NJIA KUMI KUSAIDIA KUPUNGUZA UNENE
- Get link
- X
- Other Apps
Ni makala muhimu sana. Wastani wa maisha ya
Mtanzania ( na Waafrika wengi) hata wale waliosoma au wanaojiweza kiuchumi ni
miaka 40-50. Kati ya sababu kuu zinazopunguza uhai wetu ni afya, unene na
kutojua kujiangalia vyema afya zetu.
1-ULAJI
Ipo
mifumo miwili ya kula. Chakula unachokula na namna unavyokila.
·
Unavyokula.
-Kuna kula vyakula vidogo vidogo
vyenye madini, vitamini, mafuta nk mara nyingi kwa siku; au kula milo michache
(mmoja au miwili) mikubwa ili kujaza tumbo. Ulaji mdogo mdogo husaidia afya na
kuingia mwilini vyema kuliko ulaji mkubwa wa mara chache. Tumbo lina musuli
zinazofanya kazi kama mashine au mnyama. Gari likijaa sana hupata taabu kwenda.
Punda hivyo hivyo. Ulaji mdogo mdogo unaosambazwa mara kadhaa kwa siku ni
bora maana mwili unachambua kila kitu kwa wepesi na haraka. Unapokula
milo michache mikubwa unapalilia zaidi mafuta mwili.
(PENDEKEZO la kwanza. Asubuhi, kunywa
maji kwanza, matunda, kisha ndiyo chai na vitu vingine kama mkate au maandazi)
·
Wapo wanaodai kwamba wanakula matunda na mboga.
Tatizo ni kwamba mipangilio
yao huwa ya makosa. Mathalan wengi hula matunda baada
ya chakula. Vimeng’enya chakula (enzymes) tumboni hufanya
kazi namna tofauti. Mathalan vile vinavyonyambua matunda ni tofauti na
vinavyomeng’enya vitu vigumu zaidi kama nyama au wanga. Matunda hunyambuliwa
haraka zaidi kuliko vyakula vingine. Hivyo ni bora kula matunda dakika10-20
kabla ya chakula. Ukila baadaye matunda hugeuzwa aina fulani ya pombe
(fermented food) inayoelea tu juu ya chakula na kubakia kitu kingine badala ya
kuingizwa haraka ndani ya damu kupitia utumbo mdogo, uwengu, moyo, ini, nk.
·
Tatizo jingine ni kupika sana mboga
hadi zikapoteza nguvu.
-Mseto
wa vyakula pia ni muhimu. Kwa mfano vyakula vyenye uchachu (“acid”) na vile
vinavyomumunyuka haraka (“alkaline”) havitakiwi viliwe pamoja. Mfano ni
matunda. Matunda chachu kama machungwa, mananasi na maembe yatakiwa yawe
pamoja; na yale laini zaidi: ndizi mbivu, matikiti maji, mapapai,
matufaha, nk yaende kivyake, maana yana mfumo tofauti, wa kumeng’enywa.
Hali hiyo pia iko katika nyama. Nyama nyeupe
(ndege na samaki) tofauti na nyama nyekundu (ng’ombe, kondoo, nk) ziliwe
tofauti.
·
Chakula unachokula
Watanzania/Waafrika hatuna
tabia ya kula mboga mboga mbichi. Tunafuata
ladha na mazoea kuliko thamani.
Bara
letu lina mboga na vyakula bora kuliko bara lolote duniani lakini sisi tunakufa
mapema na kwa utapia mlo kuliko wale wanaotoka nchi kame. Ulaya nzima imejazana
mboga mboga zinazoagizwa toka Afrika. Kenya na Tanzania zinauza mboga za
maharagwe mabichi (green beans), matunda toka Afrika Kusini na Ivory Coast; nk.
Waafrika tunapenda kujaza matumbo. Unene umekithiri hata wale walio matajiri
waliosoma bado wanakufa kwa kisukari shauri ya kutokula mboga mbichi.
Ulaji
wa mboga mbichi ni upi?
