Serikali yatoa ratiba ya mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dr. William Mgimwa ambaye alifariki juzi akiwa Afrika Kusini



Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Mhe.William Lukuvi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Mazishi ya aliyekuwa waziri wa Fedha Marehemu Dk. William Mgimwa akiongea na waandishi wa Habari jana  jijini Dar es Salaam kuhusu mwili wa marehemu kuwasili tarehe nne saa saba mchana uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere na Shirika la Ndege la Afrika ya Kusini na kuzikwa tarehe sita katika kijiji cha Magunga mkoani Iringa. Kulia ni Naibu waziri wa Fedha Saada Salum Mkuya.
Katibu Mkuu ofisi ya Waziri Mkuu Dk. Florens Turuka (kulia) na Katibu Mkuu wizara ya Afya na Stawi wa Jamii Charles Pallangyo (kushoto) wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Mhe.William Lukuvi (hayupo pichani) Wapigapicha kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakimpiga picha Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Mhe.William Lukuvi (hayupo pichani) 
 ****
Na Kiza Sungura-MAELEZO Dar es Salaam
KAMATI ya Taifa inayohusika na mazishi ya aliyekuwa waziri wa Fedha Dk. William Mgimwa  imetoa ratiba ya mazishi ambapo mwili wa marehemu utawasili siku ya jumamosi tarehe nne saa saba mchana  katika uwanja wa Mwalimu Nyerere  Terminal  II na kupelekwa nyumbani kwake Mikocheni B jijini Dar es salaam.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge) Dk. William Lukuvi alisema kamati itakayohusika na mapokezi ya mwili wa marehemu ni ofisi ya Waziri Mkuu  itakayohusika na ndugu, viongozi na wananchi na Kamati ndogo ya mkoa wa Iringa inayoongozwa na mkuu wa mkoa huyo Dk. Christine Ishengoma. 

Dk. Lukuvi alisema siku hiyo ya jumamosi saa kumi na moja jioni mwili marehemu utapelekwa katika hospitali ya Lugalo na tarehe tano siku ya jumapili saa tano na nusu asubuhi mwili wa marehemu utapelekwa katika  ukumbi wa Karimjee kwa ajili ya ibada na kutoa heshima za mwisho.
 
Alisema ifikapo saa nane mchana mwili wa marehemu Dk. Mgimwa utapelekwa uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere Terminal I kwa ajili ya kuelekea Mkoa wa Iringa.Ifikapo saa kumi kamili alasiri mwili wa marehemu utakuwa umewasili Mkoa wa Iringa katika uwanja wa ndege Nduli  na kuagwa na viongozi na wananchi wa mkoa huo katika ukumbi wa Siasa kilimo na baada ya hapo utapelekwa kijijini kwake Magunga. 

Waziri Lukkuvi alimalizia kwa kusema kuwa shughuli za mazishi ya Marehemu Dk. Mgimwa zitafanyika 6.1.2014 kuanzia majira ya saa sita mchana  katika kijiji cha Magunga mkoani Iringa na atazikwa kwa heshima zote za Kiserikali.

Comments

Popular posts from this blog