JK ABEBESHWA ZIGO LA MAWAZIRI DHAIFU
- Get link
- X
- Other Apps
Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kimemtupia mpira Rais Jakaya Kikwete wa kuamua hatima
ya mawaziri saba, wanaotuhumiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.
Mawaziri
hao waliotajwa ni ‘mzigo’ kwa Serikali juzi walihojiwa na Kamati Kuu ya
Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake Rais Kikwete, ambapo
jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema
wamemshauri Rais Kikwete mambo matatu; kuwafukuza, kuwahamisha wizara au
kuwahimiza wafanye kazi.
“Kamati
Kuu imetoa maazimio saba ambayo yote yanazihusu wizara saba
zinazoongozwa na mawaziri hao. Tumemshauri Rais Kikwete, yeye ndiye
ataamua nini cha kufanya kwa sababu ndiye aliyewateuwa mawaziri hao,”
alisema Nape.
Wakiwa
Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma katika ziara ya chama hicho, Nape
pamoja na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana aliwatupia
lawama mawaziri hao wakati wakielezea changamoto zinazowakabili wakulima
ambao ni asilimia 80 ya Watanzania, huku mawaziri husika wakikaa kimya.
Nape
alisema mawaziri hao waliitwa kuhojiwa na kutakiwa kutoa maelezo ya
masuala yaliyoibuliwa wakati wa ziara hiyo ambayo pia iliwahusisha
baadhi ya wajumbe wa Sekretarieti.
Katika
maelezo yake kwa waandishi wa habari jana, Nape aliwataja mawaziri hao
kuwa ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa,
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Christopher Chiza, Naibu Waziri wa
Fedha Saada Mkuya (alihojiwa kwa niaba ya Waziri wa Fedha Dk William
Mgimwa).
Wengine
ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda, Waziri wa
Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk Mathayo David, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Hawa Ghasia.
Sakata la
kutaka mawaziri ‘mizigo’ kutoswa limekuwa likiibuliwa na wabunge
mbalimbali katika mikutano ya Bunge mjini Dodoma, huku baadhi
wakipendekeza hata Waziri Mkuu, Mizengo Pinda naye atoswe kutokana na
kushindwa kuwasimamia mawaziri.
Ushauri wa CCM kwa JK
Nape
alisema kuwa kazi ya Kamati Kuu ni kushauri, “Kazi yetu ni kushauri na
siyo kufukuza. Rais Kikwete ndiye amewateua mawaziri hao, ameupokea
ushauri na yeye ndiye mwenye uwezo wa kuwafukuza, kuwahamisha au
kuwasukuma watende kazi. Hiyo siyo kazi yetu”
Alipobanwa
zaidi kueleza ushauri ambao Kamati Kuu ilimpa Rais Kikwete Nape
alisema, “Kuna ushauri mwingine ambao tumempa Rais Kikwete hatuwezi
kuuweka hadharani.”
Alisema
kuwa wakati wa kuhojiwa kila waziri alikuja na majibu yanayoihusu wizara
yake kutokana na udhaifu ulioelezwa na wananchi.
“Katika
kikao kijacho cha Kamati Kuu moja ya mambo yatakayojadiliwa ni pamoja na
kuangalia utekelezaji wa mambo saba tuliyoishauri Serikali kupitia hizo
wizara saba,” alisema.
Nape
alisema kuwa walipoeleza udhaifu wa mawaziri hao hawakueleza kuwa ni
mzigo kwa Serikali, bali walilenga kueleza upungufu wao katika kusimamia
masuala mbalimbali.
“Mfano
Waziri wa Kilimo kwa miaka minne hajawahi kwenda mkoani Ruvuma ambako
kuna ghala la chakula pia hajawahi kushughulikia matatizo yanayowakabili
wakulima wa korosho na mahindi,” alisema.
Hata
hivyo, Nape alisema kuwafukuza mawaziri siyo dawa na kuweka mambo sawa
kwa maelezo kuwa wakati mwingine utendaji kazi ndani ya Serikali
unakwenda ovyo kwa sababu ya mfumo na sheria mbovu.
