Simulizi Za Mzee Madiba: Mandela ' Alipochacha Mfukoni' Akiwa Safarini.

1472784_10201893038180362_546525959_n_6bd7c.jpgNa Maggid Mjengwa,
Tunaendelea na simulizi hizi za Mzee wetu Madiba. Na hapa kuna bashraf ya tulikoishia asubuhi...
"Mandela akajikuta amesimama miongoni mwa waheshimiwa na kukaribishwa chai. Na ghafla kukawa na foleni ya waheshimiwa wabunge mbele yake Mandela. Naye Mandela akashangazwa sana kuona wabunge wale wamejipanga mstari, na mmoja baada ya mwingine anakwenda mbele yake kumshika mkono na kumsalimu kwa heshima kubwa.
Wakati tukio hilo likiendelea kumshangaza Mandela, basi, ilipofika zamu ya Mbunge wa tatu kwenye mstari kumsalimu Mandela akasikia sauti ikimtamkia kutoka kwa Mbunge huyo;
" It is a great honour to shake the hand of the reverend Chief Luthuli, winner of the Nobel Peace Prize." ( Nelson Mandela, Long Walk To Freedom, pg. 357.)
Kwamba mbunge huyo alitamka kuwa ilikuwa heshima kubwa kwake kushikana mikono na Chifu Luthuli, mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobeli. Ndipo hapo Mandela akafahamu, kuwa Karani yule wa Bunge alichanganya mambo! .. Endelea..(P.T)
Mwaka bado ni 1962, Mandela akafika mpaka nchi ya Liberia, huko akakutana na Rais Tubman, ambaye, si tu alimpa Mandela dola za Kimarekani 5000 kama msaada wa kununua silaha na mafunzo, bali, Rais yule wa nchi ya Kiafrika akamtamkia Mandela kwa sauti ya upole;
" Have you any pocket money?"- ( Nelson Mandela, Long Walk To Freedom, Uk. 357)
Kwamba Rais yule alimwuliza Mandela kama anazo fedha za mfukoni kwa safari yake. Na ukweli Mandela ' alichacha' mfukoni. Hakuwa na fedha za kutosha. Mandela anasimulia, kuwa ilibidi aseme ukweli kwa kumwambia Rais Tubman kuwa hakuwa na kitu mfukoni. Mara akaja msaidizi wa Rais na bahasha yenye fedha taslimu. Ni dola za Kimarekani 400. Kwa miaka hiyo hizo ni fedha nyingi sana.
Na ikafika siku Mandela akatua Guinea ya Sekou Toure. Hapo akamkuta Rais aliyeishi kwenye nyumba ya hadhi ya wastani. Rais aliyevaa suti iliyofubaa na ambayo labda ingehitaji kupelekwa ' dry cleaner'.
Mandela anasimulia;
" Tukamwelezea Rais juu ya suala letu na hususan juu ya historia ya ANC na harakati zetu za Umkhoto We Sizwe. Kisha tukamwomba msaada wa dola za Kimarekani 5000 zisaidie kwenye harakati zetu".
Mandela anazidi kusimulia, kuwa Rais Toure alionekana kuwasikiliza kwa umakini sana. Kisha Rais akawajibu, kuwa Serikali ya Guinea inayaunga mkono mapambano yao. Na kwamba hilo wameliweka wazi hata kwenye Umoja wa Mataifa. Kisha Rais Toure akafungua kisanduku chake na kutoa vitabu viwili alivyoviandika mwenyewe. Akawapa kama zawadi; Mandela na Oliver Tambo. Na kikao kikaishia hapo.
" Oliver na mimi tulifadhaishwa kidogo" Anasema Mandela. Hisia hizo za Mandela zinatokana na ukweli kuwa walifunga safari ndefu tena kwa wito maalum wa Serikali ya Guinea, watoke Ghana waende Guinea wakutane na Rais Toure. Badala yake wamekuwa na mkutano kama huo bila kujibiwa hata maombi yao ya msaada wa kifedha kwa harakati zao. Kwamba wameambulia nakala mbili za vitabu. Mandela na Tambo walihisi wamepotezewa muda wao.
Baadae, Mandela na Tambo wakarudi kwenye hoteli waliyofikia. Na hapo akafika afisa wa Idara ya Mambo ya Nje ya Guinea. Akagonga mlango wa akina Mandela. Akawakabidhi sanduku lililojaa manoti. Kwanza Mandela na Tambo walibaki wameduwaa.
Oliver Tambo akazinduka na kumwambia Mandela;
" Nelson, this is Guinean currency, it is worthless outside here; it is just paper"
Kwamba sanduku walilopewa lilijaa noti za ' fedha za madafu' kwa maana ya sarafu za Guinea ambazo nje ya mipaka ya Guinea zinageuka kuwa karatasi tu!
Na ikafika muda wa Mandela kurudi tena Afrika Kusini. Lakini, kwa vile anakwenda kushiriki harakati za kijeshi za chini chini za Ukmhoto we Sizwe, Mandela alihitaji mafunzo maalum ya kijeshi. Na Mfalme Haile Selassie, ' Simba wa Yudah' alimwandalia Mandela Kanali mahiri katika jeshi lake la Kifalme. Ni Kanali wa kumpa Mandela mafunzo hayo maalum ya kijeshi.
Je, nini kilimtokea Mandela kwenye mafunzo hayo maalum kwenye nchi ya milima ya Abyssinia kwa maana ya Ethiopia?

Comments

Popular posts from this blog