TUNA MUDA WA KUTOSHA KUJADILI MAISHA?ONGEA NA MWENZA WAKO

NI  matumaini yangu kuwa wote ni wazima wa afya njema na mnaendelea vizuri na mihangaiko ya kila sikuya  maisha. Ni wakati mwingine tena tunakutana kujadili mambo yetu ya mapenzi na maisha.

Leo nina jambo moja la msingi ambalo ningependa kujadili kwa pamoja, wakati huu tunapokaribia kumaliza mwaka na kuukaribisha mwaka mwingine. Najua wazazi wengi hiki ni kipindi cha maumivu kwa vile tutalazimika kutumia fedha kwa ajili ya kuandaa sherehe za Krismas na mwaka mpya.


Lakini wakati tukishangilia kwa kuuona mwaka mpya 2014 kwa wale watakaojaaliwa, tutakutana tena na machungu ya maisha kwa sababu tutakuwa tunajipanga kuwapeleka watoto shuleni, ambao nao watachukua sehemu kubwa ya kipato kidogo kitakachobaki baada ya matumizi ya sikukuu.
Mara nyingi tumekuwa tukijadili kuhusu mapenzi baina ya wanandoa na walio katika uhusiano, migogoro, adha, raha na karaha zake, lakini ni mara chache sana tumezungumzia juu ya watoto wetu, ambao ni muhimu mno kwetu pengine kuliko hata sisi wenyewe.
Na hapa ni kuhusu tabia zao. Wote sisi ni mashahidi wa jinsi baadhi ya watoto tunaoishi nao katika mazingira yanayotuzunguka walivyo na tabia mbaya au nzuri. Tumejaribu kujiuliza ni nani hasa yupo nyuma ya tabia hizi?
Kama hatukupata muda huo, basi ni vyema nikawashirikisha kujua kwamba anayetengeneza tabia ya mtoto ni sisi wazazi, kwa maana ya baba na mama au walezi. Hakuna jinsi ambavyo tunaweza kukwepa, vijana wetu wanavyogeuka kuwa wadokozi, malaya, wavuta bangi, mashoga na tabia nyingine ambazo ni kinyume na maadili yetu kama taifa.
Wengi wetu, hasa wale wenye kipato cha kutosha kuwapeleka watoto shule hizi za binafsi, huliacha jukumu hili mikononi mwa walimu, tukiamini kwamba kwa kulipa ada, jukumu letu kama wazazi linakuwa limemalizika.
Na tena, akina baba ambao kwa hulka yetu ndiyo tunaowalipa ada, huliacha jukumu la kuratibu ratiba ya watoto mikononi mwa akina mama. Mama ndiye anayejua watoto wanafanya lini mitihani, anasimamia kazi za nyumbani (home works), lini wanafunga shule na jinsi ya kwenda kuwachukua.
Na kama mama naye ni muajiriwa, hali huwa mbaya zaidi, kwani jukumu hili sasa huachiwa msichana wa kazi. Kila siku wazazi watarudi nyumbani watoto wakiwa wamelala. Hupata maagizo ya walimu kupitia kwa msaidizi wa kazi, kitu ambacho ni hatari.
Ni kwa msingi huo basi, najaribu kuwashauri wazazi kutenga muda kila siku kuhakikisha ratiba ya mtoto zao zinakwenda kama vile wanavyependa iwe. Kama hutajishughulisha, hautaweza kujua kama kijana wako wa kiume ameanza kufanyiwa mchezo mbaya na wenzake shuleni.
Vilevile, ni vigumu kujua kuwa binti yako mdogo, anatendewa ndivyo sivyo, ama na jirani, walimu, wahuni au watu wengine wowote wenye nia mbaya. Tutenge muda, tuzungumze na watoto wetu, tuwaulize na tuwape nafasi ya wao pia kutuuliza maswali.
Kama nilivyosema awali, kutokujali au kujali kwetu, ndiko kunakotengeneza tabia zao. Kama baba atarudi nyumbani kila siku akiwa anayumba kwa kilevi na haulizi kuhusu watoto, atatoa picha kwamba hajali au anamuamini mama.
Kanuni moja muhimu sana katika malezi ya watoto ni kwa wazazi kutoaminiana. Kila mmoja lazima ajenge wasiwasi juu ya malezi ya mwenzake kama yanatia shaka. Aamini kuwa yeye ndiye bora zaidi katika malezi kuliko mwenzake.
Hapo tutatengeneza tabia za watoto tuzitakazo. Tutawahimiza kwenda katika ibada, tutawakataza kucheza ovyo, tutawafundisha kufanya kazi za nyumbani, tutawaelekeza jinsi ya kuwaheshimu wakubwa zao na kila kilicho chema.

NINI MAONI YAKO MDAU WETU?

Comments

Popular posts from this blog