ANGALIA PICHA YA MSAIDIZI WA RAIS KWA MAREKANI BARACK OBAMA ALIYEKULIA TANZANIA
- Get link
- X
- Other Apps
WAKATI
anaingia madarakani rasmi Januari 20, mwaka 2009 kuiongoza Marekani,
nchi kubwa yenye nguvu za kiuchumi na kisiasa duniani, Barack Obama
alikuwa na malengo mengi. Mojawapo ni kuzidi kuipaisha Marekani na
kuwasuta waliodhani nchi hiyo haiwezi kuongozwa na mtu mweusi.
Itakumbukwa
kwamba, Obama mwenye asili ya Kenya ambaye kwa sasa ni Rais wa 44 wa
Marekani, ndiye mtu wa kwanza mwenye asili ya Afrika kuwahi kuiongoza
Marekani.
Hivyo,
katika kuhakikisha anatimiza ndoto zake, alipanga safu imara ya
wasaidizi, miongoni mwao aliibuka kijana mdogo aliyekuwa na umri wa
miaka 35 tu, lakini aliyekuwa na kichwa adimu katika utundu wa kazi,
hasa kwa upande wa teknolojia.
Huyu si
mwingine bali ni Vivek Kundra aliyezaliwa huko New Delhi, India. Huyu
alipewa jukumu la kuwa Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano katika Serikali ya Marekani. Kundra, ingawa ana asili ya
India, ni ‘Mswahili’ anayeijua vyema Tanzania, kwani amekulia Tanzania.
Historia
yake inaonesha kuwa, akiwa na umri wa mwaka mmoja tu, yeye na wazazi
wake, walihamia Afrika, katika nchi ya Tanzania. Baba yake alikuwa
miongoni mwa maprofesa na walimu waliokuja nchini kufundisha katika
shule kadhaa.
Kutokana
na mpango huo, Kundra alijikuta akiishi na wazazi wake huko Korogwe,
Tanga na pia mkoani Dodoma. Ni huko ndiko alikozama katika Kiswahili,
akiifanya lugha yake ya kwanza huku Kihindi na Kiingereza zikiwa lugha
za ziada kwake.
Aliishi Tanzania hadi alipofikisha umri wa miaka 11 ambapo wazazi wake walihamia Washington D.C, Marekani.
“Kwa hiyo
ninaijua vizuri Tanzania na ninakifahamu vizuri Kiswahili,” anasema
Kundra ambaye akiwa Marekani, alihitimu Shahada ya Kwanza katika
Saikolojia aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Maryland Park.
Hakuishia
hapo, alirudi tena darasani kusoma Teknolojia ya Habari katika Chuo
Kikuu cha Maryland, lakini pia alisoma katika Taasisi ya Uongozi wa
Siasa ya Sorensin ya Chuo Kikuu cha Virginia.
Kutokana
na umahiri wake kitaaluma, Machi mwaka 2011 alitangazwa kuwa mmoja wa
waliothibitisha vipaji vya uongozi duniani, akichaguliwa na jopo la
wajuzi na wasomi kutoka Mkutano wa Uchumi Duniani (WEF).
Mwaka
huo, katika mkutano uliofanyika Amman, Jordan, Kundra alikuwa mwenye
furaha kukutana na kijana mwingine aliyepewa heshima kama yake, Susan
Mashibe wa Tanzania ‘milionea mtoto’ ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na
Mwanzilishi wa Kampuni ya TanJet, kampuni ya kimataifa na ya kwanza ya
aina yake nchini inayoshughulikia masuala ya kiufundi katika ndege
binafsi, za biashara na hata za kidiplomasia.
Mwanadada
huyu, pia anamiliki kampuni nyingine inayojulikana kama Kilimanjaro
Aviation Logistic Center, ambayo inashughulikia taratibu za utuaji na
urukaji wa ndege binafsi katika Bara la Afrika.
Aidha,
ameanzisha Huduma ya Matengenezo na Ukarabati wa Ndege Kilimanjaro, kwa
lengo la kutoa huduma za kisasa, yenye kiwango na salama katika usafiri
wa anga wa jumla na ushirika katika eneo la Afrika. Lakini pia Susan
ndiye Mwanamke wa Kwanza Afrika Mashariki mwenye Cheti cha Rubani cha
FAA na Mhandisi Matengenezo wa Ndege.
Tangu
kuanzishwa TanJet mwaka 2003, Mashibe ametunukiwa Tuzo mbalimbali
ikiwemo ya Askofu Desmond Tutu ya mwaka 2009 na ile ya Mwanamke
Mjasiriamali mwenye Mafanikio ya mwaka 2009.
Tukirudi
kwa Kundra, mwaka mmoja kabla ya tuzo ya WEF, alituzwa na taasisi ya
teknolojia ya SANS kwa kuwezesha kufichua wizi wa dola za Marekani
milioni 300 (Sh bilioni 450) uliokuwa unafanywa kwa njia ya mtandao kwa
takribani kila mwaka na baadhi ya watendaji serikalini.
Aidha,
Kundra amewahi kutunukiwa Tuzo kemkem kutokana na umahiri wake katika
miundombinu ya teknolojia na habari na mawasiliano, akiwa amegundua
mifumo kadhaa ya kisasa. Ndiyo maana Chuo Kikuu cha Harvard hakikutaka
kuuachia ujuzi wake, na hivyo kuamua kuingia naye mkataba wa kufundisha
kwa mkataba chuoni hapo.
Nje ya
kazi hiyo, Kundra pia ni Makamu Mwenyekiti wa kampuni kubwa ya masomo ya
Salesforce ya Marekani. Majukumu mengine ya kitaaluma aliyokuwa nayo
kabla ya kuitwa Ikulu ya Marekani kumsaidia Rais Obama ni kuwa
Mkurugenzi wa Miundombinu ya Teknolojia huko Arlington, Virginia mwaka
2001 na miaka mitano baadaye, aliteuliwa na Gavana wa Virginia, Tim
Kaine kuwa mkuu wa shughuli za kiteknolojia jimboni humo.
Ilipofika Machi 27, 2007, Meya wa Columbia, Adrian Fenty alimteua Kundra kuwa Ofisa Teknolojia Mkuu wa Columbia.
Je,
anazungumziaje kuaminiwa kwake na Rais Obama? Anasema: “Ni heshima
kubwa. Sikuwaza kuwa msaidizi wa Rais katika nchi muhimu kama Marekani.
Kama unavyojua, nilizaliwa India, nikakulia Tanzania.
Ni mhamiaji tu hapa na ikumbukwe nilikuja Marekani mwaka 1985 nikiwa sijui hata Kiingereza, zaidi ya Kihindi na Kiswahili.
“Lakini
bidii katika masomo na nyanja ya utawala, vitu nilivyorithi kutoka kwa
wazazi wangu, ndivyo vilivyonifikisha hapa, kiasi cha kuaminika na jamii
na hata Rais wa nchi.Namshukuru Mungu kwa kila jema linalotendeka juu
yangu. Namshukuru Rais Obama kwa kuwapa nafasi vijana pia.”
Huyo
ndiye Vivek Kundra, mtaalamu wa teknolojia ya habari na mawasiliano
aliyekulia Tanzania, lakini sasa akifanya vitu vikubwa nchini Marekani.
Source: HabariLeo
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment