HELKOPTA YA CHADEMA YAPOTEA ANGANI
HELIKOPTA
ya Chadema maarufu kama Chopa, juzi ilipotea angani na kusababisha
viongozi wa chama hicho kushindwa kufanya mkutano katika Kijiji cha
Mpwayungu wilayani Chamwino, kama ilivyokuwa imepangwa kwenye ratiba.
Kwa mujibu wa
ratiba iliyokuwa imepangwa, viongozi wa kitaifa ambao ni Mwanasheria
Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu na Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana
(BAVICHA), walikuwa wafanye mkutano katika kijiji hicho saa 4 asubuhi.
Akizungumza na MTANZANIA, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Dodoma,
Steven Massawe alikiri kupotea kwa helikopta hiyo na kukanusha kwamba
hakuna njama zozote zilizofanywa na CCM kutokana na kupotea kwa
helikopta hiyo.
Kijiji cha Mpwayungu kipo katika Kata ya Mpwayungu, ambayo nafasi ya
udiwani ipo wazi na vyama vya Chadema na CCM vyote vimesimamisha
wagombea.
“Sababu kubwa ya kupotea kwa helikopta ni tatizo la mawasiliano kama
mnavyojua Kijiji cha Mpwayungu hakina mawasiliano. Helikopta ilikuwa
ifike katika Kijiji cha Mpwayungu saa nne asubuhi, lakini Kapteni
alipotea na kusababisha kukaa angani kwa saa moja na dakika arobaini na
akatua Kijiji cha Chipogolo.
“Alipofika Chipogolo akaambiwa sio kijiji hicho chenye mkutano na
akatakiwa kurudi nyuma kwa upande wa magharibi kwa kilometa 40, hata
hivyo hakufanikiwa ikabidi arudi mjini kujaza mafuta,” alisema Massawe.
Alisema baada ya kujaza mafuta, viongozi hao hawakwenda tena kufanya
mkutano Mpwayungu badala yake wakaenda Mpwapwa ambapo kulikuwa na
mkutano mwingine saa 7 mchana kwa mujibu wa ratiba.
“Leo (jana) hii viongozi hao kwa kutumia helikopta wamekwenda tena
Mpwayungu na kufanikiwa kufanya mkutano majira ya saa nne asubuni na
baada ya hapo waliekea Kijiji cha Segala Wilaya ya Chamwino, baadaye
wataenda Kiteto na Moshi,” alisema.
Alisema sio kweli kwamba CCM walifanya njama helikopta ya Chadema
ipotee ili isifanye mkutano katika kijiji hicho na kwamba Chadema na CCM
vyote vilishafanya uzinduzi wa kapteni katika kata hiyo.
“Chadema ilifanya uzinduzi wake wa kampeni katika Kata ya Mwayungu,
Januari 26 mwaka huu na CCM walifanya uzinduzi wao Januari 20,” alisema
Massawe.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.
Willibrod Slaa, amesema iwapo Serikali ya CCM haitaweka mazingira ya
haki kwa makundi mbalimbali ndani ya jamii kwa ajili ya amani ya kudumu,
migogoro ya ardhi italitumbukiza taifa katika sintofahamu na hatari
kubwa nchini.
Dk. Slaa aliyasema hayo kwenye mikutano ya M4C Pamoja Daima, jana
alipokuwa akiwahutubia wananchi wa maeneo ya Iselamagazi, Kishapu,
Mhunze, Itilima, Lugulu na Bariadi.
Alisema ni haki kwa wananchi kuwa na matumaini, kwani ndiyo misingi wa amani ya kweli ambayo haihitaji kuhubiriwa jukwaani.
Comments
Post a Comment