‘Mijimama’ inavyoingiza waosha kucha, miguu katika hatari ya kuambukizwa VVU


Biashara hii inazidi kukua huku pia huduma zinazotolewa zikizidi kuongezeka kila kukicha, ambapo mara nyingi wanaotengeneza kucha, hujihusisha na
usuguaji wa miguu, uchoraji wa tattoo ukandaji wa mwili (massage)na nyingine zinazofana na hizo. 



Kwa ufupi


  • Eneo alilotaka nimchore ndilo lilianza kunipa wasiwasi, lakini kwa sababu ya pesa nikapiga moyo konde
  • Kazi hiyo huchangia kwa kiasi kikubwa pia kuwaweka vijana katika hatari ya kupata maradhi ya ngozi hasa fangasi kutokana na wengi wao kutotumia vifaa vya kujikinga.




Utengenezaji wa kucha na uoshaji miguu ni biashara inayokuwa kwa kasi hasa maeneo ya mijini ambapo wanawake wengi wanahusudu na kujihusisha na masuala ya urembo.
Biashara hii inazidi kukua huku pia huduma zinazotolewa zikizidi kuongezeka kila kukicha, ambapo mara nyingi wanaotengeneza kucha, hujihusisha na usuguaji wa miguu, uchoraji wa tattoo ukandaji wa mwili (massage)na nyingine zinazofana na hizo.
Kazi hii imetokea kuwa chanzo kimojawapo cha mapato na ajira mpya kwa vijana wengi hasa wa kiume, wenye umri wa miaka 17 hadi 35.
Hata hivyo, uchuguzi uliofanywa na gazeti hili hasa jijini Dar es Salaam, umegundua kuwa vijana wengi wanaofanya biashara hii huishia kufanya ngono na wateja wao hasa wanawake wenye umri mkubwa na wa kati (Mijimama), ambao wamewahi kuwahudumia zaidi ya mara moja, hivyo kutumbukia katika hatari ya kuambukizwa magonjwa ya zinaa na Virusi Vya Ukimwi(VVU).
Kwa mujibu wa takwimu za Ukimwi nchini, vijana wengi walio kwenye umri  kati ya miaka 17 hadi 35 ndilo kundi linalotajwa kuwa katika hatari kubwa ya kupata maambukizi ya VVU.
Hatari hiyo inatokana na mazingira hatarishi wanayokutana nayo vijana hao wanapofanya shughuli zao na kufanya vitendo hivyo kwa makusudi, wakati mwingine kwa kushawishiwa.
Uchunguzi unaonyesha kuwa wakati wa ufanyaji wa shughuli hiyo, hutokea baadhi ya wanawake wakaoshwa au kusuguliwa sehemu za miguu zinazokaribia maeneo ya mapaja, hivyo kuamsha hisia kati ya mtoa huduma na mpokea huduma.
Hatua hiyo inatajwa kuwasababashia baadhi yao kufanya ngono ambayo mara nyingi siyo salama, wanapotoa huduma katika maeneo tulivu ikiwamo saluni maalumu na  nyumbani kwa wateja.
Mmoja wa wafanyabiashara hiyo katika Soko la Mwenge Hamis Shaban(19) (siyo jina halisi) anasema kuwa kuna wakati wamekuwa wakiingizwa katika mtego na wateja wao, ambayo huwasababishia kufanya ngono.
Anasema kuwa hali hiyo hutokea mara nyingi hasa mteja anapotaka kwenda kuhudumiwa nyumbani kwake, ambapo hukuta tayari wameandaa mazingira, ambayo mwisho wake huishia katika hatua hiyo.
“Mimi mwenyewe imenitokea siku chache zilizopita; kuna binti fulani amekuwa mteja wangu kwa muda mrefu, amekuwa akinifanyia vituko vya hapa na pale. Nilikuwa sijali, ila majuzi akaniambia niende kwake nikamchore tattoo,” anasema Shaban na kuongeza:
“Eneo alilotaka nimchore ndilo lilianza kunipa wasiwasi, lakini kwa sababu ya pesa nikapiga moyo konde. Akavua blauzi yake na kutaka nimchore kwenye titi; nilijaribu kutimiza wajibu wangu, lakini mambo ambayo alikuwa akifanya, yalinisababishia uzalendo kunishinda, hatimaye tukajikuta tukifanya ngono.”
Shaban anakiri alifanya tendo hilo bila kutumia kinga akiamini kuwa msichana huyo ni mbichi na hana uwezekano wa kuwa na VVU.
Anafafanua kuwa sababu nyingine iliyosababisha kufanya ngono ilikuwa kutaka kujenga heshima kwa mteja wake huyo, ili amwone kuwa ni mwanaume aliyekamilika.
“Yule sista amenifanyia vituko muda mrefu, nikaona asije kunitangazia vibaya bure kwamba mimi siyo mwanaume kamili; hivyo kumwonyesha kuwa nimekamilika, nikalazimika kufanya, ingawa sasa hivi unavyoniuliza naanza kupata wasiwasi.”
Mahamod Abdalah anayefanya biashara hiyo eneo la Makumbusho, naye anakiri kuwepo na changamoto mbalimbali, ambazo huwafanya wengi wao kuingia kwenye mitego na kufanya kazi ya kuwafurahisha wake za watu.
“Hiyo changamoto kweli ipo, inahitaji moyo wa ziada kukabiliana nayo. Wanakuja wanawake wa haja, utakuta anakufunilia maungo, anataka umsugue; yaani hatari tupu, sasa kama huna ujasiri, lazima utaingia kwenye mtego.”
Pamoja na kuingizwa kwenye vishawishi hivyo kuna muda vijana hao hujikuta katika wakati mgumu, hasa wanapofanya shughuli hiyo nyumbani na kukutwa na waume wa wateja wao.
“Si wanaume wote wanaelewa kama hii ni kazi, mwingine akikukuta nyumbani kwake unamsugua mkewe, unaweza kuambulia kichapo na mambo kama hayo. Hizo ni miongoni mwa changamoto tunazokutana nazo,”anasema Abdalah.
Kauli ya TACAIDS
Mkurugenzi wa Uraghabishi na Habari wa Tume ya Taifa ya Kuthibiti Maambukizi ya Ukimwi (TACAIDS), Jummane Issango anakiri kuwa hali hiyo ni changamoto dhidi ya mapambano ya ugonjwa huo unaogharimu maisha ya vijana wengi nchini.
Anasema kuwa kutokana na hali hiyo kwa mwaka huu wa fedha, TACAIDS imejiwekea mkakati wa kutoa elimu kwa makundi ya vijana, ambao shughuli zao zinawaweka katika hatari ya kupata maambukizi ya Ukimwi.
“Kuna fursa nyingi za ajira kwa vijana, ambazo zimekuwa zikiibuka kila kukicha, lakini kwa bahati mbaya na kasi ya maambukizi ya Ukimwi inanyemelea katika fursa hizo, ndiyo maana mwaka huu tunakuja na mkakati wa elimu kwa vijana,”alisema.
Issango aliongeza: “Mpango huu utahusisha vijana walio shuleni na walio nje ya shule kama vile wasichana wanaojiuza, wahudumu wa bar na vijana wanaojihusisha na masuala ya urembo kama hayo kutengeneza kucha, kukanda mwili na mengineyo.”
Anasema kuwa mkakati huo utalenga kutoa hamasa kwa vijana wapende kujua hali zao kiafya na kujitoa katika hatari ya kupata maambukizi na kupima VVU kwa hiari.
Mtaalamu wa Afya, Samuel Shitta anasema kuwa hali hiyo kwa kiasi kikubwa inasababishwa na masuala ya kisaikolojia, pamoja na hisia za kimapenzi ambazo huwashika kwa haraka zaidi wanaume.
Anasema kuwa kisaikolojia, wanaume hushikwa na hisia za mapenzi kwa haraka zaidi kuliko wanawake, hivyo kitendo cha kuchezea au kusugua mwili wa mwanamke kinaweza kumsababishia akajikuta akifanya ngono bila kutarajia.
“Wapo ambao inawatokea kisaikolojia, lakini vilevile kuna kundi lingine ambalo hufanya kwa makusudi kwa lengo la kujiingizia kipato, wakiamini kuwa kufanya hivyo kunaweza kuwasaidia kupata kipato zaidi,”anasema Shitta.
Madhara mengine
Pamoja na madhara hayo, Shitta anafafanua kuwa kazi hiyo huchangia kwa kiasi kikubwa pia kuwaweka vijana katika hatari ya kupata maradhi ya ngozi hasa fangasi kutokana na wengi wao kutotumia vifaa vya kujikinga.
Anataja pia hatari ya kupata maradhi ya uti wa mgongo, kutokana na kundi hilo kuinama kwa muda mrefu linapokuwa kazini.
 “Kufanya shughuli hiyo kwa muda mrefu kunaweza kumfanya mtu akavunja pingili za mgongo hivyo kupata maradhi ya mgongo, hususani wakiwa uzeeni,”anasema Dk Shitta.



Comments

Popular posts from this blog