MTU MMOJA AKUTWA NA BUNDUKI PAMOJA NA RISASI 13 JIJINI ARUSHA

GEDSC DIGITAL CAMERAKamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas akiwaonyesha waandishi wa habari (Hawapo pichani) bunduki aina ya shortgun iliyokutwa nyumbani kwa mtu anayejulikana kwa jina na Jumanne Abdallah Maarufu kwa jina la Babu G (25) Unga Ltd jijini hapa ambaye anatuhumiwa kuhusika katika matukio mbalimbali ya ujambazi hapa nchini. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
GEDSC DIGITAL CAMERAKamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas akionyesha risasi zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa wa ujambazi Jumanne Abdallah maarufu kwa jina la Babu G maeneo ya Unga Ltd jijini hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Na Rashid Nchimbiwa Jeshi la PolisiArusha
Mtu mmoja anayetuhumiwa kwa ujambazi ajulikanaye kwa jina la Jumanne Abdallah Maarufu kwa jina la Babu G (25) Mkazi wa Unga Limited jijini hapa amekamatwa na Jeshi la Polisi akiwa na bunduki aina ya short gun pamoja na risasi 13 zinazotumika katika bunduki ya aina hiyo.
Bunduki hiyo yenye namba C. 056900 iliyokuwa imekatwa kitako na mtu ilikutwa nyumbani kwa mtuhumiwa huyo, maeneo ya Unga Limited katika Halmashauri ya jiji la Arusha mara baada ya Jeshi la Polisi kupata taarifa kutoka kwa raia wema.
“Mara baada ya kupata taarifa, askari wetu walikwenda katika nyumba hiyo muda wa saa 2:30 asubuhi na kumkuta mtuhumiwa katika chumba chake ambaye kwa wakati huo alikuwa anajiandaa kutoka, ndipo walipomkamata kisha kufanya upekuzi katika chumba hicho na kuikuta silaha hiyo pamoja na risasi hizo”. Alisema Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Liberatus Sabas.
Kamanda Sabas aliendelea kusema kwamba, mara baada ya mtuhumiwa huyo kuhojiwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa, alikiri kuhusika katika matukio mbalimbali ya uhalifu kama vile unyang’anyi wa kutumia nguvu na silaha katika maeneo mbalimbali hapa nchini huku akiwataja wenzake ambao wanaendelea kutafutwa na Jeshi hilo na atafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika.
Kamanda Sabas ameendelea kuwashukuru wananchi wa Mkoa huu kutokana na ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa jeshi hilo.

Comments

Popular posts from this blog