Mwanajeshi aua vijana wawili kwa bastola

 
Mwanajeshi wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ), ambaye jina lake limehifadhiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi baada ya kuwaua kwa kuwapiga risasi vijana wawili na kisha kuwajeruhi vibaya wengine wawili walipokuwa katika shamrashamra za kuukaribisha mwaka mpya. Tukio hilo lilitokea majira ya saa sita na robo usiku wa kuamkia jana, katika eneo la Pugu Kinyamwezi, Ilala jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na NIPASHE jana Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Marietha Minangi (pichani) alisema tukio hilo lilitokea baada kundi la vijana waliokuwa wakisherehekea mwaka mpya kuzingira gari la mwanajeshi huyo aliyekuwa akielekea nyumbani kwake Pugu Kinyamwezi, akitokea katikati ya Jiji kwa shughuli zake.

Alisema mwanajeshi huyo alikuwa na gari aina ya Toyota Rava 4 na baada ya kufika katika eneo hilo alizingirwa na kundi la vijana hao waliokuwa wakisherehekea mwaka mpya na ndipo aliamua kutoa bastola yake na kufyatua risasi ambapo iliwapata vijana hao na kufa papo hapo na kujeruhi wengine.
Aliwataja waliokufa katika tukio hilo kuwa ni Ibrahim Mohamed(16) mkazi wa Pugu Kinyamwezi, Abubakari Hassan(14) naye mkazi wa Pugu Kinyamwezi.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Rupano Wanga(17) mkazi wa Pugu Makange na Kassim Abdul (16), mwanafunzi wa shule ya sekondari Tandika.

Minangi alisema polisi walifanikiwa kumkamata mwanajeshi huyo na kumweka rumande katika kituo cha polisi cha Stakishari usiku huohuo.
Alisema vijana hao waliojeruhiwa walipelekwa Hospitali ya Amana kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.

Wakati huohuo, wakazi wa Kiwalani, Wilayani Temeke walipata wakati mgumu baada ya kutokea kwa kundi la vibaka waliokuwa wakipora simu, fedha na kutembeza mapanga kwa wakazi hao.
Kwa mujibu wa baadhi ya wakazi wa maeeno hayo, kundi hilo lilikuwa likizungukia kila nyumba na katika nyumba za starehe na kila aliyekutwa nje walichukua simu yake, fedha na wengie kupigwa mapanga. 
CHANZO: NIPASHE

Comments

Popular posts from this blog