SALAMU ZA X- MASS TOKA PAPA FRANCIS


Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Francis.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Francis.
Leo ni sikukuu ya Krismasi inayoadhimisha miaka 2,013 ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo, ambapo mkuu wa Kanisa Katoliki, Baba Mtakatifu Francis, amewatolea wito Wakristo kufungua nyoyo zao na kupambana na nguvu za giza.
Akiendesha misa ya mkesha wa Krismasi katika Kanisa la Mtakatifu Petro, ambayo ni ya kwanza kwake tangu kuchaguliwa kuongoza kanisa hilo lenye wafuasi bilioni 1.2 duniani, Baba Mtakatifu Francis amesema Wakristo hawapaswi kuachia ubinafsi kuyaongoza maisha yao.
"Mungu ni nuru, na kwake hakuna giza lolote", alisema Papa Francis akinukuu kitabu cha Injili ya Mtakatifu Yahya, akiwasifu wachunga kondoo wa Uzawa, ambao alisema ni watu pekee walioshuhudia kuzaliwa kwa Yesu Kristo mjini Bethlehem "kwa kuwa walikuwa ni watu wa mwisho, masikini wanaotengwa.
Papa huyo mwenye asili ya Argentina na ambaye amewavutia wengi kama mwanaharakati wa haki za wanyonge tangu kuchukua nafasi ya mtangulizi wake, Mjerumani Benedict wa 16 mapema mwaka huu, alitoa wito kwa waumini wa Kikristo kupambana na udanganyifu, ufahari na ubinafsi, ambavyo kwa pamoja aliviita roho ya giza.
Krismasi Bethlehem
Katika mji wa Bethlehem ulioko Ukingo wa Magharibi, na ambako Wakristo wanaamini ndiko alikozaliwa Yesu Kristo, Askofu Mkuu Fuad Twal, aliongoza misa ya mkesha wa Krismasi iliyohudhuriwa pia na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton.
Maelfu ya watalii na mahujaji walivuuka ukuta uliojengwa na Israel kuzitengenisha pande hizo mbili, kufika kilele cha mlima wa Palestina, ambako bado mabaki ya theluji yangalipo kutokana na majira ya kipupwe yanayoendelea huko. Katika eneo ambalo inaaminika Bikira Maria alimzaa Yesu kumewashwa mishumaa kuashiria uzawa wake.
Askofu Twal ametumia hotuba yake ya misa ya Krismasi kutoa wito wa kupatikana kwa suluhisho la haki na usawa kwenye mgogoro wa miongo kadhaa kati ya Israel na Palestina.
"Kwa Wakristo, jibu halipo kwenye kuhama wala kujifungia, bali kubakia hapa," alisema kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 73, akiongeza kwamba kutokea kwenye ardhi tukufu aliyozaliwa Yesu, Wakristo wanakumbuka majanga ya kilimwengu hivi sasa: "kutokea vita vya wenyewe kwa wenyewe barani Afrika hadi kimbunga cha Ufilipino, hali ngumu Misri na Iraq na msiba unaoendelea Syria."
Miongoni mwa athari za vita vya Syria, ni kuharibiwa kwa kijiji cha asili cha Wakristo cha Maalula, ambalo maelfu ya wakaazi wake wamegeuka wakimbizi, na wengi wao hadi leo wanazungumza lugha ya asili ya Kiarmania, iliyozungumzwa na Yesu.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/ReuterS
Mhariri: Iddi Ssessanga

Comments

Popular posts from this blog