Rasimu ya pili ya Katiba Mpya yakamilika

 
Hatimaye Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba imekamilisha kazi ya kuboresha rasimu ya kwanza na kupata rasimu ya pili ya Katiba Mpya tayari kwa hatua nyingine.
Taarifa zilizotufikia jana zilieleza kuwa Makamishna na Wajumbe wa Sekretarieti wa tume hiyo, walianza kurejea ofisini juzi na jana, wakitokea Hoteli ya White Sands walikojichimbia tangu Desemba Mosi mwaka huu kukamilisha rasimu hiyo. Awali, Rais Jakaya Kikwete aliiongezea tume hiyo siku 14 zaidi kukamilisha kazi zake. Siku hizo zitakamilika siku 11 kuanzia leo.
Jaji Warioba, Makamu wake Jaji Augustino Ramadhan na Katibu wa Tume hiyo, Assaa Rashid hawakupatikana kutokana na kilichoelezwa kuwa walikuwa kwenye kikao. Gazeti hili lililazimika kumtafuta Naibu Katibu, Casmil Kyuki ambaye naye alithibitisha taarifa hizo.
“Ni kweli sisi (Wajumbe wa Sekretarieti) tumerejea ofsini jana na wenzetu (Makamishna) walirejea tangu juzi. Kazi zetu tumezikamilisha kilichobaki tunafanya mawasiliano na Mkuu (Rais Jakaya Kikwete), tujue lini tutawasilisha kazi hii,” alieleza Kyuki
Hata hivyo, kiongozi huyo aligoma kutoa taarifa zaidi akisema maelezo kamili yatatolewa kwenye mkutano utakaohusisha tume na vyombo vya habari wakati wowote kuanzia kesho.
Akizungumzia uamuzi uliyofikiwa na Bunge, unaotaka tume hiyo ivunjwe mara baada ya kukabidhi rasimu hiyo kwa Bunge Maalumu la Katiba, Kyuki alisema wao wanaafikiana na uamuzi huo.
“Kila kitu maishani kina uzuri na ubaya wake, hata kama tungetakiwa kuwamo tungewasaidia wakiwa ndani ya kamati, lakini wangeweza kufanya tofauti wakiwa kwenye mijadala bungeni kwa hiyo bado kuwepo kwetu kusingesaidia kitu,” alisema Kyuki ambaye pia ni Mwandishi Mkuu wa Sheria Tanzania.

Comments

Popular posts from this blog