MAN UNITED YAKATAA MABILIONI KWA JANUZAJ
HATUTAKI,
na tena hatutaki hata kusikia. Na ikiwezekana msirudi tena. Ndivyo
ambavyo mapovu yamewatoka mdomoni watu wa Manchester United baada ya PSG
kurudi mezani juzi Jumapili na ofa ya kumtaka kinda wao mahiri, Adnan
Januzaj.
PSG
wamekuwa wakitokwa udenda kwa kinda huyo mwenye asili ya Albania
aliyezaliwa Ubelgiji miaka 18 iliyopita na hawajali kama aliingia
mkataba mpya wa kuichezea Man United mwishoni mwa msimu uliopita.
Hata
hivyo, kocha David Moyes amekataa ofa hiyo ya PSG inayodhaniwa kuanzia
Pauni 25 milioni na kuendelea huku wakisisitiza kwamba hawana mpango
hata wa kukaa chini na kuzungumza na matajiri hao wa mafuta kutoka
Paris.
Man
United imempatia mkataba mrefu wa miaka mitano Januzaj Oktoba mwaka jana
baada ya kugundulika kuwa huenda mchezaji huyo angekuwa huru na
kuondoka Mei mwaka huu mara baada ya msimu kumalizika.
Kabla na
baada ya kusaini mkataba huo, Januzaj ameibuka kuwa miongoni mwa
wachezaji wachache mahiri katika kikosi cha Man United ambacho msimu huu
kimekuwa kikisuasua ndani ya uwanja.
Kwa
mujibu wa gazeti la Guardian la Uingereza, Januzaj angeingiza kiasi
kikubwa cha pesa kama angeamua kukubali kwenda PSG, lakini mwenyewe
ameamua kubaki Man United licha ya timu hiyo kuwa katika hatari ya
kukosa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Katika
mkataba wake wa awali nyota huyo alikuwa akiingiza kiasi cha Pauni 1,000
tu kwa wiki kutokana na kuwa kinda mwanafunzi, lakini mkataba wake wa
sasa unamwingizia kiasi cha Pauni 30,000 kwa wiki.
Akiwa na
PSG angeweza kuingiza kiasi cha zaidi ya Pauni 80,000 kwa wiki, lakini
staa huyo ameamua kubaki Man United na kuendelea kujifunza zaidi wakati
huu kocha Moyes akimwamini na kumpanga mara nyingi zaidi katika safu ya
ushambuliaji.
Wakati
huohuo pia, PSG pia imekataliwa katika ofa yao ya Pauni 14 milioni kwa
ajili ya kumchukua kiungo mahiri wa Newcastle United, Yohan Cabaye
ambaye amekuwa akisakwa kwa muda mrefu na kocha Laurent Blanc.
Newcastle
inaamini kuwa staa huyo Mfaransa ana thamani ya Pauni 25 milioni na
inadaiwa kuwa hata Man United wameanza kumtolea macho Cabaye. Chanzo:
mwanaspoti
Comments
Post a Comment