“Watu wanadhani ushauri tuliompa Rais Kikwete ni kuwafukuza mawaziri, wakati mwingine kufukuza siyo mwisho wa suluhisho.
Kwa
mfano tumebadili mawaziri Tamisemi lakini kila mwaka ripoti ya Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inaonyesha udhaifu katika
wizara hiyo,” alisema Nape.
Maagizo
Nape
alisema agizo la kwanza ni kuhusu kilimo cha pamba ambapo Kamati Kuu
iangalie upya Serikali ipitie upya upatikanaji wa pembejeo za ruzuku kwa
wakulima wa pamba nchini.
Alisema
kuwa kuhusu kilimo cha mkataba kwa wakulima wa pamba, Serikali imetakiwa
kuratibu utaratibu wa kilimo hicho ikiwamo kutowalazimisha.
“Kwa
mfano Waziri husika hajafika kwa muda wa miaka minne na nusu mkoani
Ruvuma ambako ndiko kuna ghala la chakula na tulipofika Tunduma tulikuta
foleni pale mizani huku watumishi wakiwa wanafanya kazi kwa saa tisa,
lakini baada ya kueleza udhaifu huo sasa wanafanya kwa saa 24,” alisema.
Aliongeza,
“Chama kimeiagiza serikali kutowalazimisha wakulima kutumia mbegu ya
Quiton, badala yake elimu itumike zaidi badala ya nguvu.”
Alisisitiza
kuwa Kamati Kuu imeitaka Serikali kuangalia upya urasimu katika
uwekezaji wa viwanda nchini, hasa vinavyoongeza thamani ya mazao na
kutoa ajira.
Kwa
upande wa wakulima wa korosho, Nape alisema kuwa Kamati Kuu
imeisisitizia serikali kujipanga kutatua tatizo la korosho na
kuhakikisha inabanguliwa nchini.
“Serikali
inatakiwa kuangalia upya orodha ndefu ya makato kwa wakulima hasa wa
korosho na vyama vya msingi au mamlaka zinginezo, ili kuondoa makato
yasiyo ya lazima na kuongeza kipato cha mkulima,”
“Kuhusu
pembejeo za ruzuku Kamati Kuu imepokea taarifa ya malalamiko ya wakulima
juu ya ufanyaji kazi wa mbolea ya Minjingu na kuagiza wananchi wawe
huru kutumia mbolea wanayoitaka badala ya kulazimishwa,” alisema.
Kwa
upande wakulima wa mahindi alisema kuwa serikali imetakiwa kumalizia
malipo yaliyobaki na kuhakikisha wanakomesha utaratibu wa kuwakopa
wananchi mazao yao bila kuwalipa.
“Utaratibu
uwekwe wa kufanya tathmini mapema ya mahitaji na uwezo wa kununua
mahindi wa serikali ili kuepusha utaratibu wa kuchukua mahindi ya
wakulima bila kuwalipa,”alisema.
Nnauye
alisema kwa upande wa madai ya walimu Kamati Kuu imeiagiza Serikali
kukamilisha uhakiki wa madai ya walimu na kuwalipa haki zao ikiwamo
kuhakikisha madeni hayazaliwi tena.
Kamati hiyo pia imekemea watendaji wachache wanaojihusisha na ubadhirifu kwenye halmashauri mbalimbali nchini.
“Serikali
imeshauriwa kuangalia upya sheria kama zinakidhi mahitaji ya wakati na
mazingira ya sasa ili kuongeza uwezo wa udhibiti na kuokoa pesa za
walipakodi zinazopotea kwa walafi wachache kwenye halmashauri mbalimbali
nchini,” alisema Nnauye.
Kwa
upande wa matatizo ya upatikanaji wa maji safi na salama serikali
imeagizwa kufanya mkakati wa makusudi na wa dharura kulitafutia ufumbuzi
wa haraka na wa kudumu tatizo hilo ikiwamo kuangalia upya utaratibu
uliotumika kuwamilikisha watu wachache maeneo makubwa ya ardhi, ambao
wameshindwa kuyaendeleza badala yake wanayatumia kuwakodishia wakulima
wadogo.
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment