Daktari bingwa wa upasuaji aliyepooza viungo

Pichani Dk Ted Rummel akiwa katika chumba cha upasuaji akiwahudumia wagonjwa Picha na AFP
Watu wengi hususani katika jamii za Kiafrika wamekuwa na mtazamo kuwa mtu mwenye ulemavu hawezi kufanya kitu chochote, ambacho kinaweza kuwa na manufaa katika jamii.
Hali hii inachangia kwa kiasi kikubwa walemavu wengi kuishi katika umaskini, huku hata baadhi yao wakiamini kuwa hakuna mchango wowote wanaoweza kuutoa katika jamii, matokeo yake ni kuishia kuombaomba barabarani.
Hata hivyo kwa wenzetu wa mataifa yaliyoendelea ulemavu siyo sababu ya kumfanya mtu ashindwe kufanya shughuli za kijamii au kutoa huduma pale inapohitajika, tena kwa usahihi zaidi wakati mwingine kuliko hata mtu asiyekuwa na ulemavu.
Hilo limedhihirishwa na Ted Rummel raia wa Uingereza ambaye licha ya kupooza mwili wake mpaka kufikia hatua ya kutembelea baiskeli ya wagonjwa, lakini bado ni daktari tegemezi kwenye idara ya upasuaji katika hospitali za Progress West na Barnes Jewish St Peters nchini humo.
Daktari huyo ambaye amepooza kuanzia kiunoni mpaka miguuni, ameonyesha kuwa taaluma yake haiwezi kupotea kwa sababu ya ulemavu, alioupata ukubwani hivyo kuamua kuendelea na kazi hiyo katika mazingira magumu.
Licha ya kuishi katika hali ya kupooza kwa muda wa miaka mitatu sasa, Rummel anamudu kuhudumia wagonjwa na kuwafanyia upasuaji ilhali akiwa kwenye kigari maalumu.
Hali ya kupooza mwili haijapunguza ufanisi wa kazi ya Rummel, kwani licha ya kukumbana na changamoto ya kushindwa kusogeza miguu bado ana uwezo mkubwa katika kufanya upasuaji.
Hali hiyo ilivyoanza
Tofauti na watu wengi Rummel alizaliwa mzima kabisa lakini mwaka 2009 akaanza kupatwa na maumivu katika nyonga zake, ingawa hakufikiria kuwa hali hiyo ingeendelea kumsumbua kwa muda mrefu.
Katika mahojiano yake na gazeti la Daily Mail la Uingereza, Rummel anaeleza kuwa aliendelea kuishi na maumivu hayo mpaka Septemba 2010, ambapo ndipo hali ya kupooza ilipoanza rasmi na kujikuta mwili wake ukikosa mawasiliano. Ikamlazimu kuachana na kazi hiyo kwa muda ili apate matibabu na mapumziko ambayo yalichukua kipindi cha miaka miwili, licha ya kutibiwa viungo.
Muda wote aliokuwa katika matibabu Rummel alikuwa karibu sana na familia yake, pamoja na wafanyakazi wengine hali iliyompa faraja na kujikuta akitamani apone haraka ili aweze kurejea kwenye kazi yake.
"Wakati matatizo haya yananikuta nilikuwa tayari nina taaluma na elimu ya kutosha lakini najua wapo wengine ambao yanawakuta wakiwa katika hali mbaya zaidi, ndiyo maana nataka kutumia nguvu na taaluma yangu kuwasaidia," anasema Rummel na kuongeza;
"Nashukuru familia yangu hata wafanyakazi wenzangu walikuwa karibu na mimi na muda wote walinionyesha upendo, hapo ndipo nikafikiria na kujiapiza kuwa lazima nipone ili niweze kuwasaidia wengine."
Maisha mapya ya Dk Rummel
Anasema hata baada ya kubaini kuwa viungo vyake vimepooza akaona hakuna haja ya kuachana na taaluma yake ambayo ameifanya kwa muda mrefu na inasaidia kuokoa maisha ya watu wengi, hivyo mchango wake bado unaendelea kuhitajika.
"Kitu cha kwanza kukifikiria ilikuwa ni taaluma yangu na namna ambavyo watu wengi wangekosa huduma yangu, hivyo nikaamua nitajitahidi kwa namna yoyote ile nirudi kwa mara nyingine katika chumba cha upasuaji," anasema Rummel.
Hatimaye dhamira yake ilitimia akarudi hospitali na upasuaji wake wa kwanza aliufanya chini ya uangalizi wa daktari mwingine, ambaye alikuwepo katika chumba cha upasuaji kumsaidia endapo angehitaji msaada lakini alifanikiwa kufanya upasuaji huo bila kuhitaji msaada.
Kabla ya kupata maradhi hayo Dk Rummel alikuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa 60 kwa siku na kufanikiwa kuwashughulikia wagonjwa wasiopungua 1,000 kwa mwaka, hali iliyosababisha pengo lake kuonekana kipindi chote alichokuwa katika mapumziko ya matibabu.
Anakiri kuwa anakumbana na changamoto mbalimbali wakati wa kufanya upasuaji akiwa katika hali hiyo, kutokana na kushindwa kusimama na kumudu kumzunguka mgonjwa wakati wa upasuaji kama ilivyokuwa awali.
Sasa hivi analazimika kufanya upasuaji akiwa amekaa kwenye kiti cha umeme, ambacho humsaidia kunyanyuka na kumzunguka katika eneo analolifanyia upasuaji.
Kwa upande mwingine Rummel anasema kuwa hali hiyo imemfanya kuwa karibu sana na wagonjwa na kujua hali zao na namna ambavyo wanajisikia wakiwa katika maumivu.
"Sasa hivi namwelewa sana mgonjwa najiweka katika nafasi yake na kuhisi ambavyo anajisikia, hivyo inakuwa rahisi kumpatia matibabu sahihi," anasema.

Comments

Popular posts from this blog