Ni
mathalani ulaji wa salad. Tanzania tunaita kachumbari. Lakini si lazima iwe
kachumbari ya nyanya, vitunguu na chumvi tu. Waweza kuchanganya matango, nyanya
kwa maparachichi; au vitunguu saumu, giligilani na karote. Huu mseto wa mboga
mbichi ni mzuri ukienda na chakula chenye nyama za minofu na wanga (ugali,
wali, ndizi za kupika nk). Ulaji wa wanga asubuhi, mchana na jioni kila siku
huchangia sana katika unene.
(PENDEKEZO LA 2. Ugali kwa samaki; mboga ya
majani ya matango kwa nyanya. Usiweke chumvi kwenye hiyo mboga mbichi ya
majani.)
2-UNYWAJI MAJI
Waafrika
hatunywi maji, hasa wanawake. Wanaokunywa maji zaidi ni wacheza michezo. Wengi
wetu hunywa zaidi soda (vinywaji baridi kama Cocacola, Pepsi, Mirinda
,Tangawizi na gesi za kisasa kama Red Bull) zilizojaa gesi inayoleta
vidonda tumboni; na chai. Kuliko maji. Na maji haya hutakiwa dakika 10-20
kabla ya chakula au nusu saa kuendelea baada ya chakula. Ukila chakula
huku unasakatia maji huimanisha mtu una kiu. Ulaji chakula na unywaji maji ni
vitu viwili tofauti.
Ila
utawaona watu wanakula huku wakibugia maji. Unapokula chakula huku unabugia
maji unapunguza nguvu za chakula, unajaza tumbo maji na kuchelewesha mmeng’enyo
wa chakula (digestion).
Chakula
kisipomeng’enywa vizuri kinaketi tu tumboni. Matokeo wengi wetu tuna
matumbo makubwa. Kama hufanyi mazoezi lile tumbo linakwenda pembeni (chini ya
mbavu) hasa kwa watu wa makamo linaleta maradhi kama kisukari, kiungulia, kuvimbiwa,
uyabisi wa tumbo, nk. Kizungu huitwa “love handles.”…
3-SUALA LA UMENG’ENYAJI
Chakula
huanza kumeng’enywa au kusagwa (kwa lugha iliyozoeleka) mdomoni. Mate yako
mdomoni ni chanzo cha uchambuaji chakula. Unapobugia chakula bila kutafuna
sawasawa unasababisha mambo mawili. Moja chakula kutochambuliwa vizuri, pili
chakula kwenda kukaa tu tumboni, au kama kikipita hakisaidii lolote mwilini.
Utafunaji
wa taratibu husaidia umeng’enyaji. Chakula kinapofika tumboni hukaa pale dakika
ishirini. Hapo huchanganywa na asidi (ya manjano iitwayo Hydrochloric)
inayokibadilisha tayari kupelekwa utumbo mkubwa, kupitia kongosho. Kule uchafu
utapelekwa chini na rutuba kusafirishwa na utumbo mdogo kuelekea katika uwengu,
moyo. Moyo utadunda chakula kilichoshageuzwa damu kuelekea mwilini kufanya kazi
na akiba hubakishwa katika ini.
Sasa
kama usipotafuna vizuri, ukila huku unakunywa sana maji au vinywaji vingine
chakula hakimeng’enywi vizuri. Ndiyo maana unawaona watu wengine wanakula sana
lakini hawana afya. Wanaugua ovyo ovyo, wanatoka jasho ovyo, wanajamba ovyo,
wana matumbo makubwa, wanavimbiwa, wanakaa siku nyingi bila kwenda choo
(inatakiwa mtu kwenda haja kubwa mara moja au mbili kwa siku) nk.
4-ULAJI WA VYAKULA VYA
MAFUTA
Mafuta
ni suala muhimu sana mwilini. Ila ulaji wake shurti uwe wa mpangilio. Yaani
unaowiana. Lazima mtu uwe na wastani mzuri wa vyakula vya nguvu, yaani “wanga”
(ugali, ndizi, wali, viazi mbalimbali, mikate, mahindi, nk), ujenzi yaani
“protini” (mboga na nyama), “madini” (mbegu mbegu mbichi si za kukaanga sana na
chumvi) na “vitamini” (matunda, maziwa, mayai, nk).
Waafrika
tunapenda nyama. Nyama ni muhimu sana maana ina madini aina ya chuma (nyama
nyekundu) protini,nguvu na mafuta. Ila mafuta yaliyoko katika nyama mara nyingi
si mazuri shauri hayatoki, huganda. Chukua nyama ya kuku na samaki ambayo huwa
na ngozi. Wengi wetu hupenda sana kula ile ngozi ya wanyama hawa kwa kuwa tamu.
