ZAIDI YA RAIA 479 WA TANZANIA WANATUMIKIA VIFUNGO NA WENGINE KUNYONGWA BAADA YA KUKUTWA NA HATIA KWA MAKOSA YA KUKUTWA NA MADAWA YA KULEVYA NJE YA NCHI IKIWEMO CHINA, BRAZIL NA HONG KONG.
- Get link
- X
- Other Apps
Haya ni maelezo binafsi ya Mheshimiwa Ester Amos Bulaya bungeni Dodoma November 4 2013 kuitaka serikali kufanya mabadiliko ya sheria ya dawa za kulevya na kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia wahalifu wa dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa
Kanuni ya 28(8) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la mwaka 2013,
napenda kutoa maelezo binafsi ya juu ya tatizo sugu la uagizaji, uuzaji
na usafirishaji wa dawa za kulevya linaloongezeka kwa kasi kubwa nchini,
lengo likiwa ni kuitaka serikali ifanye mabadiliko/marekebisho ya
sheria ya Dawa za kulevya na kuanzisha Mahakama Maalum kushughulikia
wahalifu wanaojihusisha na usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika,
Nimeona
ni wakati muafaka kutoa maelezo haya, ili Bunge lako tukufu na Serikali
ipate fursa ya kuona uzito wa tatizo hili kutokana na ukweli kwamba
katika miaka ya karibuni tatizo la dawa za kulevya katika nchi yetu
limeongezeka kwa kasi ya ajabu hali inayopelekea athari kubwa za
kiuchumi, kijamii na kiafya. Na mbaya zaidi kundi kubwa linaloathirika
ni kundi la vijana, ambao ndio nguvu kazi ya Taifa letu.
Na
mbaya zaidi sasa hivi, wafanya biashara hawa wa dawa hizi haramu
wameanza kuwatumia watoto wa shule za msingi chini ya falsafa yao mpya
“wapate wakiwa wadogo…wafanye watumwa wa dawa za kulevya… na kupata
uhakika wa soko la baadae pale ambapo watakuwa wameajiriwa au
wamejiajiri”.
Mheshimiwa Spika,
Tafiti
za hivi karibuni za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kwamba kuna ongezeko
kubwa na la kutisha katika matumizi ya dawa za kulevya aina ya heroin na
kwa njia ya kujidunga katika nchi za Kenya, Libya, Mauritius,
Shelisheli na Tanzania.
Halikadhalika,
Ripoti ya mpya ya hivi karibuni ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya
kupambana na mihadarati na uhalifu (UNODC) imetamka bayana kwamba
Tanzania ni kinara wa kupitisha dawa za kulevya katika nchi za Afrika
Mashariki, na Mkoa wa Tanga ukitajwa kama mkoa hatari zaidi!
Mheshimiwa Spika,
Ripoti
hiyo inasema jumla ya Tani 64 za dawa za kulevya aina ya Heroin
ilisafirishwa bila kukamatwa kwenda au kupitia Afrika Mashariki ikiwamo
Tanzania kati ya 2010 na 2013.
Na
kwa Mkoa wa Tanga, ambao umetajwa wazi kama eneo hatari zaidi Afrika
Mashariki wastani wa ukamataji wa shehena za dawa za kulevya eneo hilo
umefikia KG 1,011 mwaka 2013 toka KG 145 mwaka 2010. Na kwamba Dola za
Kimarekani takriban milioni 160 zinatumiwa na Watanzania na wakenya kila
mwaka kwa utumiaji na usafirishaji kwa mwaka!Hili sio jambo la kufumbia
macho, lazima tuchukue hatua sasa.
Mheshimiwa Spika,
Lazima
tuchukue hatua sasa, kwa sababu kama nilivyoainisha hapo juu kwamba kwa
kipindi cha miaka mitatu tu (2010-2013), wakati Tani 64 za dawa za
kulevya zilipita bila kukamatwa…zikiwa mtaani zikiharibu vijana na
watoto wetu katika kipindi hicho hicho, kiasi kilichoweza kukamatwa ni
tani 1.6 tu! Takwimu hizo za kutisha zinatoa picha kwamba sehemu kubwa
ya shehena za dawa za kulevya hupitishwa bila kugundulika au kukamatwa
na vyombo vya dola!
