bila woga wala aibu, wameshajitangaza kuwa wagombea wa Urais, Ubunge, Udiwani na nafasi zingine za kupigiwa kura na wameanza kwa kampeni za kishindo za rushwa na vishawishi mbalimbali nje kabisa ya taratibu, kanuni na maadili ya chama.
Kinachotishia kutoweka kabisa kwa mshikamano ndani ya Chama ni makundi ya mashabiki yanayoundwa na "wagombea" hawa wasio rasmi yanayopita nchi nzima kushawishi (kwa fedha na rushwa zingine) makundi mbalimbali ya kijamii, ya kijasiriamali ili kuungwa mkono.
Ilani ya CCM ya 2010 imewekwa pembeni, kinachonadiwa ni "Ilani" binafsi za kumwaga pesa nchi nzima, kusambaza elimu kama njugu, bila kuelezea vyanzo vya mapato vya serikali zao za kusadikika.
Huu ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za nchi, maadili, miiko na taratibu ndani ya Chama; ni fedheha kubwa kwa Chama na Serikali yake ambayo iko wima kuhakikisha kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2010 inatekelezwa kwa ufanisi mkubwa .
CCM ina taratibu zake za kupata uongozi na wote tunazijua, kufanya kinyume na taratibu hizo ni uasi, upungufu wa busara, na ukosefu wa sifa ya uongozi.
Hivyo vijana wa CCM tunamuunga mkono Mwenyekiti wa CCM Taifa Mh. Dr Jakaya Mrisho Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa CCM Ndugu Philip Mangula, na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama, Ndugu Nape Nnauye na viongozi mbalimbali wa Chama waliokemea tabia hii mpya na hatarishi ndani ya chama chetu ya kuhaha kupata uongozi nje ya taratibu na kutumia vishawishi vyenye sura ya rushwa vinavyokitia doa Chama.
Kwa kuwa dhamira ya miiko, maadili na kanuni za Chama ni kutuunganisha wana CCM wote kuwa kitu kimoja , dalili zozote nje ya tunu hizo ni usaliti, uasi ambao hauna budi kupigwa vita kwa nguvu zetu zote hasa sisi vijana.
Hapa hatutakiwi kumwangalia nyani usoni. Gharama ya kuendelea kuvumilia kauli na vitendo hivi vipya na hatarishi katika historia ya Chama chetu, ni majuto.
Waswahili hunena bandu bandu humaliza gogo, na bandu bandu hii iliyoanza tusiivumilie, itatuweka pabaya.
Wana CCM wote tunaamini kuwa hakuna mtu yeyote aliye juu au mkubwa kuliko chama, hivyo uasi ulioanza kuota mizizi ndani ya chama hauna budi kung'olewa mara moja tena bila ganzi, bila huruma.
Kamati ya Maadili ya CCM ina wajibu wa kutafsiri hasira ya wana CCM na Viongozi wao kwa vitendo. UVCCM inahimiza kuwa wale wote walioanza kampeni za uraisi, ubunge, udiwani na nafasi nyingine zozote kwa vitendo na kauli za kukiuka taratibu, hivyo kukikejeli Chama, kukejeli uongozi wa nchi uliopo na kuleta nyufa katika chama chetu, waonyeshwe mlango wa kutokea.
Tusipoziba ufa huu sasa, tujiandae kujenga ukuta mwakani kwa gharama kubwa ya kupindukia.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Paul Makonda
MKUU WA IDARA YA UHAMASISHAJI NA
CHIPUKIZI TAIFA
Comments
Post a Comment