Lakini haya ni mafuta mabaya.
Mafuta
ya samaki lakini ni mazuri. Samaki anayo mafuta ya Omega-3 ambayo husaidia mwili
na kinga maradhi mwilini.
Tunapokula
nyama choma au ya kukaanga, lazima tule pia mboga za majani (mbichi) na si
vizuri kula nyama kila siku. Kama huwezi kukaa bila nyama kila siku, fanya
mazoezi ya mwili.
PENDEKEZO LA 3- Kula
mbegu mbegu za korosho, karanga (ziwe mbichi badala ya kukaanga na chumvi) kati
kati ya siku. Haya ni mafuta yenye rutuba mwilini kuliko nyama za mafuta.
5-MAZOEZI YA MWILI NA
VIUNGO
Mazoezi
ni mfalme wa kupunguza unene.
Ukiwauliza
wengi watakuambia wanafanya kazi ngumu za sulubu (wanachuruzikwa jasho) kwa
hiyo hayo ni mazoezi. Ila kazi na mazoezi ni vitu viwili tofauti. Ingekuwa
kufanya kazi ni mazoezi basi kusingekuwa na wastani mfupi wa maisha kwa maskini
hasa sisi Waafrika.
Wengine
watadai kwamba walipokuwa wadogo shuleni walifanya mazoezi sasa wamekuwa watu
wazima (miaka 40 kuendelea) kwamba eti mazoezi ni suala la ujana; kumbe kadri
unavyokuwa ki umri ndivyo kadri unavyotakiwa kufanya mazoezi na kujitazama
zaidi kiafya.
Watazame
Wachina na Wajapani wanavyoishi maisha marefu.
Mazoezi
ni shughuli inayokufanya kwanza uheme (mapafu na moyo kwenda kasi), viungo na
mifupa kujinyoosha (stretching), kutoka jasho na usafishaji wa damu. Mazoezi
yanayosaidia haya ni pamoja na kutembea kasi, kukimbia, kuogelea, michezo
mbalimbali ya riadha (kama mpira wa miguu, nyavu, kikapu, mikono, nk); michezo
ya kupigana na kujilinda yaani masho ati(karate, kung fu, judo, capoeira, krav
maga, jiu jitsu, systema, kickboxing, thai boxing, kempo, kalari payatu,
aikido, nk)
Ni
muhimu mwanadamu ufanye mazoezi makali ya viungo mara mbili tatu kwa juma. Si
vizuri kufanya kila siku kwani musuli na mishipa inahitaji kupumzika na kukua.
Kama
unapenda kuinua vyuma lazima uwe na mwalimu wa kukuelekeza; na si vizuri
kufanya kila siku. Wastani wa mara mbili tatu kwa juma inatosha kabisa.
6-UPO UFANYAJI MAZOEZI WA AINA MBILI
Mazoezi
ya nguvu ya kuhema niliyotaja hapo juu (cardio-vascular) na yale laini ya
kujinyoosha yaani ambayo hutumia zaidi nguvu za ndani na pumzi. Haya ya pili ni
kama Yoga (India) , Tai Chi Chuan (China) na aina mpya mazoezi iliyoanza Majuu
miaka ya karibuni yaani Pilates (hutamkwa hivyo hivyo ilivyoandikwa Pilates).
Haya laini yanawafaa zaidi watu wazima na nchini China na Japan mathalan
utawakuta wazee wa miaka 80 hadi 90 bado wanayafanya. Husaidia moyo, damu na
akili.
Michezo
na mazoezi ya mwili ni njia kuu ya kupunguza unene, kurefusha maisha,
kuchangamsha ubongo, kupunguza ulevi, uvutaji sigara, dawa za kulevya, tabia
mbaya za uvivu, ugomvi, nk. Mataifa yenye watu wanaofanya mazoezi kama
Japan, Brazili, India, China nk huwa na wachapa kazi wengi na wananchi
wanaoipenda jamii yao.