TASWIRA YA NCHI KATIKA JUMUIYA YA KIMATAIFA
Mheshimiwa Spika,
Maelfu
ya watanzania wanatumikia vifungo mbali mbali ikiwamo vifungo vya
maisha nje ya nchi, wengine wengi wamepoteza maisha kwa kunyongwa.
Nitatoa mifano michache; China peke yake inasemekana kuna wafungwa 176
(99% – dawa za kulevya) , Brazil kuna wafungwa zaidi ya 103 na Hong Kong
kuna zaidi ya watanzania 200 wenye kesi za dawa za kulevya, ambapo 130
zimeshakwisha hukumiwa na kesi 70 zikiwa zinaendelea!
Mheshimiwa Spika,
Aibu
ya hivi karibuni, ambayo hatuwezi kuikwepa ni meli iliyosajiliwa
Tanzania (upande wa Zanzibar- MV Gold Star ) iliyoripotiwa kukamatwa
nchini Italia ikiwa imesheheni tani 30 za dawa za kulevya zenye thamani
ya pauni milioni 50 ( sawa na bilioni 123 za Kitanzania).
Mheshimiwa
Spika, uhalifu huu, unaofanywa na mtandao huu wa watu wachache, lakini
wenye nguvu umewafanya watanzania wanaokwenda nje ya nchi kudhalilika
kutokana na upekuzi unaofanywa dhidi yao kwa hofu kwamba yawezekana na
wao wamebeba dawa hizo haramu.
HALI YA DAWA ZA KULEVYA
Mheshimiwa Spika,
Changamoto
ya dawa za kulevya sio tatizo letu peke yetu ni tatizo ambalo hata
Jumuiya ya kimataifa imekuwa ikipambana nalo kwa kipindi kirefu kwani
tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 5 ya idadi ya watu wazima duniani
(watu takribani milioni 230) wanakadiriwa kutumia dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika,
Tukiwa
sehemu ya Jumuiya hii ya Kimataifa, Waheshimiwa Wabunge mtakumbuka kuwa
tarehe 19 Desember, 1988 Jumuia ya Kimataifa ilipitisha Mkataba wa
kupambana na dawa za kulevya yaani United Nations Convention Against
Illicit Traffic in Narcotic Drugs and Psychotropic Substances. Tanzania
ni sehemu ya Mkataba huo na hili limewekwa wazi hata kwenye kifungu cha
55 cha Sheria ya kuzuia dawa za kulevya [sura 95 ya sheria zetu kama
zilivyorekebishwa mwaka 2002].
Mkataba
wa mwaka 1988 ulikuwa unakazia zaidi Mkataba wa mwaka 1961 (Single
Convention on Narcotic Drugs, 1961), Itifaki (Protocol) za 1972
zilizofanyia marekebisho Mkataba wa mwaka 1971 (Convention on
Psychotropic Substances, 1971). Licha ya juhudi zote, tatizo la uuzaji
na usafirishaji wa dawa za kulevya, limezidi kuwa kubwa.
HALI YA DAWA ZA KULEVYA NCHINI NA MADHARA KWA AFYA YA BINADAMU
Mheshimiwa Spika,
Mwaka
1995 tulitunga Sheria ya kuzuia biashara ya dawa za kulevya ambayo
ilianza kufanya kazi mwaka 1996 kupitia GN.No.10/1996. Sheria hiyo
inatumika Bara na Zanzibar. Kabla ya Sheria hiyo tulikuwa tuna Sheria
iitwayo the Dangerous Drugs Ordinance (Cap.95).
Pamoja
na kutungwa kwa Sheria mpya, tatizo la dawa za kulevya limeendelea kuwa
kubwa zaidi hapa nchini. Ukamataji wa dawa za kulevya kwa miaka ya
nyuma ilikuwa kidogo na idadi ya walioathirika (mateja) ilikuwa ni ndogo
kulinganisha na sasa hivi.
Mheshimiwa Spika,
Ni
kwa bahati mbaya sana, licha ya ukubwa wa tatizo, pamoja na athari zake
kwa jamii ya Watanzania, hakuna tafiti zinazoonyesha ukubwa wa tatizo
kwa Nchi nzima, tafiti nyingi zilizofanywa zimejikita katika maeneo
machache yaliyoathirika zaidi na dawa za kulevya .
Tafiti
zinaonyesha kwamba Dawa zinazotumika kwa wingi ni bangi, mirungi,
heroine, mihadarati, vidonge na cocaine.Tafiti iliyofanywa na Shirika la
Umoja wa Mataifa linalohusika na mapambano dhidi ya dawa za kulevya
UNODC (United Nations Office on Drugs and Crime) zinaonyesha kwamba 0.2%
ya Watanzania, ambao ni karibia watu milioni 1.2 wameshawahi kutumia
dawa za kulevya aina ya heroine.
Mheshimiwa Spika,
Halikadhalika
Shirika la afya duniani (World Health Organisation -WHO) inaripoti kuwa
takribani 0.2% ya Watanzania wameathirika na Ugonjwa wa TB na takwimu
za kitaifa katika program ya Kifua Kikuu na Ukoma Tanzania zinaonyesha
maambukizi ya TB ni 0.4% wakati tafiti katika hospitali ya Taifa ya
Muhimbili inaonyesha kwamba maambukizi ya TB kwa wanaotumia dawa za
kulevya ni 11% ambayo ni mara 44 zaidi ya kiwango cha maambukizi kwa
watu ambao hawatumii dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika,
Kwa
upande wa maambukizi ya UKIMWI takwimu za mwaka 2011/2012 za TACAIDS
zinaonyesha kwamba 5.1% ya Watanzania wameathirika na virusi vya UKIMWI
wakati tafiti ndogondogo zinaonyesha maambukizi ya virusi ya ukimwi kwa
watu wanaotumia dawa za kulevya ni mara 10 zaidi ya maambukizi ya
kawaida. Kwa mfano 51.9% ya wanaotumia dawa za kulevya kwa njia
kujidunga sindano, 37% wanaotumia dawa za kulevya kwa njia ya kuvuta na
kufanya biashara ya ngono na 22.6% kwa wanaotumia dawa za kulevya kwa
njia ya kuvuta.
Mheshimiwa Spika,
Madhara
ya kiafya kwa utumiaji wa dawa za kulevya sio tu katika magonjwa ya TB
na maambukizi ya virusi vya ukimwi, bali pia katika homa ya ini.
Japokuwa hakuna tafiti za kitaifa zilizofanyika kuhusiana na mchango wa
matumizi ya dawa katika homa ya ini, tafiti ndogondogo za mwaka 2012
zinaonyesha kati ya 65% mpaka 75.6% ya watumiaji wa dawa za kulevya
wameathirika kwa homa ya Ini, hasa homa ya ini aina ya Hepatitis. Homa
ya ini ni hatari sana katika kupata magonjwa sugu ya ini ikiwepo kansa
ya ini na ini kushindwa kufanya kazi.
UKUBWA WA TATIZO NA UTENDAJI WA VYOMBO VYA DOLA
Kesi
kubwa ya kwanza inayohusu dawa za kulevya ni ile ya mfanyabiashara
NURDIN AKASHA @HABAB V.R [1995] TLR. 227 (CAT) ambaye tarehe 20/7/1993
alikamatwa nyumbani kwake Msasani village akiwa na paketi 105 za
menthaqualone (mandrax) alizo ziingiza nchini kutoka Mombasa akitumia
malori yake. Sasa hivi tunaongelea uingizaji wa kilo kadhaa za dawa za
kulevya na siyo paketi tena.
Mwezi
Machi, 2010 kilo 92 za dawa za kulevya aina ya Heroine zilikamatwa
maeneo ya Kabuku Mkoani Tanga na tayari washitakiwa 5 wanatumikia
kifungo. Tarehe 19/12/2010 kilo 50 za dawa za kulevya aina ya Heroini
zilikamatwa tena wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.
Mwezi
Septemba, 2011 kilo 179 za dawa za kulevya aina ya Heroini zilikamatwa
Dar es salaam, tarehe 14/6/2011 Kilo 35 za dawa za kulevya aina ya
Heroine zilikamatwa mkoani Mbeya na tarehe Januari kilo 211 za dawa za
kulevya zilikamatwa mkoani Lindi.
UTENDAJI WA OFISI YA DPP
Natambua
jitihada zinazofanywa na baadhi ya watendaji wa Serikali ya awamu ya
nne katika vyombo vya dola kwa kufanikisha jitihada za kuwakamata
watuhumiwa wanaojihusisha na dawa za kulevya. Kutokana na jitihada hizo,
kuanzia mwaka 2008 mpaka mwaka huu wa 2013 watuhumiwa wa dawa za
kulevya ni kama ifutavyo:-
i) Cocaine kilo 395 zilikamatwa na washitakiwa waliokamatwa ni 1074
ii) Heroini kilo 768.8 na washitakiwa waliokamatwa ni 1130,
iii) Mirungi kilo 56,562 na washitakiwa waliokamatwa ni 3,712,
iv) Bangi kilo 487,472 sawa na tani 487 na washitakiwa waliokamatwa ni 20,255
v) Mandrax kilo 5 na gramu 9 na washitakiwa waliokamatwa ni 20.
Licha
ya juhudi za baadhi ya watendaji waaminifu kuwakamata watu walioko
katika mtandao huu hatari kumekuwa na hujuma za dhahiri dhidi ya
wanaopambana na dawa za kulevya. Moja kati ya ofisi inayoshutumiwa kuwa
na maafisa wanaoshirikiana na wanamtandao, ni ofisi ya DPP
MTANDAO KATIKA OFISI YA DPP NA MAHAKAMA
Natambua
kazi nzuri na jitihada zinazofanywa na baadhi ya watumishi wazalendo
kwa upande kwa Ofisi ya Muendesha Mashtaka, Majaji na Mahakimu
waaminifu.
Lakini
katika ofisi hizo za umma, kumekuwa na baadhi ya watumishi ambao
wamekuwa wakihujumu kesi za dawa za kulevya kwa kushirikiana na
watuhumiwa katika kupanga jinsi ya kuwasaidia washinde kesi kwa
kuwapatia taarifa za siri zinazohusiana na ushaidi na jinsi ya kuharibu
ushahidi nzima.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana
na kupanuka kwa mtandao huu wa kuhujumu, licha ya kushirikiana na
washitakiwa, mtandao uliopo katika Ofisi hiyo ya DPP umekuwa ukituhumiwa
kufanya njama za kushirikiana na baadhi ya watumishi wa mahakama hasa
Majaji kuhamisha kesi kupeleka kwa Majaji ambao wanadaiwa kuhusika na
mtandao huu (sihitaji kutaja majina ya Majaji hapa, baadhi yao
wanafamika na wengine wametajwa mara kadhaa na vyombo vya habari).
Mheshimiwa Spika,
Kwa
kutumia mtandao huo, baadhi ya Majaji wamekuwa wanatafsiri sheria kwa
jinsi wanavyotaka na kuwapa dhamana watuhumiwa wa kesi za dawa za
kulevya ambazo hazina dhamana. Mfano mzuri ni kesi Na.6/2011, Jamhuri
dhidi ya Fred William Chonde na wenzake ambao walikutwa na kilo 179 za
Heroine yenye thamani ya shilingi Bilioni 6.5.
Washitakiwa
hawa wanashitakiwa kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya ambalo kwa
mujibu wa kifungu cha 148(5)(a)(ii) cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya
Jinai pamoja na kifungu cha 27(1)(a) cha Sheria ya Kuzuia usafirishaji
wa dawa za kulevya halina dhamana.
Kwa
tafasiri yoyote ile aliyokuwa nayo mheshimiwa Jaji, bado asingewapa
dhamana kwani kifungu cha 148(5)(a)(iii) cha sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai na kifungu cha 27(1)(b) cha Sheria ya Kuzuia
usafirishaji wa dawa za kulevya kinazuia dhamana kwa kosa ambalo thamani
ya dawa za kulevya inazidi shilingi milioni kumi.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana
na Mahakama kutoa dhamana, washitakiwa wawili raia ya Pakistani
wametoroka na hawapo tena nchini. Aidha, katika kesi ya R. v. Mwinyi
Rashid Ismail @Mkoko, (KLR /IR 4143/2011), mshitakiwa aliomba dhamana
Mahakama Kuu wakati kesi ilikuwa bado ipo Mahakama ya Kisutu ndipo
wakili wa Serikali akamwambia jaji kuwa anaomba kuifuta.
Mheshimiwa
Jaji huku akifahamu kuwa kesi hiyo imefika mbele yake kwa ajili ya
kusikiliza maombi ya dhamana tu, na kuwa ilikuwa haijafikishwa Mahakama
Kuu kwa taratibu wa sheria, aliamua kumfutia kesi mshitakiwa na kuamuru
kuwa yuko huru. Sambamba na hilo, katika kesi No.
794/2011
katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala Mheshimiwa Hakimu aliwafunga kifungo
cha nje kwa miezi kumi na tano washikiwa Abdurahman Shaban Sindanema,
said Nassoro Khamis na Abdurahim Haroub Said waliokiri kosa la kuuza na
kusambaza dawa za kulevya aina ya Heroini.
Mheshimiwa Spika,
Adhabu
iliyotolewa na Hakimu huyu, haipo kwa mujibu wa sheria. Kwa mujibu wa
kifungu cha 16 cha Sheria ya kuzuia dawa za kulevya, adhabu iliyowekwa
kwa wauzaji au wasambazaji wa dawa za kulevya ni kifungo cha maisha na
si chini ya miaka ishirini (20) jela kwa kipindi hicho.
Kesi
nyingine ni Na. 274/2005 Jamhuri dhidi ya Yusuph Hashim Nyose
aliyekamatwa na kilo 1.3 za dawa za kulevya aina ya Heroine alizokuwa
amemeza na kisha kuzitoa kupitia njia ya haja kubwa baada ya kukamatwa
na zilikuwa na thamani ya shilingi milioni kumi na mbili na laki sita
(12,600,000/=).
Pamoja
na ushahidi uliotolewa mahakamani na mashahidi sita(6) wa upande wa
Jamhuri ikiwa ni pamoja na mkemia aliyethibitisha kuwa ni dawa za
kulevya na mashahidi walioshuhudia mshitakiwa akizitoa kwa njia ya haja
kubwa, Hakimu alimuachilia huru.
Mheshimiwa Spika
Katika
hukumu yake Hakimu alisema kuwa ameridhika kuwa hizo ni dawa za kulevya
na zina madhara kwa binadamu na kuwa hana ubishi kuwa mshitakiwa
alikutwa nazo. Hata hivyo alimuachilia huru kwa kuwa upande wa mashtaka
umeshindwa kuelezea mbinu walizotumia kumgundua mshitakiwa kuwa alikuwa
amebeba dawa za kulevya kabla ya kumkamata.
Mfano
mwingine ni hukumu iliyotolewa tarehe 4/5/2007 inayoihusisha Jamhuri
dhidi ya Chriswell Simon Mobini (561/2007) ambapo mtuhumiwa alikamatwa
tarehe 9/4/2007 katika uwanja wa JKNA akiwa na pipi 93 aina ya heroine
yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 30 za kitanzania. Baada ya
kufikishwa Mahakama ya Kisutu na kufunguliwa mashtaka chini ya kifungu
16 (1) (b) (i) cha dawa za kulevya.
Mheshimiwa Spika,
Katika
shauri hili, Hakimu alimwachia huru baada ya mshtakiwa kulipa faini ya
shilingi milioni 1 za kitanzania kwa maelezo kwamba kwa kumtazama tu
mtuhumiwa, anaonekana ni mgonjwa wa vidonda vya tumbo na hivyo hawezi
kupata huduma nzuri iwapo atapelekwa rumande! Hii ni mifano michache tu
kati ya mingi iliyopo!
KESI ZILIZOKO MAHAKAMANI
Mheshimiwa Spika,
Kama
nilivyoainisha hapo juu, na ili kuonyesha msisitizo naomba nirejee
takwimu husika kama ifuatavyo, kwamba kati ya watuhumiwa 26,191
waliokamatwa mpaka sasa kuna jumla ya kesi 89 tu zinazosubiri
kusikilizwa Mahakamani.
Katika
vikao vya Mahakama Kuu vilivyokaa kuanzia mwezi Augosti hadi Octoba,
2013 hakuna kesi hata moja ya dawa za kulevya iliyosikilizwa na kutolewa
hukumu, japo zilikuwa zimepangwa.
DHANA YA UHURU WA MAHAKAMA
Mheshimiwa Spika,
Natambua kuwa Mahakama ni muhimili unaojitegemea katika kutenda shughuli zake na iko huru.
Natambua
pia kuwa Bunge haliwezi kuingilia shughuli za Serikali au Mahakama.
Lakini pamoja na uhuru huo, Bunge hili limekuwa linakosoa Serikali pale
linapoona imekosea. Kwa ujumla lazima kuwe na checks and balance. Pamoja
na mapungufu niliyoelezea hapo juu kuhusiana na mwendendo wa Mahakama
katika kusikiliza kesi za dawa za kulevya, Mahakama imekuwa inafanya
kazi zake bila kukosolewa na chombo kingine na ndiyo maana baadhi
wamekuwa wakitumia dhana ya uhuru wa Mahakama vibaya.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana
na matumizi mabaya ya uhuru wa Mahakama kwa baadhi ya watumishi wa
Mahakama, ni mapendekezo yangu kwamba Serikali iunde tume maalumu ya
kiuchunguzi kuchunguza mwenendo wa kesi hizi za dawa za kulevya ili
watakao bainika kuwa wametumia nafasi /wadhifa/ madaraka yao vibaya
wachukuliwe hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuvuliwa madaraka
waliyonayo.
Kwa
kufanya hivyo, itaonyesha kuwa hakuna aliye juu ya sheria. Na itakuwa
ni fundisho kwa wengine. Na taarifa ya Tume iletwe katika Bunge lako
tukufu kwa hatua zaidi.
KESI KUSIKILIZWA NA MAHAKIMU WASIO NA MAMLAKA
Mheshimiwa Spika,
Kwa
ujumla watuhumiwa wote wanaokamatwa wakisafirisha dawa za kulevya
hutakiwa kufunguliwa mashtaka chini ya kifungu 16(1)(b)(i) cha sheria ya
dawa ya kulevya.
Kosa
hili halina dhamana na husikilizwa na Mahakama Kuu peke yake. Hata
hivyo baadhi ya Mahakimu wamekuwa wakilisikiliza kesi hizo na wengine
kushirikiana na waendesha mashtaka hubadilisha hati ya mashtaka na
kufanya wawe na mamlaka ya kusikiliza kesi hizo. Mfano ni shauri la
Jamhuri dhidi ya Shirima (CC 433/2009).
Mheshimiwa Spika,
Katika
shauri hili Mtuhumiwa alikamatwa tarehe 02/05/2009 katika Bandari ya
Dar es salaam akiwa na kilo 1 ya heroine yenye thamani ya Tshs.
18,000,000/=….Tarehe 05/05/2009 alifikishwa Mahakamani na kufunguliwa
mashtaka chini ya kifungu cha 16(1)(b)(i) cha sheria ya dawa ya kulevya,
tarehe 9/05/2009 hati ya mashtaka ilibadilishwa na mashtaka kuwa chini
ya kifungu 12(d) ya sheria ya dawa za kulevya .
Tarehe
14/7/2009 aliamriwa kulipa faini ya Tshs. 4, 000,000. Ubadilishwaji wa
vifungu vya sheria katika hati ya mashtaka hulenga kuwasaidia watuhumiwa
washtakiwe na makosa madogo badala ya yale makubwa yenye adhabu kubwa
kisheria.
Mheshimiwa Spika,
Kifungu
cha 16(1)(b)(i) cha sheria ya dawa za kulevya kinataja kosa la dawa za
kulevya kuwa kosa ambalo halina dhamana. Hivyo waendesha mashtaka kwa
kushirikiana na watuhumiwa hupendelea kuwafungulia mashtaka madogo chini
ya kifungu cha 12(d) cha sheria ya dawa za kulevya.
Katika
kesi ambazo watuhumiwa walifunguliwa mashtaka chini ya vifungu ambavyo
haviendani na makosa yao halisi , Mahakama zimekuwa zikitoa adhabu ndogo
ya faini na kuwaachia huru! tena katika mazingira mengine kutoa hukumu
ndogo kuliko ambayo imeainishwa katika sheria.
MAPUNGUFU YA SHERIA
Mheshimiwa Spika,
Sheria ya kuzuia dawa za kulevya haina adhabu kwa mtu anayesafirisha au anayekutwa na kemikali bashirifu (Chemical precursors).
Kemikali
hizi ni muhimu sana katika kutengeza dawa za kulevya aina ya Heroin na
Cocaini, crystal-methamphetamine. Muathirika wa dawa
crystal-methamphetamine hawezi kutibika maishani mwake (Permanent Brain
Damage). Kwa sasa hivi kuna wimbi kubwa la uingizaji wa kemikali hizo
zinazoenda kuangamiza nguvu kazi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
Miongoni
mwa matukio ya uingizaji na usafirishaji wa kemikali hizo ni kesi ya
Saada Ally Kilongo aliyekamatwa uwanja wa ndege wa J.K. Nyerere akiwa na
10 kilo za Ephedrine. Nyingine ni kesi ya Agnes Gerald Delwaya
(Masogange) na mwenzake waliokamatwa Afrika Kusini wakiwa na kilo 150 za
Ephedrine.
Aidha,
Rumishaeli Mamkuu Shoo na mwenzake wamekamatwa kwenye Kiwanda cha
kutengeza Ephedrine nchini Kenya na tayari alikuwa na kilo hamsini (50)
za kemikali hizo. Hawa watu licha ya madhara makubwa waliolitelea Taifa,
wako mtaani wanapeta na kujipongeza!
Mheshimiwa Spika,
Kama
hatutarekebisha sheria mapema iwezekanavyo, tutajikuta tunakuwa na
kiwanda au viwanda vya kutengeneza dawa za kulevya hapa nchini. Hivyo,
wauzaji badala ya kuagiza dawa hizo nje ya nchi, wataanza kutengeneza
hapa na kuna taarifa kwamba pindi dawa za kulevya zinapokosekana
wafanyabiashara huuza kemikali hizo na watumiaji wanatengeza wenyewe na
kutumia.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na mapungufu yaliyojitokeza kama hoja yangu ilivyoeleza, naomba Serikali ifanye mambo yafuatayo:-
1:
Iunde Mahakama Maalumu, haraka iwezekanavyo itakayokuwa na jukumu la
kushughulikia kesi za dawa za kulevya tu kama ilivyo Mahakama ya
Biashara na iliyokuwa Mahakama ya Ardhi.
2: Ifanye marekebisho ya sheria ya dawa za kulevya kwa kuongeza makosa ya kusafirisha, kuuza au kukutwa na kemikali bashirifu
3:
Iundwe Tume ya kuchunguza baadhi ya watendaji wa Mahakama na Serikali
ambao kwa makusudi wamekuwa wakihujumu kesi za dawa za kulevya pamoja na
jitihada za Serikali katika kupambana na biashara hii haramu na kuleta
taarifa katika Bunge hili tukufu
4: Kiundwe haraka chombo huru chenye nguvu na mamlaka kamili kitakachokuwa na dhamana ya kupambana na dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Spika, Naomba kuwasilisha.
EPUKA MATUMIZI YA MADAWA YA KULEVYA NI HATARI, NINI MAONI YAKO?USISAHAU KULIKE UKURASA WETU WA FACEBOOK
- Get link
- X
- Other Apps
Comments
Post a Comment