ZIARA YA RAIS KIKWETE WILAYANI MBOGWE, BARABARA YAPANDISHWA DARAJA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiweka jiwe la msingi kuashiria uzinduzi rasmi wa ujenzi wa barabara ya Bwanga – Uyovu yenye urefu wakilometa 45 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Geita.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete (aliyeshika mkasi) akikata utepe kuashiria uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Bwanga – Uyovu yenye urefu wa kilometa 45 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Geita. Kulia kwa Rais ni Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na kushoto kwa Rais ni Mbunge wa Bukombe Mhe. Kulikoyela Kahigi kutoka CHADEMA. Wengine ni baadhi ya Mawaziri na Viongozi wa Kitaifa na kutoka mkoa wa Geita waliokuwepo katika sherehe hizo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na Kiongozi wa Kikundi cha Mchelemchele kilichotumbuiza wakati wa sherehe za uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya Bwanga – Uyovu inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Geita.
Waziri wa Ujenzi Mhe. Dkt John Pombe Magufuli(aliyeshika kipaza sauti) akitoa taarifa kwa wananchi wa Iboya waliosimamisha msafara wa rais Kikwete alipokuwa kwenye ziara ya kikazi katika Wilaya ya Mbogwe, Mkoani Geita.
(Habari na picha kwa hisani ya Michuzi Blog)

Wananchi wa wilaya ya Mbogwe mkoani Geita wamenufaika kwa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kusikilizwa ombi lao ambapo barabara inayounganisha maeneo ya Masumbwe na Makao Makuu ya wilaya hiyo imepandishwa daraja na kuwa barabara ya mkoa. Awali barabara hiyo ilikuwa ikihudumuwa na wilaya lakini ikipatiwa matengenezo ambayo hayakidhi ongezeko la magari yanayotumia barabara hiyo kwa sasa.

Mheshimiwa Rais akiwa njiani kutokea mji wa Masumbwe kupitia makao makuu ya wilaya mpya ya Mbogwe kabla ya kuingia Geita alisimamishwa mara kadhaa na wananchi wanaoishi katika vijiji inakopita barabara hiyo ambao walitumia fursa hiyo kuwasilisha kero zao na hususan suala la barabara ambayo ilielezewa kutokidhi mahitaji halisi kwa wakazi hao na maeneo jirani.

Akijibu maombi ya wananchi hao, Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli alielezea kuwa barabara hiyo inayolalamikiwa kwa hivi sasa iko chini ya usimamizi wa wilaya husika. Hata hivyo, kwa kuzingatia umuhimu wa barabara husika na uchanga wa wilaya hiyo mpya, alikipokea kilio cha wananchi hao na kukubali barabara hiyo ipandishwe daraja na kuwa ya mkoa.

“Nitatumia mamlaka niliyopewa chini ya Sheriaya Mfuko wa Barabara Namba 13 ya mwaka 2007 kuipandisha barabara hii ambayo inaanzia Masumbwe kupitia Mbogwe, Nyikanga hadi Butengo Lumasa yenye urefu wa kilometa 81 kwamba itakuwa ya mkoa na hivyo kuwa chini ya usimamizi wa Tanroads” alisemaWaziri Magufuli.

Aidha, katika hatua nyingine Mheshimiwa Magufuli alibainisha kuwa katika mipango ya mwaka ujao wa fedha wa 2014/2015, wizara yake itaanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara inayotokea mji wa Katoro hadi Ushirombo yenye urefu wa kilometa 56 ili kuijenga kwa kiwango cha lami.

Naye Mbunge wa Mbogwe Mheshimiwa Augusto Manyanda Masele kwa upande wake alielezea kufurahishwa kwake na hatua hiyo na hasa katika kipindi hiki ambacho wilaya hiyo mpya inahitaji kuimarisha miundombinu mbalimbali kwa lengo la kuharakisha maendeleo katika eneo hilo.

“Hii imekuwa ni faraja kubwa kwa wana Mbogwe kwani suala la usafiri limekuwa ni kero ya muda mrefu, tunashukuru sana kwa kutembelewa na ugeni huu wa Kitaifa hapa mkoa ni kwetu” alisisitiza Mheshimiwa Masele

Comments

Popular posts from this blog