7-KULA
SANA CHUMVI SI VIZURI
Ulaji
chumvi mwingi hutokana na suala la ladha. Kisayansi vyakula vyote vina
chumvi asilia sema tu tumezoea kuongezea madini hii iitwayo Sodium. Sodium
inachangia sana kufupisha maisha. Huifanya mishipa ya damu ichoke; ni kama
bomba lolote la maji ukilitazama baadaye hugeuka rangi kutokana na yale maji
kupita pale kila siku.
Kwa
wale tunaoishi nchi za joto na kutoka sana jasho kula chumvi ni muhimu. Ila
tatizo letu ni kwamba hatunywi maji ya kutosha. Mtu ukiwa na kiu unakunywa soda
au kinywaji cha sukari; inakuwa kama unaendelea kuutesa mwili. Kwa vipi?
Mishipa inayopitisha damu mwilini badala ya kusaidiwa kwa maji inawekewa kazi
zaidi ya kusafisha sukari na chumvi. Ndiyo maana vifo vingi vinatokea mapema;
wastani wetu wa maisha haupiti miaka 50.
Utafiti
uliofanywa chuo kikuu cha California, Marekani mwanzoni mwa 2010, umethitibisha
kwamba vifo vingi duniani husababishwa na maradhi ya moyo na saratani ambavyo
hutokana na uvutaji sigara, unene, ulevi na ulaji sana wa chumvi na sukari.
Tukipunguza ulaji wa chumvi tunasaidia pia kupunguza maradhi ya moyo, utafiti
unasema.
8-TAFITI ZA VYUO KADHAA
ULIMWNGUNI KUHUSIANA NA AFYA
-Jarida
la Kimarekani la sayansi lilieleza mwaka jana kwamba utapunguza ugonjwa wa moyo
(ambao husababishwa na unene , wasiwasi na purukshani) kwa asilia mia 42 kama
utakula matunda na mboga za majani peke yake kila siku, juu ya msosi wa
kawaida.
(PENDEKEZO LA KULA- Na
4- Kula mlo wako. Baada ya saa mbili au tatu, sakatia tunda au matunda; baada
ya mlo mwingine, kula sahani ya mseto wa mboga mbichi kama karote na matango.
Utaona tofauti ya afya, ngozi, wajihi, kinyesi, usingizi, nk. Kidesturi
tumezoea kunywa chai au soda za sukari sukari na gesi kati kati nya milo badala
ya matunda na mboga mbichi za majani).
-Utafiti
uliofanywa na wanasayansi chuo kikuu cha South Carolina mwanzo wa mwaka
2010 kuhusu faida za kuogelea.
Zoezi
la kuogelea lina faida zaidi ya kukimbia au kutembea kwa vile huchanganya
mazoezi makali na pumzi, kusaidia mapafu na moyo. Utafiti ulithibitisha
kuogelea hupunguza hatari za kifo kwa asili mia hamsini.
-Utafiti
wa jarida la chuo cha uganga Ulaya umeeleza (desemba 2009) kwamba kulala nusu
saa kila mchana (“nap”) husaidia kupunguza ugonjwa wa moyo kwa asilimia
37.
-Uchunguzi
wa chuo cha michezo cha Hispania mwanzoni mwa 2010 umethibitisha kwamba
ukikimbia mara tatu kwa juma (jogging) unaongeza nyege mwilini kwa asili mia
75. Hasa kwa watu wa makamo mnaoanza kupoteza nguvu za urijali.
-Uchunguzi
chuo kikuu cha Leeds, Uingereza mwanzoni mwa 2010 umeonyesha unapotembea
kwa miguu, ukikwepa barabara kubwa zisisokuwa na mioshi ya magari (pollution)
unapunguza matatizo ya maradhi ya hewa chafu kama pumu, mapafu na appendix.
-Uchunguzi
wa chuo kikuu cha Texas mwaka 2010 umegundua kwamba kula tunda la divai
nyekundu mara kwa mara husaidia kupunguza kupata ugonjwa wa kisukari.
-Hapo hapo tunaelezwa kwamba watu weusi na bara
la Asia wanakumbwa zaidi na ugonjwa wa kisukari kutokana na vinywaji vya sukari
sukari na gesi (fizzy drinks). Ukinywa kiasi cha miligramu 300 za vinywaji hivi
(Cocacola, Red Bull, Fanta, nk) kwa siku unajitahadharisha kupata
kisukari.
9-KUFUNGA
Neno
kufunga linatambuliwa rasmi kuhusiana na Waislamu (mwezi Ramadhani) au Wakristo
(Lenti nk). Ufungaji huo una masharti mengine ya kidini tofauti na haya ya
kiafya.
Mathalani
wafungaji hawa hula chakula kingi usiku; ukihesabu wanafunga wastani wa
saa 12 tu. Kawaida ukitaka virusi na takataka nyingine mwilini zitoweke, au
viungo vipumzike wahitaji saa 20 kuendelea.
Ufungaji
ninaouongelea ni ufungaji wa kutokula kabisa kwa saa 24, 36 hadi 48 kuendele
Ufungaji
ni nini?
Kama
mashine yeyote mwili wa mwanadamu unahitaji kupumzika na kujisafisha. Hata
tukiwa tumelala bado viungo mbalimbali mwilini vinafanya kazi. Kwa hiyo faida
ya kwanza kabisa ya kufunga ni kuupumzisha mwili kama mfanyakazi yeyote
anapokwenda likizo.
Faida
ya pili ya kufunga ni kusafisha mwili kutokana na uchafu ambao haukutoka
(kinyesi hakitoi mabaki yote toka utumbo mkubwa), dawa na takataka za mazingira
tunayoyavutia hewa, virusi au kuyanywa katika maji na vyakula mbalimbali na pia
uchafu wa hisia, yaani hasira, huzuni, nk.
Kuna
ufungaji wa aina mbalimbali.
1-Kufunga
kwa kunywa maji tu, saa 24 kuendelea…
2-Kufunga
kwa kutokunywa maji au kula chochote, saa 24 kuendelea…
3-Kufunga
kwa kula tu matunda au mboga zilizopondwa kama karote, matango nk, saa 24
kuendelea…
Ufungaji
huu unatakiwa ufanywe kwa mpangilio. Kitu muhimu si tu kufunga bali NAMNA
unavyofungua. Ukianza kula tena, unaanza taratibu. Kawaida ni vizuri kuanza na
maji, kikombe au bilauri ya kwanza taratibu. Subiri tena nusu saa, bilauri
nyingine, halafu hadi ya tatu, halafu ndiyo matunda yasiyo ya chachu, na
kadhalika. Kuanza kufungua kwa kunywa chai ya maziwa, uji au vyakula vingine
vya wanga hakusadii sana mfungo huu.
Maana
lengo lake ni kusafisha mwili.
PENDEKEZO LA 5- Kwa
wenye imani za kidini. Unaweza pia kufunga hivi ukawa pia unasali au kuvaa
mavazi yanayokufanya mtu wa amani. Ukifanya hivi unajitakasa kimwili na kiroho.
Si lazima ungojee ile miezi ya kufunga na wengine.
10-USINGAJI
Usingaji
au masaji ni njia nzuri sana ya kupunguza unene. Ikiwa unaangalia namna
unavyokula, unafanya mazoezi na kusingwa mara moja au mbili kwa mwezi
unaupalilia mwili vizuri. Nini faida ya usingaji? Kusinga husaidia ngozi,
mishipa ya damu na sura nzima ya mwili na taswira yako mwanadamu. Wengi wetu
tunaposikia neno kusinga tunafikiria usingaji wa mapenzi. Hivi ni vitu viwili
tofauti kwani usingaji wa mapenzi unaimanisha mahusiano ya kihisia.
Kifupi
mwanadamu unatakiwa uwe unautunza na kuungalia mwili wako kama nyumba au hekalu
lako. Wengi wetu tunaoga, tunajipaka marashi, tunasuka, tunanyoa nywele au
ndevu; lakini miili yetu kiundani inaoza taratibu…
Kama
alivyosema mpiganaji, msanii, mwanafalsafa, mwigizaji, mwandishi mashuhuri
marehemu Bruce Lee katika shairi lake Mazingira Yako Kimya (toka kitabu
“Msanii wa Maisha”, Turtle Publishing, 2001):
“NYAKATI NZURI,
HAZITAKAA ZIRUDI TENA”
(akiwa na maana yakabili
maisha yako sasa hivi, usisubiri; nyakati hazirejei nyuma).
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment