HII NDIO LISHE KWA WANAOISHI NA UKIMWI
Tatizo la VVU/UKIMWI linaendelea kuwa tishio kwa maisha ya binadamu. Pamoja
na jitihada mbalimbali za kitabibu, imeonekana kuwa watu wengi wanaoishi na
virusi vya UKIMWI (VVU) au UKIMWI huathirika au hupoteza maisha yao
mapema zaidi kwa kukosa lishe bora.
Lishe bora kwa watu hawa ni muhimu ili
kuimarisha kinga ya mwili, ambayo huuongezea mwili uwezo wa kupigana na magonjwa nyemelezi na hivyo kumfanya mtu anayeishi na VVU/UKIMWI kuishi
muda mrefu zaidi.
Vile vile lishe bora huuwezesha mwili wa mtu anayeishi na
VVU/UKIMWI kustahimili dawa anazotumia.
Lishe bora hutokana na kula chakula mchanganyiko na cha kutosha. Pamoja na
lishe bora, mazoezi ya mara kwa mara ni muhimu vile vile katika kuimarisha
kinga ya mwili na kuupa mwili uwezo wa kupigana na magonjwa nyemelezi.
Watu wanaoishi na VVU/UKIMWI huweza kupata matatizo mbalimbali
yanayoweza kuwafanya washindwe kula vizuri au chakula kisiweze kutumika
ipasavyo mwilini na hivyo kudhoofisha zaidi kinga ya mwili.
Makala hii nitakupa maelezo kuhusu ulaji bora kwa watu wanaoishi na
VVU/UKIMWI.
Maelezo haya yamegawanyika katika maeneo mawili muhimu.
Eneo la kwanza linatoa maelezo ya jumla kuhusu ulaji bora kwa mtu anayeishi na
VVU/UKIMWI.
Eneo la pili linatoa maelezo zaidi kuhusu matatizo mbalimbali
yanayoambatana na VVU/UKIMWI ambayo yanaweza kukabiliwa kwa ulaji bora.
Ulaji bora kwa watu wanaoishi na VVU/UKIMWI
Kuishi na virusi vya UKIMWI huathiri kinga ya mwili hali ambayo husababisha
kuugua mara kwa mara na kupungua kwa uzito. Hali hii huchangia kuongezeka
kwa mahitaji ya virutubisho mwilini ambayo yasipokabiliwa huweza kusababisha
utapiamlo. Kuboresha hali ya lishe kutasaidia kuimarisha kinga ya mwili na hivyo
kupunguza makali ya UKIMWI.
Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya virutubisho, mtu anayeishi na
VVU/UKIMWI anapaswa kuongeza kiwango cha ulaji wa vyakula vyenye nishati,
utomwili (protini), vitamini na madini. Virutubisho hivi vinaweza kupatikana kwa
kula chakula cha mchanganyiko na cha kutosha kila siku.
Inashauriwa kuwa vyakula hivyo vitokane na makundi yafuatayo:
1.Vyakula vya nafaka, aina ya mizizi na ndizi za kupika
Kazi kubwa ya vyakula hivi ni kuupa mwili nguvu na joto. Vyakula katika kundi
hili ni pamoja na nafaka kama vile mahindi, mchele, mtama, ulezi, ngano na
uwele; aina ya mizizi kama viazi, mihogo na magimbi; na ndizi za kupika.
Nafaka zisizokobolewa zina virutubisho zaidi vya vitamini B na nyuzinyuzi (fibre)
kuliko zile zilizokobolewa. Mara nyingi vyakula hivi huchukua sehemu kubwa ya
mlo. Pamoja na vyakula hivi kuupa mwili nguvu na joto, vile vile huupa kiasi
kidogo cha madini, vitamini na utomwili (yaani protein)
2.Vyakula vya jamii ya mikunde, vile vyenye kokwa na vyenye asili ya wanyama
Vyakula hivi huupatia mwili utomwili(protein) kwa wingi ambao ni muhimu katika kujenga
mwili na misuli. Vyakula vyenye asili ya mikunde ni kama maharage, njegere,
kunde, soya, njugumawe, dengu na choroko; vyenye kokwa kama karanga na
korosho. Vyakula vyenye asili ya wanyama ni pamoja na nyama, samaki, dagaa,
maziwa, mayai, jibini, maini, figo, senene, nzige na kumbikumbi. Vile vile vyakula
hivi huupatia mwili kiasi kidogo cha vitamini na madini.
3.Mafuta na sukari
Mafuta na sukari huongeza nguvu na uzito wa mwili. Vyakula hivi pia huongeza
ladha ya chakula. Vyanzo vya mafuta ni kama vile samli, siagi, ufuta, alizeti,
kweme, mawese na karanga; na sukari hupatikana katika asali, miwa, sukari
guru na ile ya kawaida. Asali na sukari guru zina vitamini na madini kwa wingi
kuliko sukari nyeupe.
4.Matunda
Matunda ni chanzo kizuri cha vitamini na madini. Virutubisho hivi husaidia
kuimarisha kinga ya mwili. Kundi hili linajumuisha matunda kama vile mapapai,
maembe, mapera, malimao, mapesheni, mananasi, peasi, ubuyu, ukwaju,
machungwa na mabungo.
5.Mboga mboga
Mboga mboga kama vile mchicha, majani ya kunde, matembele, mnafu,
mchunga, majani ya maboga na karoti zina vitamini na madini kwa wingi.
Vitamini na madini ni muhimu sana katika kuboresha kinga ya mwili hasa kwa
watu wanaoishi na VVU/UKIMWI.
6.Maji
Maji pia ni muhimu kuuwezesha mwili kufanya kazi inavyotakiwa. Inashauriwa
kunywa maji safi na salama na ya kutosha kiasi kisichopungua lita 1.5 ambazo ni
karibu sawa na glasi nane kwa siku. Vinywaji vingine vinavyoweza kuupa mwili
maji ni pamoja na madafu, togwa na maji ya matunda mbali mbali.
7.Vyakula vyenye nyuzi nyuzi
Vyakula vyenye nyuzi nyuzi ni muhimu mwilini kwa sababu humsaidia mtu
aweze kupata haja kubwa kwa urahisi. Vyakula vitokanavyo na mimea kama vile
mboga za majani, matunda, nafaka zisizokobolewa na jamii ya mikunde vina
nyuzi nyuzi kwa wingi. Vyakula hivi ni kama viazi vilivyopikwa na kuliwa bila
kumenywa, karoti, spinachi, kunde, mbaazi, maharage, machungwa; na mahindi
yasiyokobolewa.
Inashauriwa
• Kula chakula cha kutosha kutoka katika makundi yote ya vyakula kila siku;
• Kuongeza kiasi cha matunda na mboga mboga;
• Kutumia zaidi nafaka zisizokobolewa;
• Kupika vyakula vya asili ya nyama mpaka viive vizuri. Vyakula hivi vikiwa
havijaiva ni chanzo cha maambukizo;
• Kuepuka unywaji wa pombe kwani hupunguza uwezo wa mwili kupata virutubisho muhimu;
• Kuepuka uvutaji wa sigara kwani hupunguza hamu ya kula na kudhoofisha
kinga ya mwili;
• Kupunguza utumiaji wa vinywaji vyenye kafeini kwa wingi kama vile
kahawa, chai na soda aina ya kola kwa sababu huathiri ufyonzwaji wa
baadhi ya virutubisho;
• Kuzingatia usafi wa mwili na mazingira ili kupunguza hatari ya kupata
magonjwa ya kuambukiza; na
• Kupunguza kazi ngumu na nzito kwani hutumia kiasi kikubwa cha nishati
ambayo huhitajika ili kujenga kinga ya mwili.
KUMBUKA
Watu wanaoishi na VVU/UKIMWI wanahitaji virutubisho zaidi kuliko watu wasio na virusi kwa sababu miili yao inatumia virutubisho kwa kasi zaidi ili kupigana na maambukizo hayo.
Imeandaliwa na;
Sayi Manyanda
Comments
Post a Comment