Taarifa ya kusimamishwa uongozi kwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilayani Monduli
- Get link
- X
- Other Apps
TAARIFA KWA UMMA
Kwa
niaba ya baraza la uongozi la mkoa wa Arusha, napenda kuujulisha umma
wote kwa ujumla kuwa mwenyekiti wa wilaya ya monduli Mchungaji Amani
Silanga Mollel amekoma/amesimamishwa kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya
ya monduli kuanzia tarehe 29 Novemba 2013 kufuatia tuhuma nzito za
uvunjifu wa kanuni za maadili ya chama.
Hatua
hii imefikiwa baada ya kuthibitika na yeyé mwenyewe kukiri mbele ya
kikao cha kamati tendaji ya wilaya ya monduli kilichoketi tarehe 29
Novemba 2013 saa NNE asubuhi kuwa alitoa tamko batili akitumia wadhifa
wa mwenyekiti wa wilaya bila ridhaa ya kamati tendaji na huku
akidanganya kuwa ni tamko kwa niaba ya wilaya ya monduli.
Katika
tamko lake ametoa tuhuma dhidi ya wajumbe wa kamati kuu na viongozi
wakuu wa kitaifa kwa maamuzi halali ya kikao cha kamati kuu huku akijua
kuwa anavunja kanuni za chama kwa mujibu wa katiba ya chama toleo la
mwaka 2006 ya
Kanuni za uendeshaji kazi za chama, sura ya KUMI, ibara ya 10 (X) “Kiongozi
asitoe tuhuma zozote juu ya viongozi wenzake pasipo kupitia vikao
halali na kuzingatia taratibu na ngazi zilizoelezwa kwenye kanuni za
chama”.
Sambamba
na hilo, Mchungaji Amani Silanga ametoa tuhuma za uzushi, uongo na
upotoshaji na kutaka kuaminisha jamii kuwa chadema ina makundi ya
CHADEMA Asili na CHADEMA Family kitu ambacho ni upotoshaji mkubwa na wa
hatari kwa ustawi na umoja wa chama na kinyume na kanuni za uendeshaji
kazi za chama, sura ya KUMI, ibara ya 10 (VII), “Kiongozi
anatakiwa kuwa mkweli na muwazi wakati wote hususani katika vikao
halali na aachane na vikundi vya majungu, wadanganyifu (Rumour Mongers).
Ni mwiko kwa kiongozi kujihusisha na upotoshaji wa maamuzi wa vikao
halali”.
Kamati
tendaji ya wilaya ilipomtaka aonyeshe CHADEMA asili ni kina nani na
CHADEMA family ni kina nani alishindwa kutoa maelezo yoyote ya maana na
kufikia hatua ya kutaka kuvuruga kikao kwa kuleta vijana wahuni wapatao
17 ndani ya kikao ambao wengi walijulikana kuwa sio WANACHADEMA. Katika
utambulisho wake wa majigambo Mchungaji Amani SIlanga kwa kiburi na
kejeli amejitambulisha na kukiri kuwa yeye yupo kambi ya Zito Kabwe na
hakuna wa kumfanya kitu maana ni mjumbe wa baraza kuu la chama. Maneno
yake yalidhihirisha kuwa Mchungaji Amani Silanga anashiriki mpango wa
kuunda makundi yasiyo na tija ndani ya chama na hivyo kuwa kinyume na
sura hiyo hiyo ya kumi ya kanuni za uendeshaji kazi za chama ibara ya 10
(IX), “Kiongozi asijihusishe au
kushiriki na vikundi au vitendo vya kuchonganisha au kuzua migogoro
ndani ya uongozi wa chama au wanachama wake”.
AZIMIO LA BARAZA LA UONGOZI LA MKOA WA ARUSHA:
Baraza
la uongozi la mkoa lililoketi tarehe 29 Novemba 2013, limepokea
mapendekezo ya kamati tendaji ya wilaya na kuzingatia hofu kubwa
iliyoainishwa na kamati tendaji kufuatia matendo mengi yanayotia shaka
ya uadilifu na uwezo wa kiuongozi wa Mchungaji Amani Silanga na hivyo
baraza la uongozi la mkoa limeridhia kuwa amevunja kanuni za maadili ya
chama sura ya KUMI ibara ya (VII) hadi (XII) na hivyo kupelekea ukomo wa
yeye kuwa Mwenyekiti wa wilaya kuanzia tarehe 29 Novemba 2013. Baraza
la mkoa likiwa mamlaka ya nidhamu kwa mujibu wa katiba ibara ya 6.3.6
(a) (iv) limemjulisha tuhuma zake na hatua hii stahiki iliyochukuliwa.
Kwa vile Mchungaji Amani Silanga alikiri kosa hili mbele ya kamati
tendaji ya wilaya bila kulijutia au kuomba msamaha, baraza la mkoa
limechukua hatua hii stahiki kwa maslahi ya chama na kuwa uchunguzi
zaidi utafanyika ili kufikia maamuzi makubwa zaidi ya tuhuma nyingi kwa
mujibu wa kanuni za hatua za kinidhamu.
Baraza
la uongozi la mkoa wa Arusha, linatoa onyo kwa wote ambao wapo katika
mtandao huu mchafu, ama watoke wenyewe mapema maana hawatavumiliwa
kamwe. Baraza la uongozi wa mkoa liliona kuwa Mchungaji Silanga
amepotoka na hivyo yeyé kuendelea kuwepo ndani ya chama wakati wa
uchunguzi wa tuhuma hizi nzito dhidi yake ni hatari zaidi kwa ustawi wa
chama na hivyo baraza likaridhia kwa kuzingatia tafsiri ya katiba ya
chama ibara ya 6.3.4 (c) wa yeyé kukoma uongozi na hivyo akae nje kwa
muda na waliopotoka wenzake.
Amani Golugwa
Katibu wa CHADEMA – Mkoa wa Arusha.
(Kwa niaba ya Baraza la Uongozi la Mkoa wa Arusha)
Tarehe 30 Novemba 2013
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment